Tafuta

Papa Francisko anawataka Maaskofu na Mapadre kuwa karibu zaidi na vijana kwa sababu wao ni amana na utajiri wa Kanisa. Papa Francisko anawataka Maaskofu na Mapadre kuwa karibu zaidi na vijana kwa sababu wao ni amana na utajiri wa Kanisa. 

Papa Francisko: Vijana ni amana na utajiri wa Kanisa wasikilizwe

Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini kujenga mazingira yatakayoziwezesha jumuiya zao kupyaisha sura na maisha ya Kanisa; kuwa kweli ni chemchemi ya furaha ya Injili na mahali pa mshikamano wa upendo na ukarimu. Jumuiya ziwe ni mahali pa kuonja na kushirikishana huruma na upendo wa Mungu katika maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi yake, Jumatano tarehe 30 Januari 2019 amewahimiza Maaskofu na Mapadre kufuatilia kwa ukaribu na umakini mkubwa maadhimisho ya Siku za Vijana Duniani, ili vijana waweze kujisikia kuwa ni sehemu ya maisha na utume wa Kanisa. Maaskofu waoneshe mshikamano wa upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii na wajitahidi kuwa karibu sana na waamini wao, ili kuchota nguvu na ari mpya katika maisha na utume wao.

Baba Mtakatifu amewakumbusha waamini kwamba, maadhimisho ya Siku ya XXXV Duniani kwa Mwaka 2022 yatafanyikia Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno. Amewapongeza kwa namna ya pekee kabisa vijana kutoka Ufaransa na Poland, aliobahatika kukutana na kuongea nao kwa karibu zaidi. Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani imekuwa ni nafasi ya pekee kuweza kukutana na kuzungumza na vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu anawashukuru waamini na watu wote wenye mapenzi mema waliojisadaka kwa ajili ya kuombea ufanisi wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani. Hili ni tukio muhimu sana kwa maisha na utume wa Kanisa; ni mahali pa kushirikishana furaha ya Injili, ari na mwamko wa imani; pamoja na kufurahia zawadi ya maisha ya ujana.

Kwa mwaka huu, vijana wametafakari maisha yao kwa mwanga wa maisha na utume wa Bikira Maria katika historia nzima ya ukombozi, ambaye kwa kukubali kwake kuwa Mama wa Mungu, ameweza kuleta mabadiliko makubwa katika historia ya mwanadamu. Baba Mtakatifu anawataka waamini kujenga mazingira yatakayoziwezesha jumuiya zao kupyaisha sura na maisha ya Kanisa; kuwa kweli ni chemchemi ya furaha ya Injili na mahali pa mshikamano wa upendo na ukarimu. Jumuiya ziwe ni mahali pa kuonja na kushirikishana huruma na upendo wa Mungu katika maisha. Mwishoni Baba Mtakatifu amekumbusha kwamba, tarehe 31 Januari, Mama Kanisa anaadhimisha Kumbu kumbu ya Mtakatifu Yohane Bosco, aliyejisadaka kwa ajili ya utume kwa vijana. Baba Mtakatifu anasema, elimu bora, malezi makini ya kiroho na kiutu ni muhimu sana kwa vijana wa kizazi kipya.

Papa: Siku za Vijana
30 January 2019, 15:41