papa Francisko: Njia ya Msalaba ni safari ya imani na ukimya pamoja na Bikira Maria papa Francisko: Njia ya Msalaba ni safari ya imani na ukimya pamoja na Bikira Maria 

Papa Francisko: Njia ya Msalaba ni safari ya imani na B. Maria

Njia ya Msalaba, Via Crucis, ni safari ya imani inayomwezesha mwamini kusindikizana na Bikira Maria, katika hali ya ukimya, amani na utulivu wa ndani, ili kutafakari huruma na upendo wa Kristo Yesu, aliyejisadaka kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu. Waamini wanahimizwa mara kwa mara kufanya tafakari ya Njia ya Msalaba na kwamba, hizi ni kati ya Sala zipendwazo na Papa Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Njia ya Msalaba, “Via Crucis” ni Ibada ambayo inamwonesha Kristo Yesu akiwa katika hatua za mwisho mwisho wa maisha yake hapa duniani kama sehemu ya mchakato wa kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Ni njia iliyoanza kule kwenye Mlima wa Mizeituni na kuishia Mlimani Golgotha, mahali ambapo Yesu alisulubiwa na hatimaye, kujisadaka kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti.

Hii ni njia ambayo Roho Mtakatifu alimwandalia Mwana wa Mungu, ikapendwa na Mama Kanisa kama chemchemi ya Sakramenti za Kanisa na mshikamano kwa binadamu. Yerusalemu ni mji ambamo Yesu aliweza kufanya Njia ya Msalaba kwa mara ya kwanza, tukio ambalo waamini wanalirudia wakati wa Kipindi cha Kwaresima, lakini kwa namna ya pekee, Ijumaa kuu. Fumbo la Msalaba ni ufunuo wa hali ya juu kabisa wa huruma, upendo, msamaha na upatanisho unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kristo Yesu, Uso wa huruma ya Baba wa milele!

Udhaifu wa mwili wa Yesu kutokana na mateso makali ni changamoto ambayo inawahamasisha vijana, kusimama tena na kusonga mbele kwa imani na matumaini mapya, baada ya kuanguka na kutopea katika: matumizi haramu ya dawa za kulevya, fujo na ghasia, ukahaba na mambo yale yote yanayochafua sura na mfano wa Mungu katika maisha yao. Njia ya Msalaba, ni safari ya imani inayomwezesha mwamini kusindikizana na Bikira Maria, katika hali ya ukimya, amani na utulivu wa ndani, ili kutafakari huruma na upendo wa Kristo Yesu, aliyejisadaka kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu. Waamini wanahimizwa mara kwa mara kufanya tafakari ya Njia ya Msalaba na kwamba, hizi ni kati ya Sala ambazo zinapendwa sana na Baba Mtakatifu Francisko.

Katika katekesi yake, Jumatano, tarehe 30 Januari 2019, Baba Mtakatifu amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuungana naye kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani, kwa matendo makuu aliyolifanyia Kanisa katika maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani huko nchini Panama. Anawashuruku viongozi wa Serikali, Kanisa, familia, vijana wa kujitolea pamoja na vijana ambao walijisadaka na hatimaye, wakapiga moyo konde kwenda Panama! Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza wanafamilia nchini Panama ambao wanawaonea fahari watoto wao kuwa ni matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi!

Hii ni changamoto kwa familia Barani Ulaya kuangalia tena “ukame wa watoto wanaozaliwa”! Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 imekuwa ni fursa ya kukutana na vijana wazawa kutoka Amerika ya Kusini, waliofungua maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, ili kuonesha amana na utajiri wa watu wa Amerika ya Kusini. Umati huu wa vijana wazawa kutoka Amerika ya Kusini, ulitajirishwa zaidi na vijana kutoka katika mataifa mengine; vijana wenye lugha, tamaduni, mila na desturi mbali mbali mbali, lakini hata katika utofauti huu, bado wote walijisikia wamoja katika imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Vijana ni alama ya kinabii inayotaka kubomolea mbali kuta za utengano zinazojengwa na baadhi ya wanasiasa kila kukicha. Vijana hawa ni kielelezo makini kwamba, vijana Wakristo ni chachu ya amani.

Maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019, yameongozwa na kauli mbiu “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; iwe kwangu kama ulivyosema”. Lk. 1:38. Kauli mbiu hii imerudiwa kwa ari na moyo mkuu na wawakilishi wa vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Hii ndiyo changamoto pevu ambayo vijana wanatakiwa kuimwilisha katika uhalisia wa maisha yao, ili kujisadaka kwa ajili ya kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Wakati wa Njia ya Msalaba, vijana wamebeba moyoni mwao shida, mahangaiko na matamanio halali ya vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, lakini zaidi, wale wanaotoka Amerika ya Kati. Hawa ni vijana wanaopekenywa na umaskini na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo. Ni kutokana na umuhimu huu, Baba Mtakatifu wakati wa hija yake ya Kitume nchini Panama ameadhimisha Liturujia ya Upatanisho kwenye Gereza la Watoto Watukutu huko Panama pamoja na kutembelea Kituo cha Msamaria Mwema cha Juan Diaz kinachotoa huduma kwa waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi.

Baba Mtakatifu anawapongeza vijana walioshiriki mkesha wa sala kwa ajili ya kufunga rasmi maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa mwaka 2019 na baadaye, asubuhi na mapema, wakawa tayari kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu. Katika mkesha, kumefanyika majadiliano ya kina na vijana wa kizazi kipya! Wamesikiliza kwa makini na wakati wa ukimya, kimya kikuu kiliweza kusikika licha ya umati mkubwa wa vijana kiasi kile! Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, ndiye mfano bora wa kuigwa, kwa “Ndiyo” yake, ambayo imeshuhudiwa na vijana wakati wa mkesha. Ibada ya Misa takatifu, asubuhi na mapema, Siku ya kwanza ya Juma, yaani Ufufuko wa Kristo, vijana wakiwa wamesheheni nguvu ya Roho Mtakatifu, wakatafakari leo ya Mungu na Kanisa katika maisha yao!

Wazazi, walezi na jamii katika ujumla wake, inapaswa kuchakarika ili kwamba, vijana waweze kupata: elimu bora, kazi, jumuiya na familia. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, mkutano wake na Maaskofu wa Sekretarieti ya Mabaraza ya Maaskofu Katoliki, Amerika ya Kati, SEDAC, imekuwa ni faraja kubwa sana kwake. Kwa pamoja walijiachilia na kujikabidhi mikononi mwa Mtakatifu Oscar Romero ili aweze kuwafunda kwa ushuhuda wake, ili kufikiri na kutenda pamoja na Kanisa; kwa kuwa karibu zaidi na vijana, maskini, wakleri na watu wa Mungu.

Baba Mtakatifu anasema, akiwa nchini Panama, ametabaruku Altare ya Kanisa kuu la Jimbo kuu la Panama. Kanisa hili lilikuwa limefungwa kwa muda wa miaka saba, kwa ajili ya kufanyiwa ukarabati mkubwa. Ilikuwa ni sherehe kubwa ya kuweza tena kugundua uzuri, utakatifu na imani ya watu wa Mungu. Altare hii ilitabarukiwa kwa kupakwa Mafuta ya Krisma ya Wokovu, yanayotumika pia kwa ajili ya kuwapaka waamini waliobatizwa; wale wanaoimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara pamoja na kuwaweka wakfu Maaskofu na Mapadre. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, familia ya Mungu nchini Panama itaendelea kuimarika siku hadi siku, ili kweli vijana waweze kuwa ni wamisionari mitume wa Kristo Yesu!

Papa: Katekesi

 

30 January 2019, 15:58