Tafuta

Papa Francisko, tarehe 18 Januari 2019 anatarajia kuongoza Masifu ya Jioni, Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo 2019 Papa Francisko, tarehe 18 Januari 2019 anatarajia kuongoza Masifu ya Jioni, Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo 2019 

Papa Francisko: Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo 2019

Ijumaa tarehe 18 Januari 2019, Papa Francisko anatarajiwa kuongoza Ibada ya Masifu ya Jioni kwa ajili ya kufungua Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo linalohitimishwa kwa Siku kuu ya Kuongoka kwa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa. Maadhimisho haya kwa Mwaka 2019 yanaongozwa na kauli mbiu “Yaliyo ya haki kabisa ndiyo utakayoyafuata”. Kumb. 16:18-20.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 18 Januari 2019, anatarajiwa kuongoza Ibada ya Masifu ya Jioni kwa ajili ya kufungua Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo linalohitimishwa kwa Siku kuu ya Kuongoka kwa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 25 Januari. Maadhimisho haya kwa Mwaka 2019 yanaongozwa na kauli mbiu “Yaliyo ya haki kabisa ndiyo utakayoyafuata”. Kumb. 16:18-20.

Sehemu hii ya Maandiko Matakatifu inakazia: haki kati ya watu wa Mungu; inakataza rushwa na ufisadi; kwani rushwa hupofusha macho ya wenye akili, na kugeuza daawa ya wenye haki. Wakristo wanahamasishwa kutafuta haki na kuiambata ili waweze kuirithi nchi ya ahadi wapewayo na Mwenyezi Mungu. Tafakari ya Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo kwa mwaka huu, imeandaliwa na Wakristo kutoka nchini Indonesia, yenye watu zaidi ya milioni 265, na kati yao, asilimia 85% ni waamini wa dini ya Kiislam.

Asilimia 10% ni Wakristo kutoka katika Makanisa na Madhehebu mbali mbali ya Kikristo. Indonesia inasimikwa katika msingi wa umoja katika utofauti unaojikita katika masuala ya: kikabila, lugha na dini za watu. Licha ya tofauti zao msingi, familia ya Mungu nchini Indonesia inaendelea kujikita mchakato wa ushirikiano na umoja ili kupambana na matatizo na changamoto mamboleo, ili kuweza kudumisha haki jamii, ustawi na maendeleo ya wengi. Tafakari ya Juma la Kuombea Umoja wa Kanisa inaandaliwa kwa ushirikiano kati ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni na Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo.

Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, anaendelea kutoa kipaumbele cha pekee kwa majadiliano ya kiekumene, ili Makanisa yaweze kutembea yakiwa yameshikamana; yanasali na kushirikiana katika huduma makini kwa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Majadiliano ya kiekumene hayana budi kujikita katika utakatifu wa maisha, ushuhuda wa uinjilishaji unaowawezesha wakristo kupambana na changamoto mbali mbali za maisha pamoja na utamadunisho ili kweli Injili ya Kristo iweze kuenea miongoni mwa watu wa Mataifa.

Baba Mtakatifu anawataka Wakristo kuwa ni vyombo na mashuhuda wa upendo wa kiinjili kati yao na kati ya watu wa Mataifa, ili kujenga na kudumisha umoja na udugu, alama yenye mvuto na mashiko kwa Kanisa na jamii katika ujumla wake, na kama sehemu muhimu sana ya mapambano dhidi ya changamoto mamboleo. Wakristo kama ilivyokuwa kwa nyakati za Mtakatifu Paulo wanapaswa kujitahidi kuungana pamoja kwa njia ya mawazo na maneno na kwamba, umoja huu si mkakati wa kibinadamu bali ni changamoto kutoka kwa Kristo mwenyewe, anayewavuta wafuasi wake kuungana sanjari na kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu, ili aweze kutenda kadiri ya mapenzi yake yanayojikita katika upendo kwa mwanadamu. Mwenyezi Mungu ndiye kiini, sababu na kikolezo cha umoja miongoni mwa Wakristo.

Utengano miongoni mwa Wakristo si jambo la kawaida anasema Baba Mtakatifu Francisko, linahitaji kufanyiwa marekebisho ya kina, kwani utengano kati ya Wakristo una madhara makubwa katika Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Unahatarisha ushuhuda unaopaswa kutolewa na Wakristo duniani. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Kristo ndiye msingi wa Kanisa na urithi wa wakristo wote. Lakini inasikitisha kuona kwamba, bado Wakristo wenyewe wamegawanyika kinyume kabisa cha utashi wa Kristo mwenyewe na utengano huu unaendelea kuwa ni kielelezo cha kashfa ya ushuhuda wa utangazaji wa Injili duniani. Baba Mtakatifu anawatia shime Wakristo kufanya hija pamoja na kutegemezana ili kujenga na kuimarisha umoja miongoni mwa Wakristo.

Katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, dhana ya Khalifa wa Mtakatifu Petro imejidhihirisha wazi, mwaliko wa kuendelea kufahamiana zaidi kwa ajili ya majadiliano ya Kiekumene kwa kutambua utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, hata kwa siku za usoni. Changamoto na vikwazo vinavyoendelea kujitokeza katika majadiliano ya Kiekumene ni mambo ambayo hayawezi kufichika, lakini kuna haja kwa Wakristo wapige kupiga moyo konde na kuanza kujivika utashi wa Kristo kwa ajili ya umoja miongoni mwa Wakristo. Wawe tayari kuvuka vikwazo vyote vinavyosababisha utengano na hivyo kujivika nguvu ya upendo inayotolewa na Roho Mtakatifu kwa ajili ya Kanisa.

Papa: Umoja wa Wakristo
09 January 2019, 08:44