Vatican News
Papa Francisko, Ijumaa, tarehe 11 januari 2019 amewatembelea watawa wa ndani kwenye Monasteri wa Vallegloria, Spello Papa Francisko, Ijumaa, tarehe 11 Januari 2019 amewatembelea watawa wa ndani kwenye Monasteri ya Vallegloria, Spello 

Papa awatembelea watawa wa Vallegloria, Spello!

Lengo la Baba Mtakatifu lilikuwa ni kuwatia shime watawa wa ndani katika wito na maisha yao ya sala na tafakuri, ili kushirikishana utajiri wa Fumbo la Ekaristi Takatifu pamoja na chakula. Itakumbukwa kwamba, watawa hawa wa ndani, kunako tarehe 25 Agosti 2016 walimtembelea Baba Mtakatifu mjini Vatican na kuwakabidhi Katiba ya Kitume “Vultum Dei Quaerere”

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa linawahitaji watawa ambao kimsingi ni mashuhuda na manabii wa matumaini. Hawa ni watu wasiokata tamaa licha ya kupungua kwa idadi ya miito duniani pamoja na kuongezeka kwa idadi ya watawa wazee; ni watu wanaokumbana na changamoto za ukwasi na hali ngumu ya kiuchumi; wanakodolewa macho na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine; ni watu wanaopambana na mchakato wa utamadunisho na mwelekeo wa mashirika ya kimataifa ili kupata utambulisho wao katika Makanisa mahalia: Watawa pia wanakabiliana na “ndago” ubinafsi bila kusahau changamoto za kijamii zinazobeza maisha ya kitawa.

Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 11 Januari 2019 amewatembelea watawa wa ndani wanaoishi kwenye Monasteri ya Vallegloria, huko Spello, Perugia, nchini Italia. Lengo la Baba Mtakatifu lilikuwa ni kuwatia shime watawa wa ndani katika wito na maisha yao ya sala na tafakuri, ili kushirikishana utajiri wa Fumbo la Ekaristi Takatifu pamoja na chakula. Itakumbukwa kwamba, watawa hawa wa ndani, kunako tarehe 25 Agosti 2016 walimtembelea Baba Mtakatifu mjini Vatican na kuwakabidhi Katiba ya Kitume “Vultum Dei Quaerere” Yaani “Kuutafuta Uso wa Mungu”  kwa niaba ya watawa wote wa ndani sehemu mbali mbali za dunia.

Tangu wakati huo, watawa hawa wameendeleza urafiki na uhusiano wa pekee na Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya Katibu wake muhtasi, Padre Yoannis Lahzi Gaid, kiasi hata cha kuhamasika kuwatembelea kwa faragha. Askofu Gualtiero Sigismondi wa Jimbo Katoliki la Foligno nchini Italia anakiri kwamba, Baba Mtakatifu Francisko alimgusia safari hii ya faragha kwenye Monasteri ya Vallegloria. Hii ilikuwa ni furaha ya pekee katika maadhimisho ya Kipindi cha Noeli kwa Mwaka 2018. Licha ya hali mbaya ya hewa pamoja na kuanguka kwa theluji, lakini Baba Mtakatifu Francisko ametimiza ndoto yake ya kwenda kuwatazama na kuwasalimia watawa hawa wa ndani! Baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Baba Mtakatifu alizungumza na kubadilishana mawazo na watawa hawa na baadaye kupata nao chakula cha mchana! Kwa watawa wa Monasteri ya Vallegloria, kwao Baba Mtakatifu amekuwa ni zawadi kubwa ya Noeli kwa Mwaka 2018.

Itakumbukwa kwamba, Katiba ya Kitume "Vultum Dei Quaerere", yaani "Kuutafuta Uso wa Mungu” Papa anabainisha mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa na wamonaki katika maisha na utume wao, ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo, tayari kutoa ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Anasema, kuna haja ya kudumisha majiundo makini ya awali na endelevu; umuhimu wa tafakari ya Neno la Mungu; kuzingatia vigezo muhimu kwa Jumuiya ya Kimonaki kuweza kujitegemea pamoja na uwezekano wa kuunda Shirikisho la Wamonaki ndani ya Kanisa. Haya ni kati ya mambo ambayo Baba Mtakatifu Francisko anayapatia kipaumbele cha pekee katika Katiba ya Kitume “Vultum Dei Quaerere” Yaani “Kuutafuta Uso wa Mungu” Waraka ambao utakuwa unafupishwa kwa herufi “VDQ”, uliotiwa sahihi na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani hapo tarehe 29 Juni 2016 kwa ajili ya Wamonaki wa Mashirika ya Taamuli.

Papa: Watawa wa Ndani
12 January 2019, 16:11