Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Sherehe ya Ubatizo wa Bwana: Anawaalika waamini kujiandaa vyema ili kugundua tena neema ya utakaso inayobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo. Papa Francisko: Sherehe ya Ubatizo wa Bwana: Anawaalika waamini kujiandaa vyema ili kugundua tena neema ya utakaso inayobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo.  (AFP or licensors)

Papa Francisko: Sakramenti ya Ubatizo: Ukuhani, Ufalme na Unabii

Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo waamini wanaitwa kuwa Wakristo, kwa kushirikishwa katika maisha na utume wa Kristo yaani: Ufalme, Unabii na Ukuhani wake tayari kujenga Fumbo la Mwili wake, yaani Kanisa! Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwomba Roho Mtakatifu nguvu ya kuweza kuwa kweli ni mashuhuda amini wa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi yake kuhusu Sala ya Baba Yetu, kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Paulo VI amewakumbusha waamini kwamba, Jumapili, tarehe 13 Januari 2019, Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Ubatizo wa Bwana, inayohitimisha Kipindi cha Liturujia wakati wa Noeli, changamoto na mwaliko wa kugundua tena neema ya utakaso ambao waamini walijipatia kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo.

Baba Mtakatifu anasema, ni kwa njia ya Sakramenti hii, waamini wanaitwa kuwa Wakristo, kwa kushirikishwa katika maisha na utume wa Kristo yaani: Ufalme, Unabii na Ukuhani wake tayari kujenga na kudumisha Fumbo la Mwili wake, yaani Kanisa! Baba Mtakatifu anapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya imani na anawaalika waamini kumwomba Roho Mtakatifu nguvu ya kuweza kuwa kweli ni mashuhuda amini wa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Mwanzo wa Mwaka Mpya wa 2019 ni wakati muafaka wa kutambua na kujikita katika nguvu ya Sala, ili kuweza kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu kwa kufuata Sala ya Baba Yetu, ili kuwa na uhakika wa kupata mambo mema na muhimu katika maisha, lakini kwanza kabisa kwa kujiaminisha kwa wema na upendo wa Mungu katika maisha. Sala inapaswa kukita mizizi yake katika imani, matumaini na udumifu, kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, atawakirimia waja wake, kwa wakati muafaka! Waamini waendelee kuunda mazingira ya sala, huku wakijitahidi kuomba katika ukweli na haki, kwani iko siku isiyokuwa na jina, Mwenyezi Mungu atawakirimia furaha na amani inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Watambue kwamba, Kristo Yesu ni hema la Mungu kati ya watu wake, wamkimbilia katika: furaha, shida na magumu, ili hatimaye, aweze kuwakirimia maisha na furaha ya uzima wa milele!

Ubatizo wa Bwana
09 January 2019, 12:56