Tafuta

Vatican News
Papa Francisko asikitishwa sana na vitendo vya kigaidi nchini Colombia. Papa Francisko asikitishwa sana na vitendo vya kigaidi nchini Colombia.  (AFP or licensors)

Papa Francisko asikitishwa na vitendo vya kigaidi Colombia!

Papa Francisko ameonesha masikitiko makubwa, kutokana na vitendo vya kigaidi vilivyotokea hivi karibuni, kwenye Chuo cha Polisi Kitaifa huko, Bogota, nchini Colombia na kusababisha watu 21 kupoteza maisha yao na wengine 50 kujeruhiwa vibaya. Tukio hili la kigaidi limezua hofu na mashaka ya kuzuka tena kwa vitendo vya kigaidi vilivyositishwa kunako mwaka 2016.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana ameelezea masikitiko yake makubwa, kutokana na vitendo vya kigaidi vilivyotokea hivi karibuni, kwenye Chuo cha Polisi Kitaifa huko, Bogota, nchini Colombia na kusababisha watu 21 kupoteza maisha yao na wengine 50 kujeruhiwa vibaya. Tukio hili la kigaidi limezua hofu na mashaka ya kuzuka tena kwa vitendo vya kigaidi vilivyositishwa kunako mwaka 2016, baada ya Serikali ya Colombia kutiliana sahihi mkataba wa amani na vikosi vya waasi nchini humo.

Mkataba wa amani kati ya serikali na kikundi cha waasi kimsingi ni suala la kisiasa, lakini ikumbukwe kwamba, amani inapaswa kujengeka kutoka katika akili na nyoyo za watu, kwa kujikita katika toba na wongofu wa ndani; msamaha na upatanisho wa kweli. Katika mwelekeo kama huu, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini humo kunako mwaka 2017 ilikuwa ni zawadi kubwa katika kuimarisha mchakato wa amani ya kweli nchini Colombia! Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikisha wale wote walioguswa na kutikiswa na shambulizi hili, uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala. Anaendelea kusali na kuombea amani nchini Colombia.

Papa: Mauaji Colombia
21 January 2019, 08:32