Papa Francisko: Bara la Asia halina budi kuvumbua njia mpya za kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili. Papa Francisko: Bara la Asia halina budi kuvumbua njia mpya za kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili. 

Papa: Vumbueni njia mpya za kutangaza na kushuhudia Injili!

Bara la Asia limebarikiwa kuwa na utajiri na amana ya dini, lugha na tamaduni mbali mbali. Jambo la msingi kwa Kanisa ni kuhakikisha kwamba, linaendeleza uwajibikaji wa jumla katika kulinda na kudumisha umoja na mafungamano ya imani ya Kanisa. Ni wajibu wa Kanisa kuendelea kuvumbua njia mpya zitakazowawezesha waamini kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kati ya watu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia, FABC, kuanzia tarehe 15-18 Januari 2019 linafanya mkutano unaowashirikisha wenyeviti wa Tume za Mafundisho Tanzu ya Kanisa kutoka katika Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Asia. Kardinali Luis Francisco Ladaria, anaongoza ujumbe kutoka katika Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa huko mjini Bankkok, nchini Thailand. Katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia ujumbe wa matashi mema, kama kielelezo cha uwepo wake wa kidugu kati yao, wanapojadili mambo msingi katika maisha na utume wa Kanisa!

Baba Mtakatifu anasema, Bara la Asia limebarikiwa kuwa na utajiri na amana ya dini, lugha na tamaduni mbali mbali. Jambo la msingi kwa Kanisa ni kuhakikisha kwamba, linaendeleza uwajibikaji wa jumla katika kulinda na kudumisha umoja na mafungamano ya imani ya Kanisa Katoliki. Ni wajibu wa Kanisa kuendelea kuvumbua njia mpya zitakazowawezesha waamini kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kati ya watu. Kanisa lisimame kidete kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo.

Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, katika Waraka wake wa kitume, “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili”; anakazia mabadiliko ya ari na umisionari wa Kanisa. Anahimiza Umuhimu wa Jumuiya za Kikristo katika kukabiliana na changamoto mamboleo; anawataka waamini kushiriki kikamilifu katika dhamana na utume wa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa: Waamini wawe na mwelekeo wa uinjilishaji kijamii pamoja na kukuza ari na mwamko wa wainjilishaji waliojazwa nguvu na mapaji Roho Mtakatifu ili kutangaza upendo na huruma ya Kristo Yesu inayookoa! Baba Mtakatifu analitaka Kanisa zima kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili.

Baba Mtakatifu aendelea kufafanua kwamba, uwepo na ushiriki wa wajumbe kutoka Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa unapania kuimarisha na kudumisha sera na mikakati ya shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Mama Kanisa kwa njia ya Tume za Mafundisho Tanzu ya Kanisa kutoka katika Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia. Hii pia ni fursa ya kudumisha umoja na ushirikiano wa kidugu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, mkutano huu, utaweza kushughulia changamoto changamani zinazoendelea kujitokeza katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu utangazaji na ushuhuda wa Injili ya Kristo, muhimu sana kwa familia ya Mungu Barani Asia. Mwishoni, Baba Mtakatifu anapenda kuwapatia wajumbe wote wa mkutano huu, baraka zake za kitume!

Papa: Maaskofu Asia

 

 

15 January 2019, 13:48