Cerca

Vatican News
Papa Francisko tayari amewasili nchini Panama ili kuwasha moto wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 Papa Francisko tayari amewasili nchini Panama ili kuwasha moto wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019.  (AFP or licensors)

Siku ya Vijana Duniani 2019 yaanza kutimua vumbi nchini Panama

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 23 Januari 2019, amelakiwa na umati wa familia ya Mungu kutoka ndani na nje ya Panama, iliyokuwa inaongozwa na Rais Juan Carlos Varela Rodríguez wa Panama. Kulikuwepo na wawakilishi wa vijana 2, 000, Makardinali na Maaskofu 480! Kwa hakika Panama imemkaribisha Baba Mtakatifu kwa “cheche za furaha na matumaini makubwa”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano jioni tarehe 23 Januari 2019, amewasili nchini Panama, kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani. Baba Mtakatifu amelakiwa na umati wa familia ya Mungu kutoka ndani na nje ya Panama, iliyokuwa inaongozwa na Rais Juan Carlos Varela Rodríguez wa Panama. Kulikuwepo na wawakilishi wa vijana 2, 000, Makardinali na Maaskofu 480! Kwa hakika Panama imemkaribisha Baba Mtakatifu kwa “cheche za furaha na matumaini makubwa”.

Baba Mtakatifu amejibu ukarimu huu kwa tabasamu la kukata na shoka pamoja na kuwapatia baraka zake za kitume. Vijana katika nyimbo zao, wanamwomba Mwenyezi Mungu aweze kuwakirimia matumaini, ari na moyo mkuu wa kimisionari, tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha kwa watu wa Mataifa. Baba Mtakatifu anawahamasisha vijana kutoka kimasomaso tayari kushiriki katika ujenzi wa jamii inayosimikwa katika misingi ya haki, amani, usawa, utu na heshima ya binadamu!

Baba Mtakatifu akiwa njiani kuelekea nchini Panama, safari ambayo imemgharimu masaa 13, amepata nafasi ya “kuchonga” na waandishi wa habari walioko kwenye msafara wake. Baba Mtakatifu pamoja na mambo mengine, amegusia kuhusu hija yake ya kitume nchini Japan, ambako anatarajia kutembelea Mwezi Novemba, 2019, Mwenyezi Mungu akipenda. Baba Mtakatifu anawaalika wananchi wa Japan, kuanza kujipanga kuanzia sasa.

Baba Mtakatifu ameonesha pia nia ya kutembelea Iraq, lakini viongozi mahalia wanasema, hadi sasa hakuna uhakika wa usalama! Ufafanuzi uliotolewa baadaye na Dr. Alesandro Gisotti, Msemaji mkuu wa muda wa Vatican ni kwamba, Vatican inaendelea kufuatilia zaidi, ili kuhakikisha kwamba, ndoto hii inatimia! Kama alivyobainisha Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anayo nia na sababu msingi za kwenda Iraq, lakini kwa sasa mazingira bado si rafiki sana ndiyo maana Baba Mtakatifu anaendelea kuvuta subira!

Baba Mtakatifu ameguswa na kusikitishwa sana na vifo wanavyokumbana navyo wakimbizi na wahamiaji, wakiwa njiani kutafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi ughaibuni. Baba Mtakatifu anasema, changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji, ataizungumzia, wakati wakiwa njiani kurejea kutoka Panama! Amewataka waandishi wa habari kuvuta subira! Amezungumzia pia falsafa ya baadhi ya viongozi kutaka kujenga kuta zinazowatenganisha watu! Anakaza kusema, hizi ni kuta za woga na wasi wasi usiokuwa na mvuto wala mashiko!

Papa: Kuwasili Panama 2019

 

 

24 January 2019, 12:28