Papa Francisko: Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani ni muhimu sana katika hija ya maisha na utume wa Kanisa! Papa Francisko: Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani ni muhimu sana katika hija ya maisha na utume wa Kanisa! 

Siku ya Vijana Duniani ni muhimu kwa maisha na utume wa Kanisa!

Kuanzia tarehe 22 - 27 Januari 2019 kunafanyika maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani huko Panama ambayo yanaongozwa na kauli mbiu “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; iwe kwangu kama ulivyosema”. Lk. 1:38. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kusali kwa ajili ya kuombea tukio hili muhimu katika hija ya maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe 20 Januari 2019, amewajulisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kwamba, kuanzia tarehe 22 - 27 Januari 2019 kunafanyika maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani huko Panama ambayo yanaongozwa na kauli mbiu “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; iwe kwangu kama ulivyosema”. Lk. 1:38. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuombea tukio hili muhimu katika hija ya maisha na utume wa Kanisa.

Baba Mtakatifu anasema, utume wa Kanisa kwa vijana unafumbatwa katika mambo makuu matatu: kuwasikiliza, kuwasindikiza na kuwasaidia vijana kufanya mang’amuzi makini katika maisha na wito wao. Vijana ni amana na utajiri wa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Wazazi kwa kushirikiana vyema na wazee wanaweza kuwasaidia malezi na majiundo bora zaidi ya vijana wa kizazi kipya, jambo la msingi ni marika haya kujenga utamaduni wa majadiliano unaofumbatwa katika sanaa na utamaduni wa kusikilizana!

Baba Mtakatifu anawataka wakleri ambao ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu, kuonesha uwepo wa Mungu katika maisha ya waja wake kwa njia ya: tafakari makini ya Neno la Mungu; maadhimisho na ushiriki mkamilifu wa watu wa Mungu katika Sakramenti za Kanisa kwa kutambua kwamba, Sakramenti ya Upatanisho ni chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake! Kanisa linahitaji waungamishaji, watakaowasaidia waamini kuonja huruma na msamaha wa dhambi zao, kama ilivyokuwa katika Injili ya Baba mwenye huruma kwa Mwana mpotevu! Wakati wa hija yake ya kitume nchini Panama, Baba Mtakatifu Francisko kwa mara ya kwanza atawaungamisha wafungwa na mahabusu wanaotumikia adhabu zao kwenye Gereza la Watoto Watukutu huko Garzas de Pacora.

Hospitalini ni mahali pa kutangaza na kushuhudia Injili ya huduma ya upendo na huruma ya Mungu kwa wagonjwa. Ni mahali ambapo wahudumu wa sekta ya afya wanapaswa kujisadaka bila ya kujibakiza, kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa. Kila mfanyakazi katika nafasi na dhamana yake, ajivike fadhila ya unyenyekevu katika huduma; kwa kukuza na kudumisha nia njema inayomwilishwa katika huduma ya upendo mintarafu tunu msingi za Kiinjili. Fumbo la Umwilisho ni ushuhuda wa uwepo endelevu wa Mungu kati ya watu wake! Baba Mtakatifu Francisko akiwa nchini Panama Jumapili tarehe 27 Januari 2019 atatembelea Kituo cha Msamaria Mwema cha Juan Diaz kwa ajili ya Wagonjwa wa Ukimwi, kama kielelezo cha mchungaji mwema anayeguswa na mahangaiko ya watu wake!

Ratiba elekezi ya Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Panama inaonesha kwamba, Papa ataondoka Roma, Jumatano tarehe 23 Januari 2019 asubuhi na kuwasili majira ya jioni kwenye Uwanja wa Ndege wa Tocumen nchini Panama. Baba Mtakatifu atakaribishwa rasmi na viongozi wa Serikali na Kanisa na baadaye ataelekea kwenye Ubalozi wa Vatican nchini Panama kwa mapumziko.

Alhamisi, tarehe 24 Januari 2019 majira ya asubuhi, Baba Mtakatifu atamtembelea rasmi Rais wa Panama, Ikulu baadaye atakutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, wanadiplomasia na wawakilishi mbali mbali wa vyama vya kiraia nchini Panama kwenye Jengo la Wizara la Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa nchini Panama. Baadaye, Baba Mtakatifu atakutana na kuzungumza na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kati, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Francisko wa Assis na jioni, itakuwa ni patashika nguo kuchanika, kwani Baba Mtakatifu atafungua rasmi maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 katika uwanja Cinta Costera.

Ijumaa tarehe 25 Januari 2019, Baba Mtakatifu ataongoza Ibada ya Upatanisho kwenye Gereza la Vijana Watukutu. Atarejea kwenye Ubalozi wa Vatican kwa mapumziko mafupi na jioni ataongoza Ibada ya Njia ya Msalaba kwa vijana na kutoa mahubiri. Jumamosi, tarehe 26 Januari 2019, Baba Mtakatifu ataongoza Ibada ya Misa Takatifu sanjari na kubariki Altare ya Kanisa Kuu la Bikira Maria wa Antiqua. Ibada hii itakuwa ni kwa ajili ya wakleri, watawa na waamini wa vyama na mashirika ya kazi za kitume nchini Panama. Baba Mtakatifu atapata chakula cha mchana pamoja na vijana kwenye Seminari kuu ya San Josè na jioni atashiriki katika Mkesha wa Sala kwa ajili ya kufunga rasmi Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019.

Jumapili, tarehe 27 Januari 2019: Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani, Baba Mtakatifu ataongoza Ibada ya Misa Takatifu na kusali Sala ya Malaika wa Bwana pamoja na vijana kwenye Uwanja wa Yohane Paulo II; atatembelea Nyumba ya Msamaria Mwema kwa ajili ya Watoto Yatima na baadaye jioni, ataagwa na kufunga vilago kurejea mjini Vatican ili kuendelea na utume wake.  Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuwasili mjini Roma Jumatatu tarehe 28 Januari 2019 majira ya asubuhi.

Itakumbukwa kwamba, hii ni hija ya ishirini na sita ya Baba Mtakatifu Francisko kimataifa na tayari amekwisha kutembelea nchi 40 duniani na kati ya nchi hizi, hadi sasa kwa Bara la Afrika, amebahatika kutembelea Kenya, Uganda na Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati. Kwa mara ya kwanza, Mtakatifu Yohane Paulo II alitembelea nchini Panama kunako mwaka 1983. Papa Francisko kwa mara ya kwanza katika historia ya maisha yake, anatembelea Panama, anasema Dr. Alessandro  Gisotti, Msemaji mkuu wa muda wa Vatican wakati akifafanua kuhusu ratiba elekezi ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko huko Panama, Ijumaa, tarehe 18 Januari 2019.

Baba Mtakatifu anatarajiwa kudadavua kuhusu: Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; Ushuhuda wa utakatifu wa maisha; utu, heshima na haki msingi za binadamu hasa watu mahalia dhidi ya ukoloni wa kiitikadi. Uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko nchini Panama unatarajiwa pia kuwa ni alama ya amani, upatanisho na maridhiano kati ya watu, hususan katika eno hili ambalo linakumbana na changamoto pevu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, vijana kutoka Amerika ya Kusini wataweza kufuata mfano na wito wa Bikira Maria ili kuwa mashuhuda na vyombo vya furaha ya Injili! Huu ni muda wa kusali pia Rozari takatifu, muhtasari wa historia ya ukombozi kwa ajili ya kuombea amani duniani, kila mtu kadiri ya lugha yake!

Papa: Hija Panama 2019
21 January 2019, 10:19