Tafuta

Mtandao wa utume wa Sala ya Papa: "Clicktoplay" wazinduliwa na Baba Mtakatifu Francisko. Mtandao wa utume wa Sala ya Papa: "Clicktoplay" wazinduliwa na Baba Mtakatifu Francisko. 

Mtandao wa Utume wa Sala ya Papa wazinduliwa!

Baba Mtakatifu Francisko akiwa ameandamana na Padre Frederic Fornos, Mkurugenzi wa Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa amezindua rasmi “Mtandao wa Utume wa Sala ya Papa” Ujulikanao kama “Click To Play”. Mtandao huu utakuwa unahifadhi Nia za Baba Mtakatifu kwa kila mwezi pamoja na Sala kwa ajili ya kuombea utume wa Kanisa. Vijana wanaalikwa kupakua na kuutumia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya 53 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa mwaka 2019 itakayoadhimishwa na Mama Kanisa hapo tarehe 2 Juni 2019 inawahamasisha wadau katika tasnia ya mawasiliano ya jamii kuuvua uongo, kusema ukweli kwa maana wao ni viungo, kila mmoja kiungo cha mwenzake. Huu ni mchakato wa kujenga na kudumisha jumuiya inayofumbatwa katika mawasiliano, kwa kukazia ukweli na mafungamano ya kijamii.

Wadau katika tasnia ya habari wanapaswa kuhakikisha kwamba, utu na heshima ya binadamu vinapewa kipaumbele cha kwanza katika utume wao wanaopaswa kuutekeleza kwa kuzingatia: weledi, nidhamu, uadilifu na uwajibikaji, kwa kusoma alama za nyakati, ili kujibu changamoto mamboleo na mahitaji ya watu wa Mungu kwa nyakati hizi. Baba Mtakatifu ameyasema, haya wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 20 Januari 2019 na kukazia kwamba, kuna haja ya kutafakari kuhusu umuhimu wa mitandao ya kijamii na jumuiya ya binadamu.

Matumizi ya wavuti pamoja na mitandao ya kijamii ni utajiri mkubwa katika ulimwengu mamboleo. Hii ni fursa inayowawezesha watu kujenga ujirani mwema; kushirikishana tunu msingi za maisha na miradi pamoja na kuonesha utashi wa kutaka kujenga jumuiya. Mitandao ya kijamii inaweza kuwasaidia watu kusali na kutafakari kwa pamoja katika jumuiya.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko akiwa ameandamana na Padre Frederic Fornos, Mkurugenzi wa Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa amezindua rasmi “Mtandao wa Utume wa Sala ya Papa” Ujulikanao kama “Click To Pray”. Mtandao huu utakuwa unahifadhi Nia za Baba Mtakatifu kwa kila mwezi pamoja na Sala kwa ajili ya kuombea utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu anawaalika vijana kupakua na kuanza kutumia mtandao huu, ili kusali pamoja naye Rozari Takatifu, muhtasari wa historia ya huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu! Baba Mtakatifu anawataka waamini kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao sanjari na kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea amani hasa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa mwaka 2019 huko nchini Panama.

Mtandao wa Utume wa Sala umeenea katika nchi 98 duniani na unashirikiana kwa karibu sana na Chama cha Kitume cha Vijana wa Ekaristi. Mtandao wa Utume wa Sala pamoja na mambo mengine unajihusisha kikamilifu katika kuandaa picha za video zinazosindikiza nia za Baba Mtakatifu kwa kila mwezi (www.ilvideodelpapa.org) pamoja na Jukwaa la Sala kwa ajili ya utume wa Kanisa (www.clicktopray.org).

Papa: Mtandao wa sala
21 January 2019, 09:27