Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anawataka vijana kuishi leo ya Mungu katika huduma na utume wao! Papa Francisko anawataka vijana kuishi leo ya Mungu katika huduma na utume wao!  (ANSA)

Papa Francisko awataka vijana kuishi leo ya Mungu!

Baba Mtakatifu Francisko anawataka vijana kuhakikisha kwamba, wanatekeleza kwa dhati leo ya Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Utamaduni na sanaaa ya watu kukutana pamoja na kuwasikilisha vijana ni amana na urithi mkubwa wa Kanisa kutoka kwa Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana iliyohitimishwa hivi karibuni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka vijana kuitikia wito unaowashirikisha leo ya Mungu ili kuwatangazia watu Habari Njema ya Wokovu. Ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, wanamwilisha upendo wa Mungu katika uhalisia wa maisha yao, kwa kuwa na imani na ujasiri thabiti kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria. Anawashukuru na kuwapongeza vijana waliotikisa Panama kwa uwepo na ushuhuda wao! Kwa ufupi, huu ndio ujumbe uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 27 Januari 2019, kwenye Uwanja wa Metro Park, kwa bahari ya vijana waliokuwa wanashiriki katika Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kufunga maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 huko nchini Panama.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amekazia kwa namna ya pekee, leo ya Mungu iliyofunuliwa na Kristo Yesu katika maisha yake ya hadhara. Amepakwa mafuta kuwahubiri maskini maskini Habari Njema, kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao pamoja na kuutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa. Leo ya Mungu imemwilishwa katika Kristo Yesu, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu; mtetezi na haki ya wanyonge. Leo ya Mungu anasema Baba Mtakatifu haikupokelewa kwa mikono miwili na watu wa Nazareti kutokana na mazoea yao, kiasi cha kumwona Kristo Yesu, kuwa “si mali kitu” bali mwana wa Yosefu, Seremala.

Yesu ni kielelezo cha umwilisho wa upendo wa Mungu ambao umepenya katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu, katika machungu na ufunuo wa utukufu wa Mwana mpendwa wa Mungu. Yesu amekuwa jirani kwa waja wake, lakini kwa bahati mbaya watu wanataka kuwa na Mwenyezi Mungu ambaye yuko mbali sana na watu, ambaye hawezi kuzoeleka kama ndugu, rafiki na mwana familia. Mwenyezi ni kielelezo cha upendo halisi, nguzo msingi katika maisha ya Wakristo.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, hii ndiyo hatari wanaweza kukumbana nayo hata watu katika ulimwengu mamboleo, kwa kushindwa kutambua neema ya Mungu inayotenda kazi katika maisha ya watu, kiasi cha kujisadaka kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Kishawishi cha kutaka kulifungia Neno la Mungu katika “makabati” ya majumba yao! Hii ni changamoto kwa vijana kuhakikisha kwamba, wanachangamka na kuanza kutekeleza leo ya Mungu katika maisha yao na kamwe wasikubali kuwa ni mizigo kwa jamii zao.

Vijana wawe ni watu wanaothubutu kutafuta furaha ya kweli katika upendo; kwa kuonesha udadisi ili hatimaye, kuweza kutekeleza ndoto za maisha yao, vinginevyo, watachanganyikiwa na kuanza kunyong’onyea na hatimaye, kubaki na huzuni moyoni. Baba Mtakatifu anawataka vijana kuhakikisha kwamba, wanatekeleza kwa dhati leo ya Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Utamaduni na sanaaa ya watu kukutana pamoja na kuwasikilisha vijana ni amana na urithi mkubwa wa Kanisa kutoka kwa Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana iliyohitimishwa hivi karibuni. Vijana wajitahidi kutengeneza mazingira yatakayowakutanisha kwa kutambua kwamba, wanahitajiana na kukamilishana katika safari ya maisha yao.

Kumbe, ni wajibu wao kusimama kidete kupigania leo ya maisha yao, kwa kutambua kwamba, wao kimsingi ni matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Mwenyezi Mungu anawaita na kuwatuma sehemu mbali mbali za dunia ili kutekeleza ndoto yao. Vijana ni ndiyo ya leo ya Mungu inayopaswa kumwilishwa katika huruma tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu! Upendo wa Yesu ni chemchemi ya furaha ya kweli, matumaini kwa wale waliokata tamaa, mshikamano na udugu.

Hii ni chachu ya kupambana na changamoto mamboleo inayopaswa kuwa ni dira na mwongozo wa maisha ya kila siku na wala si wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani. Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa aliyeamini na kwa ujasiri mkubwa akakubali kushiriki leo ya Mungu, awaombee vijana kutambua utume wao, kumpenda Mwenyezi Mungu na kumwachia aweze kuwatumia kama vyombo vya uinjilishaji. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawataka vijana kuhakikisha kwamba, wanamwilisha upendo wa Mungu katika maisha na vipaumbele vyao!

Baba Mtakatifu mara baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, amewashukuru viongozi wa Serikali ya Panama, wakuu wan chi mbali mbali walioshiriki, viongozi wa Kanisa pamoja na wale wote waliowasindikiza vijana kwa sala na sadaka zao, kiasi kwamba, ndoto ya maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani imekamilika huko nchini Panama. Amewashukuru na kuwapongeza vijana wa kizazi kipya na kuwataka kuendelea kufanya hija kwa kutambua kwamba, wao ni leo ya Mungu. Sasa ni wakati wa kumwilisha neema na baraka walizopata wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani katika maisha yao, ili kweli waendelee kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili!

Papa: Ibada ya Misa Kufunga

 

28 January 2019, 14:53