Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Tunu msingi za maisha ya kijamii zisaidie kupambana na mmong'onyoko wa maadili pamoja na uharibu wa mazingira nyumba ya wote! Papa Francisko: Tunu msingi za maisha ya kijamii zisaidie kupambana na mmong'onyoko wa maadili pamoja na uharibu wa mazingira nyumba ya wote!  (AFP or licensors)

Tunu msingi zisaidie kupambana na uharibifu wa mazingira!

Lengo kuu ni kuiwezesha Jumuiya ya Kimataifa kuunganisha nguvu kwa njia ya majadiliano yatakayowezesha kuimarisha mafungamano ya udugu kati ya Mataifa. Inatosha kuangalia matukio yaliyojiri kutoka sehemu mbali mbali za dunia kwa siku za hivi karibuni yanayotishia usawa wa ustaarabu mamboleo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujikita katika mchakato wa ujenzi wa tunu msingi za kijamii ili kupambana na mmong’onyoko wa maadili na utu wema pamoja uchafuzi mkubwa wa mazingira ambao ni chanzo cha maafa na umaskini wa hali na kipato. Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko aliowaandikia washiriki wa Mkutano wa Kimataifa kuhusu usawa wa dunia.

Mkutano huu umefunguliwa hapo tarehe 28 na unahitimishwa tarehe 31 Januari 2019 huko Havana, nchini Cuba. Maadhimisho yamefunguliwa wakati Cuba inaadhimisha Siku ya Kuzaliwa kwa Josè Martì. Lengo kuu ni kuiwezesha Jumuiya ya Kimataifa kuunganisha nguvu kwa njia ya majadiliano yatakayowezesha kuimarisha mafungamano ya udugu kati ya Mataifa. Inatosha kuangalia matukio yaliyojiri kutoka sehemu mbali mbali za dunia kwa siku za hivi karibuni yanayotishia usawa wa ustaarabu mamboleo.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, ni kutokana na changamoto hizi, watu wenye mapenzi mema, wanapaswa kukutana, ili kufanya tafakari ya kina na hatimaye, kuchukua hatua zitakazosaidia kukuza na kudumisha maendeleo fungamani; utu, heshima na haki msingi za binadamu na kama sehemu ya ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Mazingira ya mwanadamu na mazingira asili huzorota pamoja. Haitawezekana kukabiliana na uharibifu mkubwa wa mazingira, bila kushughulikia na kudhibiti mambo yanayowatumbukiza watu wengi katika dimbwi la umaskini.

Utamaduni wa watu kukutana ni muhimu sana, hasa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya ili kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kijamii, kwa ajili ya mchakato unaopania kumwendeleza mwanadamu. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Josè Martì, Muasisi wa Cuba alikuwa ni kiongozi mwenye upeo mkubwa alikazia umoja na mshikamano wa kidugu unaofumbatwa katika upendo unaochanua na kutoa matunda ya amani kwa ajili ya watu wote. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, mkutano huu umetoa nafasi kwa wajumbe kuweza kutafakari na kwamba, matunda yake, yataonekana kwa wakati muafaka!

Papa: Ujumbe Cuba 2019

 

 

 

31 January 2019, 15:50