Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko ana Ibada ya pekee kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa! Baba Mtakatifu Francisko ana Ibada ya pekee kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa! 

Papa Francisko na Ibada kwa Bikira Maria! Yaani we acha tu!

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kukuza na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa, ili aweze kuwasaidia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao, kielelezo cha imani tendaji! Bikira Maria ni mfano na kielelezo cha imani, matumaini na mapendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya maandalizi ya hija yake nchini Panama kuanzia tarehe 23-27 Januari 2019, Jumanne, tarehe 22 Januari 2019 amekwenda kusali kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu mjini Roma ili kujikabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria afya ya Warumi.  Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe 20 Januari 2019, amewajulisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kwamba, kuanzia tarehe 22 - 27 Januari 2019 kunafanyika maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani huko Panama ambayo yanaongozwa na kauli mbiu “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; iwe kwangu kama ulivyosema”. Lk. 1:38. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuombea tukio hili muhimu katika hija ya maisha na utume wa Kanisa.

Baba Mtakatifu anatarajiwa kudadavua kuhusu: Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; Ushuhuda wa utakatifu wa maisha; utu, heshima na haki msingi za binadamu hasa watu mahalia dhidi ya ukoloni wa kiitikadi. Uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko nchini Panama unatarajiwa pia kuwa ni alama ya amani, upatanisho na maridhiano kati ya watu, hususan katika eno hili ambalo linakumbana na changamoto pevu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, vijana kutoka Amerika ya Kusini wataweza kufuata mfano na wito wa Bikira Maria ili kuwa mashuhuda na vyombo vya furaha ya Injili! Huu ni muda wa kusali pia Rozari takatifu, muhtasari wa historia ya ukombozi kwa ajili ya kuombea amani duniani, kila mtu kadiri ya lugha yake!

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kukuza na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa, ili aweze kuwasaidia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao, kielelezo cha imani tendaji! Bikira Maria ni mfano na kielelezo cha imani, matumaini na mapendo, kwani amediriki kuwa ni mfuasi amini wa Kristo Yesu na chombo cha huduma makini kwa jirani zake; mtindo na mfumo wa maisha unaopaswa kutekelezwa na Mapadre kama sehemu ya majiundo yao ya awali na endelevu katika Kanisa.

Baba Mtakatifu anasema, ikiwa kweli waamini wanataka kuwa wafuasi amini wa Kristo Yesu na Kanisa lake; ili kuguswa na kuponywa na huruma pamoja na upendo wa Mungu, wanapaswa kuzingatia mambo makuu yafuatayo: Fumbo la Msalaba, Ekaristi Takatifu na Ibada ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Bikira Maria ni Mama wa Mungu na Kanisa, kwani ndani ya Moyo wake safi usiokuwa na doa, watu wote wanapata utambulisho wao, kwa kupenda na kupendwa, hali inayoonesha uwepo wa Mungu kati ya watu wake. Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Mama wa Mlango wa Mbinguni, ametangazwa kuanzia sasa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa ni “Bikira Maria Mama wa huruma na matumaini”.

Ni Mama ambaye daima ameonesha ulinzi na tunza kwa watu wanaomkimbilia katika shida na mahangaiko yao; upendo ambao umeendelezwa hadi nyakati hizi. Bikira Maria ni dira na kielelezo cha njia ya kwenda mbinguni; Njia ambayo kamwe haiwezi kumpotezesha mtu mwelekeo wa maisha! Njia hii, ni Kristo ambaye pia ni ukweli na uzima. Yesu ni mlango wa mbingu, unaowaalika wote kushiriki furaha ya uzima wa milele. Anawasubiri kwa moyo wa huruma na mapendo, wale wote wanaomwendea kwa toba na wongofu wa ndani. Bikira Maria, nyota ya asubuhi anawaongoza waamini kwa Kristo Yesu, ambaye ni Lango la huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu anasema, kunako mwaka 2015, Kanisa limeadhimisha Jubilei ya Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu; mwaka ambao umewawezesha waamini wengi kuvuka Lango la Huruma ya Mungu, ili kuonja upendo unaofariji, unaosamehe na kutoa matumaini. Hii ndiyo hamu inayopaswa kushuhudiwa na watu wote kwa kuwaonjesha jirani zao wema na huruma ya Mungu katika maisha yao. Bikira Maria Mama wa huruma na matumaini, asaidie watu kusambaza na kueneza wema na huruma ya Mungu kama njia ya kuganga na kuponya madonda yanayomwandama mwanadamu, tayari kusimama na kupiga moyo konde, ili kusonga mbele kwa neema na baraka ya Mungu.

Baba Mtakatifu anawataka waamini  kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu amejishusha ili kuwaokoa, mwaliko kwao pia ni kujishusha na kuwainamia jirani zao wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali, kwa kuwa na jicho la huduma kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, ili kuwaonjesha watu wanaoteseka, ile “divai ya furaha”, kama ilivyotokea kwenye Arusi ya Kana. Bikira Maria awe ni mfano na kielelezo cha wanawawake wote ambao wamekuwa kweli ni tabernakulo ya Injili ya uhai, ili kuwaheshimu na kutambua dhamana, wito na utume wao kwa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Hata katika ukimya wao, wanawake ni nguvu ya matumaini.

22 January 2019, 15:00