Papa Francisko: tarehe 24 Januari 2019, UNESCO inaadhimisha Siku ya Kwanza ya Elimu Duniani kwa Mwaka 2019 Papa Francisko: tarehe 24 Januari 2019, UNESCO inaadhimisha Siku ya Kwanza ya Elimu Duniani kwa Mwaka 2019 

Papa Francisko: UNESCO: Siku ya Kwanza ya Elimu Duniani 2019

Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii, kulihamasisha Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO kukuza na kudumisha juhudi hizi, ili amani iweze kutawale duniani kwa njia ya elimu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, watu wote wapate fursa ya kupata elimu ambayo kimsingi inapaswa kuwa fungamani na huru dhidi ya ukoloni wa kiitikadi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Elimu ni kati ya haki msingi za kibinadamu, ni sehemu ya mafao ya wengi na inawajibisha. Ni kutokana na umuhimu wa elimu katika jamii, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, mwezi Desemba 2018 likaadhimia kuanzishwa kwa Siku ya Elimu Duniani, itakayokuwa inasherehekewa kila mwaka ifikapo tarehe 24 Januari. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe, 20 Januari 2019 amekumbusha kwamba, kwa mara ya kwanza tarehe 24 Januari 2019, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Elimu Duniani.

Lengo la Umoja wa Mataifa ni kubainisha na kuendeleza dhamana ya elimu kama sehemu ya mchakato wa maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu: kiutu na kijamii. Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii, kulihamasisha Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO kukuza na kudumisha juhudi hizi, ili amani iweze kutawala duniani kwa njia ya elimu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, watu wote watakuwa fursa ya kupata elimu ambayo kimsingi inapaswa kuwa fungamani na huru dhidi ya ukoloni wa kiitikadi. Baba Mtakatifu anawatakia waalimu wote kazi njema katika kurithisha ujuzi, maarifa na stadi za maisha katika jamii!

Hivi karibuni, Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu amegusia kuhusu Katiba ya Kitume “Veritatis gaudium” yaani “Furaha ya ukweli” iliyotolewa hivi karibuni na Papa Francisko ambamo anatoa vigezo muhimu vinavyopaswa kuzingatiwa katika sekta ya elimu, kwani lengo ni kujenga na kukuza umoja na udugu, upendo na mshikamano, daima maskini wakipewa kipaumbele cha kwanza! Hii ndiyo dhamana ya umissionari wa Kanisa linatoka kifua mbele ili kuinjilisha na kutamadunisha mintarafu furaha ya ukweli wa Kikristo! Kigezo cha pili ni majadiliano katika ukweli na uwazi mintarafu mwanga wa Injili na Mafundisho ya Kanisa ili kukuza na kudumisha utamaduni wa watu kukutana.

Kigezo cha tatu ni mwingiliano makini wa masomo mbali mbali yanayotolewa na vyuo vikuu pamoja na taasisi za elimu ya juu kwa kuzingatia ubunifu kadiri ya mwanga wa Ufunuo. Majiundo, tafiti, mbinu za ufundishaji na maudhui yanayotolewa yanapaswa kuzingatia Ufunuo na Utume wa Kanisa katika dhamana ya uinjilishaji. Mkazo unaotolewa na Mababa wa Kanisa katika mfumo wa elimu unajikita katika mambo makuu manne yaani: umoja wa kisayansi, mawasiliano ya utakatifu, maisha adili na umwilishaji wa upendo katika maisha ya watu mambo yanayobubujika kutoka katika Neno la Mungu, vinginevyo, sayansi haina mizizi na wala kamwe haiwezi kuacha kumbu kumbu hai katika akili na nyoyo za vijana wa kizazi kipya! Sayansi na utakatifu ni sawa na “uji kwa mgonjwa”.

Kigezo cha nne ni kuunda mtandao wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu ili kuweza kufanya upembuzi yakinifu katika shida, changamoto na hatimaye kuibua suluhu ya mambo yote haya mintarafu mwanga wa Injili, kwa kuwa na mradi wa pamoja unaotekelezwa na Kanisa moja, takatifu, katoliki na la mitume! Lengo ni kufahamu matatizo haya na hatimaye, kuyapatia maana na ufumbuzi wake kadiri ya mwanga wa Injili, Mapokeo ya Kanisa Uinjilishaji na Utamadunisho. Maboresho yote haya yanapania kutangaza ukweli wa Injili bila kubezwa ukweli wa mambo na mafao yake kwa wengi.

Baba Mtakatifu Francisko, akihutubia Mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa mnamo 2015 alisema: haki elimu, ni haki inayopaswa kuzingatiwa kwanza kabisa kutoka kwenye familia na kwa jamii za kidini katika kuchangia elimu na malezi bora ya watoto na vijana. Huu utakuwa msingi wa utekelezaji wa Ajenda ya maendeleo endelevu kufikia 2030. Ili Jumuiya ya Kimataifa iweze kufanikisha wajibu huo ni lazima kujega utamaduni wa watu kukutana. Utamaduni huu unapaswa ujengeke katika heshima, thamani kwa wengine, majadiliano, usikilizaji, na mshikamano, bila kudharau utambulisho wa mwingine. Hatua hii itakuwa ni nyenzo ya kupiga vita ghasia, ubaguzi, umaskini, unyonyaji, na uonevu.

Papa: Siku ya Elimu Duniani 2019

 

 

22 January 2019, 09:42