Papa Francisko: Sala ya Baba Yetu inajikita katika: Imani, Matumaini na Udumifu. Papa Francisko: Sala ya Baba Yetu inajikita katika: Imani, Matumaini na Udumifu. 

Papa Francisko: Sala ya Baba Yetu: Imani, Matumaini & Udumifu

Papa Francisko amekazaia kwa namna ya pekee, umuhimu wa kudumu katika sala, kwa kusema, “Ombeni nanyi mtapewa”. Tukio la Yesu kugeuka sura mbele ya wanafunzi wake, lilionesha utukufu wa Mwana wa Mungu aliyezama kabisa katika sala, huku akisukumwa na nguvu ya Roho Mtakatifu, iliyokuwa dira na mwongozo wa maisha yake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mwinjili Luka anaonesha utajiri mkubwa wa mazingira ya maisha ya Sala yaliyomzunguka Kristo Yesu, tangu mwanzo kabisa wa maisha yake hapa duniani! Ni katika Injili hii, Mama Kanisa anachota amana na utajiri wa Sala ya Kanisa kila siku yaani: Utenzi wa Zakaria “Benedictus”, Utenzi wa Bikira Maria, “Magnificat” na Utenzi wa Simeoni, “Nunc dimittis”. Vyote hivi ni viashiria kwamba, kwa hakika Kristo Yesu alikuwa ni mtu wa sala!

Hii ni sehemu ya mwendelezo wa Katekesi kuhusu Sala ya Baba Yetu, au "Sala ya Bwana" muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake, kama ilivyochambuliwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano, tarehe 9 Januari 2019 kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Paulo VI, ulioko mjini Vatican, na kukazia kwa namna ya pekee, umuhimu wa kudumu katika sala, kwa kusema, “Ombeni nanyi mtapewa”. Tukio la Yesu kugeuka sura mbele ya wanafunzi wake, lilionesha utukufu wa Mwana wa Mungu aliyezama kabisa katika sala, huku akisukumwa na nguvu ya Roho Mtakatifu, iliyokuwa dira na mwongozo wa maisha yake na utume wake.

Yesu alisali alipokuwa anabatizwa Mtoni Yordani; alijitenga na umati, akasali kwa Baba yake wa mbinguni kabla ya kufanya maamuzi muhimu katika maisha na utume wake na mara nyingi alibaki katika hali ya upweke na daima aliwaambia wafuasi wake kukesha na kusali ili Shetani asije akawapepeta kama vile ngano na kwamba, anamwombea Mtume Petro, ili atakapoongoka, awaimarishe ndugu zake. Kwa hakika, Mtakatifu Petro, baadaye kidogo alimkana Kristo Yesu mara tatu, hali ambayo inaonesha kwamba, Kristo Yesu anawafahamu vyema waja wake na kwamba, anawakumbuka na kuwaombea, ili kila mwamini aweze kuimarika katika imani, kwani anatambua fika mahitaji yao, hali inayowapatia waamini ujasiri wa kusonga mbele kwa kutambua kwamba, hata sasa Kristo Yesu anaendelea kuwaombea kwa Baba yake wa mbinguni!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hata katika mateso na hatimaye kifo cha Kristo Yesu, aliendelea kujikita katika sala na utulivu wa ndani; kiasi hata cha kupata nguvu ya kuwafariji wanawake wa Israeli waliokuwa wanamlilia; akasali na kuwaombea watesi wake, kwani walikuwa hawajui wanalolitenda na hatimaye, akajiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu kwa kuiweka roho yake mikononi mwake. Sala ya Kristo Yesu inaponya ghadhabu na tamaa ya kutaka kulipiza kisasi; inampatanisha mwamini na mtesi wake; inampatanisha mwamini na fumbo la kifo, adui mkubwa kuliko adui mwingine awaye yote!

Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, ni Mwinjili Luka anaonesha ile kiu ya Mitume wa Yesu kutaka wafundishwe kusali, kwani daima walimshuhudia akisali, hata wao pia wakataka kujifunza kusali vyema, kwa kuwapatia kielelezo cha muhtasari wa maneno ambayo wangetumia wakati wakielekeza Sala yao mbele ya Mwenyezi Mungu na huo ndio ukawa ni mwanzo wa Sala ya Baba Yetu, kwa kutambua kwamba, mbinguni, wanaye Baba yao mpendwa, anayewakirimia imani na matumaini katika sala; anayewataka kudumu katika sala bila kuchoka kama ilivyokuwa kwa rafiki mwenye saburi anayesimuliwa na Mwinjili Luka, 11: 9; Baba mwenye huruma anayemkirimia mwanaye mema ya mbinguni na kamwe hawezi kumpatia nyoka badala ya samaki au jiwe badala ya mkate.

Hii inatokana na ukweli kwamba, Baba wa mbinguni ni mwema na mtakatifu na kamwe hawezi kuwasahau watoto wake wanaoteseka hapa bondeni kwenye machozi! Lakini, Baba Mtakatifu anaonya kwamba, si wakati wote ambao waamini wamemkimbilia Mwenyezi Mungu kwa sala na maombi wakakirimiwa kile walichoomba. Lakini, hata katika mazingira kama haya, waamini wanapaswa kudumu katika sala, wakikesha na kuomba, kwani sala ni chachu ya mageuzi katika moyo na maisha ya mwanadamu. Yesu amewaahidia kuwapatia Roho Mtakatifu wale wote wanaomkimbilia kwa sala na maombi!

Baba Mtakatifu anasema, Mwenyezi Mungu kwa hakika atajibu sala na maombi ya waja wake kwa wakati muafaka, hata kama ni safari nzima ya maisha, lakini iko siku, atawaonjesha waja wake, “cheche za furaha” pia atawakirimia haki. Waamini waendelee kusali daima kwani iko siku ushindi utapatikana dhidi ya upweke hasi na hali ya kukata tamaa katika maisha. Mwanadamu daima ni hujaji na ulimwengu unasonga mbele, kumbe, sala inapaswa kuwa ni dira na mwongozo hadi dakika ya mwisho wa maisha, na huko Baba mwema anawasubiri kuwapokea na kuwakumbatia kwa moyo mkunjufu! Huyu ndiye Baba wa Mbinguni, ambaye, waamini wanamkimbilia kwa njia ya sala!

Sala ya Baba Yetu
09 January 2019, 13:36