Tafuta

Vatican News
Kiini cha Ubatizo wa Bwana: Uhusiano wa Kristo Yesu na Watu; Uhusiano wake na Baba yake wa mbinguni! Kiini cha Ubatizo wa Bwana: Uhusiano wa Kristo Yesu na Watu; Uhusiano wake na Baba yake wa mbinguni!  (Vatican Media)

Ubatizo wa Bwana: Kielelezo cha mshikamano na utume wa Yesu!

Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Kristo Yesu, alijitwalia hali ya ubinadamu, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika dhambi na mauti. Katika Siku kuu ya Ubatizo wa Bwana, Yesu anajifunua, kama chombo cha huruma na maondoleo ya dhambi! Yesu anaungana na ndugu zake wadhambi wanaotubu na kutaka kumwongokea Mwenyezi Mungu, kiini cha ufunuo wa utume wake hapa duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya maadhisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Siku kuu ya Ubatizo wa Bwana kwenye Kikanisa cha Sistina ambako ametoa pia ubatizo kwa watoto wachanga 27, akiwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 13 Januari 2019, amewaongoza waamini kwa tafakari juu ya Siku kuu ya Ubatizo wa Bwana, inayofunga rasmi Kipindi cha Liturujia ya Noeli, tayari kuanza Kipindi cha Mwaka wa kawaida wa Kanisa. Kiini cha Liturujia ya Ubatizo wa Bwana ni kuonesha uhusiano wa dhati kati ya Kristo Yesu na watu; pamoja na uhusiano wake na Baba yake wa mbinguni!

Katika Ubatizo wa toba uletao ondoleo la dhambi, uliotolewa na Yohane Mbatizaji kule mtoni Yordani, Mwinjili Luka anafafanua jinsi ambavyo Kristo Yesu, kabla ya kubatizwa, alivyojiunga na umati mkubwa wa watu waliomwendea Yohane Mbatizaji, ili wapate kubatizwa, kielelezo cha mshikamano wa Kristo Yesu na binadamu mdhambi katika mambo yote akawa sawa na binadamu, isipokuwa hakutenda dhambi! Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai anaonesha utakatifu, huruma na neema ya Mungu.

Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Kristo Yesu, alijitwalia hali ya ubinadamu, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Katika Siku kuu ya Ubatizo wa Bwana, Yesu anajifunua, kama chombo cha huruma na maondoleo ya dhambi! Yesu anaungana na ndugu zake wadhambi wanaotubu na kutaka kumwongokea Mwenyezi Mungu, kiini cha ufunuo wa utume wake hapa duniani. Kwa njia hii Yesu, anaungana na watu wanaomwomba Yohane Mbatizaji, Ubatizo wa toba ili kuleta upyaisho wa maisha ya kiroho. Na kwa kushukiwa na Roho Mtakatifu kwa mfano wa kiwiliwili kama hua, Yesu anaanzisha mbingu na dunia mpya na kuwafanya wale wote wanaomwamini na kumpokea kuwa ni viumbe wapya.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, wale wote waliozaliwa kwa: Maji, Roho Mtakatifu na Neno wanafanyika watoto wapendwa wa Mungu, ambao Mwenyezi Mungu anapendezwa nao! Huu ni upendo ambao waamini wameupata wakati walipopokea Sakramenti ya Ubatizo na unaendelea kuwaka nyoyoni mwao, lakini, upendo hauna budi kuboreshwa kwa njia ya sala na matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Mwinjili Luka anamwonesha Kristo Yesu baada ya kuungana na umati mkubwa wa watu na kubatizwa, akiwa amezama katika sala, kielelezo makini cha muungano na Baba yake wa mbinguni, tayari kuanza maisha ya hadhara, kama mjumbe wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu ulimwenguni! Kristo Yesu kwa kutekeleza dhamana na utume wake, daima anaonesha umoja wa Fumbo la Utatu Mtakatifu. Hii ndiyo dhamana, maisha na utume wa Kanisa; hata kwa kila mwamini mmoja mmoja, kuwa mwaminifu na anayezaa matunda kwa kuendelea kushikamana na Kristo Yesu katika maisha yake!

Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, hii ni changamoto ya kuendeleza mchakato wa maisha ya sala, uinjilishaji na utume kama njia ya ushuhuda amini wa maisha ya Kikristo, tofauti kabisa na mipango ya binadamu, daima kwa kutenda mintarafu mpango na mtindo wa Mungu. Siku kuu ya Ubatizo wa Bwana ni nafasi pia ya kumshukuru Mungu kwa kuzaliwa upya katika Roho Mtakatifu, changamoto na mwaliko wa kuendelea kuwa waaminifu katika ahadi za Ubatizo; zinazomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku. Kristo Yesu amewakomboa wanadamu si kwa sababu ya matendo yao mema, bali ni kwa njia ya huruma na upendo wa Mungu kwa mwanadamu. Hii ni changamoto kwa waamini kuwa watu wema na wenye huruma kwa jirani zao. Bikira Maria, Mama wa huruma, awe kiongozi na mfano wao bora wa kuigwa!

Baada ya Siku kuu ya Ubatizo wa Bwana, Kanisa linaanza Kipindi cha Kawaida cha Mwaka wa Kanisa, kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, waamini wanamwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kuwaongoza, lakini, hawana budi kumwomba kwanza, ili awawezeshe kumwilisha upendo katika yale yote wanayoyatenda kila siku ya maisha yao. Papa amewataka waamini kuadhimisha kumbu kumbu za Siku yao kuzaliwa kwa: Maji, Roho Mtakatifu na Neno, yaani Siku ya Ubatizo wao kwani hii ni siku muhimu sana katika imani.

Papa: Sala: Ubatizo
13 January 2019, 14:11