Nia za Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwezi Januari 2019: Maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani 2019 huko Panama Nia za Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwezi Januari 2019: Maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani 2019 huko Panama 

Nia za Papa Francisko: Mwezi Januari 2019: Siku ya Vijana Duniani

Mama Kanisa anapenda kujenga sanaa na utamaduni wa kuwasikiliza, kuwasindikiza na kuwaongoza vijana kufanya maamuzi mazito katika maisha kwa kuwa na msimamo thabiti unaojikita katika imani kwa Kristo na Kanisa lake! Papa Francisko katika nia zake za jumla kwa Mwezi Januari 2019 anapenda kujielekeza zaidi katika maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani huko Panama.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani huko nchini Panama kuanzia tarehe 22 - 27 Januari 2019 yanaongozwa na kauli mbiu “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; iwe kwangu kama ulivyosema”. Lk. 1:38. Katika hija hii, vijana wanasindikizwa kwa mfano, maombezi na tunza ya Bikira Maria, aliyeteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa Mama wa Mwanaye Mpendwa, Kristo Yesu. Ni muda wa kutafakari vipaumbele vya maisha na utume wa Kanisa kwa vijana, changamoto, matatizo na fursa walizo nazo kama mashuhuda na vyombo vya furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa!

Mama Kanisa anapenda kujielekeza zaidi katika utume kwa vijana, ili kujenga sanaa na utamaduni wa kuwasikiliza, kuwasindikiza na kuwaongoza vijana kufanya maamuzi mazito katika maisha kwa kuwa na msimamo thabiti unaojikita katika imani kwa Kristo na Kanisa lake! Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa Mwezi Januari 2019 anapenda kujielekeza zaidi katika maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani huko Panama.

Nia za Papa kwa Mwezi Januari 2019

Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa njia ya video kwenye mtandao wa Utume wa sala ulioboreshwa kuanzia Mwaka 2014, anawataka vijana hasa wale wanaotoka Amerika ya Kusini, kufuata mfano wa Bikira Maria, kwa kuitikia wito kutoka kwa Kristo ili kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa! Padre Fredèric Fornos, Mkurugenzi wa Utume wa Sala Kimataifa, amekwisha wasilisha nia za Baba Mtakatifu Francisko kwa mwaka 2019.

Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuungana na Baba Mtakatifu katika sala, hasa wakati huu, Kanisa linalopendelea kupambana na mawimbi makubwa katika maisha na utume wake. Ili kufanikisha lengo hili, kuna haja kwa waamini kutenga muda wa kusali na kutafakari kama anavyofanya Baba Mtakatifu Francisko, kila siku saa 10:10 Alfajiri, anajipatia muda wa kusali na kutafakari katika hali ya ukimya, ili kujenga mahusiano na mafungamano ya dhati na Kristo Yesu!

Huu ni mwaliko unaotolewa pia na Baba Mtakatifu kwa waamini kuhakikisha kwamba, hata katika pilika pilika za maisha, wanapata muda wa kuingia katika undani wa maisha yao, ili kusali na kutafakari matendo makuu ya Mungu. Nia za Sala za Baba Mtakatifu ni matunda ya tafakari na mang’amuzi ya maisha na utume wa Kanisa kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Baada ya kuchagua nia hizi, zinaridhiwa na Baba Mtakatifu na hatimaye kutafsiriwa na kuchapishwa katika lugha mbali mbali za kimataifa.

Padre Fredèric Fornos katika mahojiano maalum na Vatican News anakaza kusema, waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema, daima wako tayari kuitikia mwaliko wa Baba Mtakatifu Francisko katika sala, kama alivyowaomba waamini kusali Rozari Takatifu kwa ajili ya kuliombea Kanisa kwa mwezi Oktoba 2018. Waamini wengi walitekeleza mwaliko huu na kwa hakika, maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa mwaka 2018 yalikwenda salama, ingawa kulikuwa na changamoto ambazo zingeweza kuwagawa Mababa wa Sinodi mintarafu kanuni maadili, utu na heshima ya binadamu kadiri ya maeneo yao.

Waamini wanaendelea kuhamasishwa na Baba Mtakatifu ili kusali kwa ajili ya kuombea umoja na mshikamano wa Kanisa; kwa kukazia zaidi mambo yanayowaunganisha waamini kuliko yale ambayo wakati mwingine yanataka kuwavuruga na hatimaye, kuwatenganisha. Kanisa linaweza kupambana na saratani ya uchu wa mali, madaraka pamoja na kashfa mbali mbali kwa njia ya toba, wongofu wa kitume na kimisionari kama anavyokazia Baba Mtakatifu katika Barua yake kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani. Kumbe, kuna umuhimu kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanajenga utamaduni na sanaa ya kusali, kwa kujiweka wazi mbele ya Mungu katika maisha yao, tayari kupokea neema na baraka zinazoleta mabadiliko makubwa katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake.

Siku ya Vijana Duniani 2019
05 January 2019, 10:12