Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuombea Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani 2019. Papa Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuombea Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani 2019.  (REMO CASILLI)

Papa Francisko: Salini kuombea Siku ya Vijana Duniani Panama 2019

Papa Francisko kabla ya kuondoka, kuelekea Panama, Jumatano, 23 Januari 2019 amekutana na vijana nane ambao ni wakimbizi kutoka mataifa mbali mbali wanaohudumiwa kwenye Kituo cha Wakimbizi cha Padre Arrupe, kilichoko Roma. Viongozi mbali mbali wa serikali ya Italia na Kanisa walikuwepo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Fumicino, ili kumsindikiza Baba Mtakatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, anawaomba waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuombea maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 huko Panama ambayo yanaongozwa na kauli mbiu “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; iwe kwangu kama ulivyosema”. Lk. 1:38. Hili ni tukio muhimu sana katika hija ya maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo.

Baba Mtakatifu kabla ya kuondoka, kuelekea Panama, Jumatano, asubuhi, tarehe 23 Januari 2019 amekutana na vijana nane ambao ni wakimbizi kutoka mataifa mbali mbali wanaohudumiwa kwenye Kituo cha Wakimbizi cha Padre Arrupe, kilichoko mjini Roma. Viongozi mbali mbali wa serikali ya Italia na Kanisa walikuwepo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Fumicino, ili kumsindikiza Baba Mtakatifu katika safari yake ya 26 ya Kimataifa nje ya Italia.

Akiwa njiani kuelekea Panama, Baba Mtakatifu ametuma salam na matashi mema kwa viongozi wakuu wa nchi ambamo amepitia katika anga lao, yaani: Italia, Ufaransa, Hispania, Ureno, Marekani, Jamhuri ya Watu wa Domenican, Uholanzi, Colombia na hatimaye, Panama. Baba Mtakatifu katika salam na matashi mema aliyomwandikia Rais Sergio Mattarella wa Italia anasema, anasukumwa kwa shahuku ya kutaka kukutana na vijana wa kizazi kipya kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaofumbatwa katika alama ya imani na matumaini. Anamtakia Rais Mattarella heri na baraka; amani na utulivu kwa watu wa Mungu nchini Italia. Kwa viongozi wengine wote, Baba Mtakatifu amewaombea amani na nguvu ya kuweza kutekekeza vyema dhamana na wajibu wao kwa wananchi wao; Ustawi, maendeleo na furaha.

Papa Francisko ni kielelezo cha upendo na mshikamano na maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Sakramenti ya Upatanisho ni chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake! Kanisa linahitaji waungamishaji, watakaowasaidia waamini kuonja huruma na msamaha wa dhambi zao, kama ilivyokuwa katika Injili ya Baba mwenye huruma kwa Mwana mpotevu! Wakati wa hija yake ya kitume nchini Panama, Baba Mtakatifu, kwa mara ya kwanza atawaungamisha wafungwa na mahabusu wanaotumikia adhabu zao kwenye Gereza la Watoto Watukutu huko Garzas de Pacora. Hili ni gereza ambalo kwa sasa linatoa hifadhi kwa watoto zaidi ya 200.

Fumbo la Umwilisho ni ushuhuda wa uwepo endelevu wa Mungu kati ya watu wake! Baba Mtakatifu Francisko akiwa nchini Panama Jumapili tarehe 27 Januari 2019 atatembelea Kituo cha Msamaria Mwema cha Juan Diaz kwa ajili ya Wagonjwa wa Ukimwi, kama kielelezo cha mchungaji mwema anayeguswa na mahangaiko ya watu wake!

Papa: Njiani Panama 2019
23 January 2019, 14:31