Tafuta

Papa Francisko: Katika Sherehe ya Ubatizo wa Bwana anatarajiwa kutoa Sakramenti ya Ubatizo kwa watoto wadogo! Papa Francisko: Katika Sherehe ya Ubatizo wa Bwana anatarajiwa kutoa Sakramenti ya Ubatizo kwa watoto wadogo! 

Papa Francisko: Sherehe ya Ubatizo wa Bwana, 2019

Maadhimisho ya Sherehe ya Ubatizo wa Bwana, yanafunga rasmi shamra shamra zote za Liturujia ya Kipindi cha Noeli. Katika Ibada hii itakayoadhimishwa kwenye Kikanisa cha Sistina, Baba Mtakatifu anatarajiwa kutoa Sakramenti ya Ubatizo kwa watoto walioandaliwa, ili waweze kuzaliwa upya kwa “Maji na Roho Mtakatifu” tayari kushiriki: Ufalme, Ukuhani na Unabii wa Kristo Yesu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili, tarehe 13 Januari 2019 majira ya saa 3: 30 Asubuhi kwa saa za Ulaya, anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Maadhimisho ya Sherehe ya Ubatizo wa Bwana, inayofunga rasmi shamra shamra zote za Liturujia ya Kipindi cha Noeli. Katika Ibada hii itakayoadhimishwa kwenye Kikanisa cha Sistina, Baba Mtakatifu anatarajiwa kutoa Sakramenti ya Ubatizo kwa watoto walioandaliwa, ili waweze kuzaliwa upya kwa “Maji na Roho Mtakatifu” tayari kushiriki: Ufalme, Ukuhani na Unabii wa Kristo Yesu. Baadaye majira ya mchana ataongoza Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Sakramenti ya Ubatizo ni msingi wa maisha yote ya Kikristo, lango la kuingilia katika maisha ya kiroho na kwa njia hii, mwamini anaweza kupata Sakramenti nyingine zinazoadhimishwa na Mama Kanisa. Ni kutokana na umuhimu huu, Baba Mtakatifu Francisko anawahimiza waamini kuhakikisha kwamba, wanaadhimisha Siku kuu ya Ubatizo wao, alama ya kufa na kufufuka na Kristo Yesu, kwa njia ya Maji ya Ubatizo na Roho Mtakatifu na hivyo kuwa ni viumbe wapya, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, sanjari na ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika haki, amani, upendo na mshikamano.

Sakramenti ya Ubatizo inachota utajiri wake kutoka katika Fumbo la Pasaka ndiyo maana, Baba Mtakatifu anasema, hii ni Sakramenti ya imani inayomwezesha mwamini kuingia katika maisha ya kiimani, kwa kuwekwa huru dhidi ya mitego ya Shetani. Kuhusu Ubatizo wa Watoto wachanga, zoezi litakalofanywa na Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku kuu ya Ubatizo wa Bwana, linapania kuwasaidia watoto hawa kuzaliwa upya kwa “Maji na Roho Mtakatifu” ili kuwaweka huru dhidi ya nguvu za giza na hatimaye, kuingizwa katika utawala wa uhuru wa watoto wa Mungu.

Ikumbukwe kwamba, imani ni kipaji cha bure kinachotolewa na Mwenyezi Mungu, hali inayodhihirishwa kwa namna ya pekee katika ubatizo wa watoto wachanga. Baba Mtakatifu Francisko anawataka wazazi, walezi na wasimamizi wa Ubatizo kushiriki kikamilifu katika kuwarithisha vyema watoto wao imani inayopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo na Kanisa lake, kwa njia ya ushuhuda wa maisha yanayofumbatwa katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.

Baba Mtakatifu anasema, ni kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, waamini wanaitwa kuwa Wakristo, kwa kushirikishwa katika maisha na utume wa Kristo yaani: Ufalme, Unabii na Ukuhani wake tayari kujenga na kudumisha Fumbo la Mwili wake, yaani Kanisa! Baba Mtakatifu anapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya imani na anawaalika waamini kumwomba Roho Mtakatifu nguvu ya kuweza kuwa kweli ni mashuhuda amini wa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Papa: Ubatizo wa Bwana
10 January 2019, 09:03