Tafuta

Papa Francisko anatarajiwa kutembelea Romania kuanzia tarehe 31 Mei- 2 juni 2019 kwa mwaliko wa Serikali na Kanisa. Papa Francisko anatarajiwa kutembelea Romania kuanzia tarehe 31 Mei- 2 juni 2019 kwa mwaliko wa Serikali na Kanisa. 

Papa kutembelea Romania: Tarehe 31 Mei - 2 Juni 2019

Papa Francisko atatembelea Romania kuanzia tarehe 31 Mei, Siku kuu ya Bikira Maria kumtembelea Elizabeti hadi tarehe 2 Juni 2019, Kanisa, sehemu mbali mbali za dunia, linapoadhimisha Siku kuu ya Kupaa Bwana Mbinguni. Papa atafanya hija katika mji mkuu wa Bucharest, mji wa Ias ulioko Kaskazini wa Romania pamoja na mji wa Blaj, Kituo kikuu cha utamaduni nchini Romania.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 31 Mei anasherehekea Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu kumtembelea binamu yake Elizabeti. Ni siku ya kufunga pia Mwezi wa Rozari takatifu, kwa changamoto ya kuendelea kusali Rozari kwani huu ni muhtasari wa Injili na matendo makuu ya Mungu katika historia ya mwanadamu. Kumbu kumbu ya Bikira Maria kumtembelea Elizabeti ni mwendelezo wa utenzi wa sifa, shukrani na furaha ya ujio wa Masiha unaotambuliwa na Yohane Mbatizaji. Hapa Bikira Maria anaoneshwa kama Tabernakulo na Sanduku la Agano Jipya na la Milele.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko amekubali mwaliko kutoka kwa Serikali pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki, ili kutembelea Romania kuanzia tarehe 31 Mei, Siku kuu ya Bikira Maria kumtembelea Elizabeti hadi tarehe 2 Juni 2019, Kanisa, sehemu mbali mbali za dunia, linapoadhimisha Siku kuu ya Kupaa Bwana Mbinguni. Katika hija hii ya kitume, Baba Mtakatifu atatembelea mji mkuu wa Bucharest, mji wa Ias ulioko Kaskazini wa Romania pamoja na mji wa Blaj, Kituo kikuu cha utamaduni nchini Romania kati ya karne 18-19 na hapa pia ni mwanzo wa tafsiri ya Biblia ya Blaj.

Baba Mtakatifu akiwa nchini Romania, atatembelea Madhabahu ya “Șumuleu Ciuc” yaani Bikira Maria Mfariji wa wanaoteseka. Hija hii ya kitume inaongozwa na kauli mbiu “Twende pamoja”, mwaliko kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kutembea kwa pamoja chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, kwa kukataa kishawishi cha uchoyo na ubinafsi, ili kutoa kipaumbele cha kwanza kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu anatembelea Romania ili kuimarisha imani miongoni mwa ndugu zake katika Kristo sanjari na kukazia umoja na mshikamano wa familia ya Mungu nchini Romania.

Itakumbukwa kwamba, mara ya mwisho, Romania ilitembelewa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1999 na watu wengi wanaifananisha Romania na “Bustani ya Mama wa Mungu”. Hili lilikuwa ni tukio la kihistoria tangu Kanisa lilipotengana kunako mwaka 1054 na huo ukawa ni mwanzo wa kuibuka kwa Makanisa na Madhehebu mbali mbali ya Kikristo! Baba Mtakatifu Francisko atafanya hija ya kitume nchini Romania wakati wa Siku kuu ya Bikira Maria Kumtembelea Elizabeti yaani Mama wa Mungu ndiye anayetoka kwa haraka kwenda kumtembelea Elizabeti. Hapa wanawake wawili wanaohifadhi ndani mwao zawadi ya maisha wanakutana Bikira Maria ni mtumishi wa Bwana na Elizabeti ni kielelezo cha matumaini mapya kwa Waisraeli na huduma ya Injili ya upendo kwa jirani na mfano wa kuigwa hasa katika ulimwengu mamboleo uliogubikwa na ubinafsi na uchoyo.

Yohane Mbatizaji anaruka kwa shangwe tumboni mwa mama yake Elizabeti, ushuhuda makini wa kufunguliwa kwa ukurasa mpya naye ndiye atakayekuwa Nabii na daraja kati ya Agano la Kale na Agano Jipya. Ni mtangulizi wa Masiha na Mkombozi wa ulimwengu, changamoto na mwaliko wa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya upendo na ukarimu kwa jirani! Ratiba elekezi ya hija za Baba Mtakatifu Francisko kwa mwaka 2019 inaonesha kwamba, Mwezi Januari atatembelea Panama, baadaye atakwenda Falme za Kiarabu, Morocco, Bulgaria na Yugoslavia ya zamani. Familia ya Mungu Barani Afrika ina shahuku kubwa ya kusikia lini tena Baba Mtakatifu ataitembelea!

Papa: Romania 2019
11 January 2019, 13:50