Tafuta

Papa Francisko anawataka vijana kutangaza na kushuhudia tunu msingi za maisha! Papa Francisko anawataka vijana kutangaza na kushuhudia tunu msingi za maisha! 

Siku ya Vijana Duniani 2019: Vijana kumbatieni tunu msingi za maisha!

Papa Francisko katika tafakari yake, amewataka vijana kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, kusema “Ndiyo” ili kukumbatia Injili ya uhai; kusema “Ndiyo” katika ujenzi wa Jumuiya, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Vijana waseme “Ndiyo” ili kulinda na kudumisha mila, desturi na tamaduni njema, tayari kuleta mabadiliko katika maisha ya jamii kwa mwanga wa Injili ya Kristo Yesu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Umati mkubwa wa vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, Jumamosi usiku, tarehe 26 Januari 2019 umehudhuria Mkesha wa Sala kwa ajili ya kufunga rasmi maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kwa mwaka 2019 huko nchini Panama. Sherehe hii ya huruma na matumaini kwa vijana, imekuwa ni fursa na mwaliko kwa vijana kufuata mfano wa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake, amewataka vijana kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, kusema “Ndiyo” ili kukumbatia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; kusema “Ndiyo” katika ujenzi wa Jumuiya, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Vijana wanapaswa kusema “Ndiyo” ili kulinda na kudumisha mila, desturi na tamaduni njema, tayari kuleta mabadiliko katika maisha ya jamii kwa mwanga wa Injili na Mafundisho Jamii ya Kanisa! Baba Mtakatifu anasema, Kristo Yesu ni chemchemi ya maisha ya uzima wa milele, anayejisadaka ili kuwavuta na kuwashirikisha watu historia ya upendo, changamoto na mwaliko kwa vijana kusema “Ndiyo” kama alivyofanya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa!

Hakuwa maarufu sana kwenye mitandao ya kijamii, lakini ni mwanamke wa “shoka” aliyeacha amana na utajiri mkubwa katika historia ya binadamu. Ni mwanamke jasiri aliyekubali kupokea na kukumbatia upendo wa Mungu unaoganga na kuponya; unaotakasa na kupyaisha maisha! Baba Mtakatifu anawataka vijana kuangalia ndani mwao ili hatimaye, waweze kukubali na kuumwilisha mpango wa Mungu katika maisha kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria! Akajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kumtumikia Mungu, ingawa alikuwa na mashaka na wasi wasi mwingi, lakini akajiaminisha kwa wema na huruma ya Mungu na kukubali kuwa kweli ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili!

Hii ni changamoto kwa wazazi na walezi kuwakubali na kuwapokea watoto ambao ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu hata kama wakati mwingine, watoto hawa wanazaliwa na ulemavu. Wazazi wawapende, wawaheshimu na kuwathamini watoto wao, kwani ulimwengu si kwa ajili ya watu wakamilifu bali hata walemavu wanayo nafasi na dhamana kubwa ulimwenguni! Vijana wawe na ujasiri wa kuthubutu kukumbatia maisha kama yalivyo, familia, nchi na marafiki zao kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo. Kila mtu anapaswa kushirikishwa upendo wa dhati kama ilivyo hata kwa wakimbizi na wahamiaji.

Hivi ndivyo alivyofanya Kristo Yesu, kiasi cha kuleta mageuzi makubwa katika maisha ya watu! Aliwapokea na kuwakumbatia wagonjwa, watoza ushuru na watenda dhambi hata dakika ya mwisho wa maisha yake, akawasamehe hata watesi wake, upendo wa Mungu kweli ni wa ajabu sana! Upendo wa Mungu unatakasa na kuokoa, changamoto na mwaliko kwa vijana kushuhudia na kuandika historia ya upendo unaotakasa na kuokoa, licha ya dhambi na mapungufu ya kibinadamu. Vijana wanapaswa kukumbatia na kuenzi Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo na hali ya kukata tamaa kutokana na ukosefu wa fursa za ajira, elimu, jumuiya, familia na utambulisho wa mtu, mambo ambayo yana athari kubwa katika maisha ya watu!

Vijana wajenge ari na moyo wa kushirikiana na kushikamana na wazee, ambao wanapaswa pia kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa kuhakikisha kwamba, watoto wao wanapata mahitaji msingi katika maisha kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Vijana wengi, hawana tena uchungu wa kukosa familia, jumuiya au jamii, kwani hawana tena mshikamano na mafungamano ya dhati na makundi haya! Leo hii, vijana wanatoa kipaumbele cha kwanza kwa simu za viganjani na mitandao ya kijamii! Kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Yohane Bosco, vijana wanapaswa kuangaliwa kwa jicho la Mungu, ili kuwapatia fursa za elimu, ajira, familia na jumuiya; mambo msingi katika utambulisho wa kijana yoyote yule!

Ni wajibu wa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema anasema Baba Mtakatifu kujenga familia, Kanisa dogo la nyumbani; mahali pa kukumbatia na kuhifadhi Injili ya uhai; mahali pa kukuza na kudumisha: imani, matumaini na mapendo, tayari kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria. Wazazi, wazee na walezi, wawasaidie vijana kupata umbulisho wao katika jamii, ili waweze kuzamisha mizizi ya furaha na matumaini, tayari kuchangia katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana kwamba, umaarufu wao si kuwa na gari la kifahari au simu ya kisasa, ambayo ukipita kila mtu “macho kodo”! Vijana washuhudie umaarufu wao kwa njia ya huduma makini kwa maskini na wazee; kwa kufumbatana imani na matumaini kutoka kwa Mwenyezi Mungu, tayari kuleta mageuzi yanayojikita katika utu, heshima na haki msingi za binadamu. Vijana wawe na ujasiri wa kumfungulia Kristo malango ya maisha yao, daima wakiwa tayari kutekeleza utume wake kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria.

Katika hija hii, vijana wanasindikizwa kwa mfano na maombezi ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa aliyediriki kusema, “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; iwe kwangu kama ulivyosema”. Lk. 1:38. Huu ni ushuhuda wa ujasiri na ukarimu kwa mwamini aliyetambua siri ya wito wake, tayari kujitosa kimasomaso bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani. Bikira Maria, katika ujana wake, alibahatika kushirikishwa na Mwenyezi Mungu mpango wa Ukombozi, akawa ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili.

Papa: Mkesha

 

27 January 2019, 13:49