Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anawapongeza vijana waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kufanikisha maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani 2019, nchini Panama Papa Francisko anawapongeza vijana waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kufanikisha maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani 2019, nchini Panama 

Papa Francisko awapongeza vijana kwa sadaka na majitoleo yao!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, mapungufu ya kibinadamu hayakuwa ni kikwazo kikubwa cha kushindwa kutoa huduma, bali wameonesha ujasiri wa hali ya juu, changamoto kwa sasa ni kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kurekebisha vilema na mapungufu yao kwa mwanga wa upendo na huruma ya Mungu, tayari kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Takwimu rasmi kutoka katika maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani, yaliyohitimishwa huko nchini Panama, Jumapili tarehe 27 Januari 2019 zinaonesha kwamba kulikuwepo na Maaskofu 450, Mapadre 2, 250. Watu wa kujitolea 19, 500 pamoja na waandishi wa habari 2, 500 kutoka sehemu mbali mbali za dunia waliohakikisha kwamba, ujumbe wa Baba Mtakatifu kwa vijana wa kizazi kipya unawafikia watu wengi zaidi.

Kabla ya kuondoka na kuanza safari ya kurejea mjini Vatican, Baba Mtakatifu Francisko alipata nafasi ya kusikiliza shuhuda kutoka kwa vijana waliojisadaka kwa ajili ya huduma katika maadhimisho haya na kuwapongeza kwa kushikamana katika huduma kwa jirani zao, iliowezesha kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hiki ni kielelezo cha upendo wa hali ya juu kama unavyofafanuliwa na Kristo Yesu! Mapungufu ya kibinadamu hayakuwa ni kikwazo kikubwa cha kushindwa kutoa huduma, bali wameonesha ujasiri wa hali ya juu, changamoto kwa sasa ni kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kurekebisha vilema na mapungufu yao kwa mwanga wa upendo na huruma ya Mungu, tayari kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa.

Vijana wanapoanguka dhambini, wawe na ujasiri wa kusimama tena kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho na kusonga mbele. Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo, daima yuko tayari kusamehe! Huduma na utume wa uinjilishaji vipewe kipaumble cha kwanza na vijana! Vijana wametekeleza dhamana na wajibu wao kwa umakini mkubwa, kwa furaha, kiasi kwamba, sala na kazi vikawa ni sehemu muhimu sana ya utambulisho wao wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani. Sala inawaunganisha vijana na familia kubwa ya watakatifu wa Mungu, ili kupambana na hatimaye, kushinda.

Dhamana na utume huu unapaswa kuendelezwa, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza, ili kuwaonjesha wengine matumaini. Baba Mtakatifu anawapongeza vijana waliojinyima mambo mengi katika maisha, ili kupata fedha ya kuwawezesha kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani. Nia na nidhamu kama hii, inawawezesha vijana kuwa na ujasiri, kukua na kukomaa na hatimaye, kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa ukarimu unaobubujika kutoka kwa Mungu. Vijana kwa njia ya majitoleo na sadaka yao, wameweza kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo! Huu ni ushuhuda wanaopaswa pia kuwashirikisha vijana wenzao, ili kupyaisha uso wa nchi. Vijana wahakikishe kwamba, ushuhuda wa imani, matumaini na mapendo unawafikia watu wengi zaidi bila kuona aibu. Mwishoni, wamesali kwa ajili kuwakumbuka na kuwaombea ndugu, jamaa, marafiki na wale wote wanaodhani kuwa ni adui zao!

Papa: Vijana Kujitolea
28 January 2019, 14:36