Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anampongeza Bwana Kiko Argùello kwa kuadhimisha miaka 80 tangu alipozaliwa. Papa Francisko anampongeza Bwana Kiko Argùello kwa kuadhimisha miaka 80 tangu alipozaliwa. 

Papa Francisko ampongeza Kiko: Miaka 80 ya kuzaliwa!

Bwana Kiko Argùello, ameadhimisha kumbu kumbu ya miaka 80 ya kuzaliwa kwake kwa Ibada ya Misa pamoja na kupata chakula cha mchana na marafiki pamoja na wajuani wake wa karibu. Baba Mtakatifu anamshukuru na kumpongeza Kiko Argùello, kwa uaminifu wake kwa Kristo na Kanisa lake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amemtumia salam na matashi mema Bwana Kiko Argùello, muasisi wa Chama cha Kitume cha Njia ya Ukatekumeni mpya anayeadhimisha kumbu kumbu ya miaka 80 tangu alipozaliwa. Baba Mtakatifu anamshukuru kwa ari na moyo mkuu katika kulitumikia Kanisa la Kristo na kwamba, Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo, amlipe ujira unaostahili kwa wema na ukarimu anaolitendea Kanisa la Kristo.

Bwana Kiko Argùello, ameadhimisha kumbukumbu ya miaka 80 ya kuzaliwa kwake kwa Ibada ya Misa pamoja na kupata chakula cha mchana na marafiki pamoja na wajuani wake wa karibu. Baba Mtakatifu anamshukuru na kumpongeza Kiko Argùello, kwa uaminifu wake kwa Kristo na Kanisa lake. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, wanachama wa Njia ya Ukatekumeni mpya wamemfanyia sherehe kubwa. Anamwomba, azidi kumkumbuka na kumsindikiza katika maisha na utume wake kwa njia ya sala na sadaka yake. Apate neema na baraka kutoka kwa Kristo Yesu; ulinzi na tunza kutoka kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, jumuiya inayosimikwa katika imani, matumaini na mapendo thabiti inakuwa ni chemchemi ya miito mitakatifu, ari na mwamko mpya wa kimisionari. Hii inatokana na ukweli kwamba, neema ya utume inabubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo, inayowakirimia waamini ari na nguvu ya kuwa kweli ni wamisionari. Waamini walei wanahamasishwa kuwa ni wamisionari kwa watu wanaowazunguka kwa kuwasikiliza na kuwapatia huduma: kiroho na kimwili; kwani ushuhuda wenye mvuto na mashiko ni chachu ya Uinjilishaji mpya inayokolezwa na Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa.

Ushuhuda wa Kanisa unafumbatwa katika huduma makini kwa maskini wa kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu Francisko anawataka wanachama wa Njia ya Ukatekumeni Mpya, (Neocatecumenale) kuwasaidia na kuwaendeleza watoto wao katika  maisha ya kiroho na utu wema, kwani wao ni jeuri na matumaini ya Kanisa la Kristo! Wajitahidi kuwafunda ili hatimaye, waweze kuwa ni wakristo watakatifu na raia wema zaidi. Njia ya Ukatekumeni Mpya ilianzishwa kunako mwaka 1968 huko Madrid, nchini Hispania. Wanachama wake wa kwanza ni watu waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na umaskini pamoja na changamoto mbali mbali walizokumbana nazo katika maisha.

Bwana Francisco Josè Gomes Arguello Wirtz, maarufu kama “Kiko” akajitosa kutangaza na kushuhudia Fumbo la Pasaka na kwa msaada wa Roho Mtakatifu akaanzisha Njia ya Ukatekumeni Mpya, mchakato wa maisha ya wakristo wa Kanisa la Mwanzo. Bwana Francisco Josè Gomes Arguello katika safari ya maisha yake, alitikiswa sana, hatimaye, akagundua mateso na mahangaiko ya watu wasiokuwa na hatia katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, changamoto iliyomfanya kuacha yote na kuanza kuandamana na maskini na watu waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii.

Hayati Mama Carmen Hernàndez, mtaalam wa masuala ya kemikali kutoka Hispania, aligundua upya wa maisha uliokuwa unabubujika kutoka katika Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Umaskini, Taalimungu na Ushuhuda wa Kerigima ya Katekesi yakawa ni mambo msingi yaliyotoa dira na mwongozo wa maisha na utume wa Njia ya Ukatekumeni Mpya, ulioanza kuenea kwa kasi kubwa nchini Hispania na baadaye sehemu mbali mbali za dunia. Mama Carmen Hernàndez akafariki dunia tarehe 19 Julai 2016 baada ya juhudi kubwa ya kupandikiza Neno la Mungu katika nyoyo na akili za watu!

Njia ya Ukatekumeni Mpya ni matunda ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, changamoto iliyotolewa kwa namna ya pekee na Mtakatifu Paulo VI, akiwataka wanachama hawa kukita maisha yao katika ukweli wa maisha ya Kikristo, chemchemi ya furaha, matumaini na ushuhuda unaotolewa na wanachama hawa. Wakristo wanaofuata Njia ya Ukatekumeni Mpya wanapaswa kwa namna ya pekee kabisa anasema Mtakatifu Paulo VI kujikita katika ukweli, uhalisia na utimilifu wa maisha ya Kikristo, chimbuko la chemchemi ya ushuhuda wa furaha na matumaini kwa wale wote wanaokutana nao katika hija ya maisha na utume wao.

Mtakatifu Yohane Paulo II katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, akawatia shime kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu wa kimisionari, akiwataka pia kulea na kukuza miito ya kimisionari. Mtakatifu Yohane Paulo II akatambua na kuandika kwamba, asili ya chama hiki cha kitume cha Njia ya Ukatekumeni Mpya ni mwendelezo wa mchakato wa majiundo makini ya kikatoliki, muhimu sana kwa watu wa Mungu kwa nyakati hizi. Mtakatifu Yohane Paulo II akawataka Maaskofu kuthamini mchango na huduma iliyokuwa inatolewa na wanachama wa Njia ya Ukatekumeni Mpya kama sehemu muhimu sana ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Njia ya Ukatekumeni Mpya inapata chimbuko lake katika Neno la Mungu, Liturujia ya Kanisa na Maisha ya Kijumuiya yanayosaidia kurutubisha na kujenga udugu na ukomavu wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, imani ambayo inapaswa kumwilishwa katika matendo.

Huu ni uzoefu na mang’amuzi ya maisha na utume wa Kanisa, changamoto iliyoibuliwa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, ikapokelewa kwa moyo wa shukrani na unyenyekevu mkuu na Askofu mkuu Casimiro Morcillo wa Jimbo kuu la Madrid kwa wakati ule na hatimaye, kama moshi wa ubani, Njia ya Ukatekumeni Mpya ukaenea pole pole na harufu yake kuijaza Hispania hadi kufikia “miisho ya dunia.” Mtakatifu Yohane Pualo wa Pili, kunako mwaka 1986 akabahatika kuona matunda ya kuanzishwa kwa Seminari ya kwanza ya Redemptoris Mater, lakini kabla ya hapo, mwaka 1984 na mwaka 1986, bahari ya vijana kutoka katika Njia ya Ukatekumeni mpya wakafurika mjini Vatican kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Kwanza ya Vijana Duniani na Jubilei ya Vijana na huo ukawa ni moto wa kuotea mbali.

Njia ya Ukatekumeni Mpya ikawa ni chemchemi ya miito mitakatifu, vijana wengi wakaamua kufunga ndoa, ili kutangaza na kushuhudia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; baadhi ya wao wakajiunga na wito wa kipadre na kitawa, ili waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu, watangazaji mahiri wa Neno la Mungu na wagawaji wa Mafumbo ya Kanisa. Mtakatifu Yohane Paulo II akaanzisha mchakato wa kuandika Katiba ya Njia ya Ukatekumeni Mpya iliyopitishwa na kuridhiwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kunako mwaka 2008. Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa kunako mwaka 2010 likapitisha na kuidhinisha Mwongozo wa Katekesi ya Njia ya Ukatekumeni Mpya.

Leo hii, Njia ya Ukatekumeni Mpya Barani Afrika imeenea huko Sudan Kongwe, Kenya, Uganda, Tanzania, Burundi, Rwanda, Zambia, DRC., Angola, Msumbiji, Pwani ya Pembe, Cameroon, Madagascar, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati,  na Afrika ya Kusini. Njia ya Ukatekumeni Mpya una mahusiano mazuri na Vatican pamoja na Maaskofu kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Jimbo kuu la Roma kuna Parokia 104 ambazo zinaundwa na Jumuiya 477, ambazo kwa hakika zimejazwa na vijana wa kizazi kipya wanaotaka kukuza na kuimarisha imani yao, ili kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu.

Kiko Miaka 80
10 January 2019, 16:15