Tafuta

Papa Francisko anawataka viongozi wa Kanisa kusikiliza kwa makini na kujibu kilio cha maskini sehemu mbali mbali za dunia! Papa Francisko anawataka viongozi wa Kanisa kusikiliza kwa makini na kujibu kilio cha maskini sehemu mbali mbali za dunia! 

Papa Francisko: Sikilizeni na kujibu kilio cha maskini!

Umuhimu wa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini; majadiliano ya kiekumene katika sala; majadiliano na mafungamano ya kijamii kati ya wazee na vijana; maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa; utekelezaji wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, elimu bora na majadiliano katika shughuli za kichungaji ni kati ya mambo ambayo Papa alikazia wakati wa mazungumzo na Wayesuit, Lithuania.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni, wakati wa hija yake ya kitume huko Lithuania, alipata bahati ya kuzungumza na Wayesuit kutoka Ukanda wa Baltic waliofika kushiriki katika hija hii. Hili ni Shirika ambalo lilikumbana na “pazia la chuma” kutoka katika utawala wa Kikomunisti, uliosigina uhuru wa kidini. Lakini, tangu baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, wameendelea kuwekeza katika mchakato wa maboresho ya maisha ya kiroho, elimu makini sanjari na majadiliano ya kiekumene.

Umuhimu wa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini; majadiliano ya kiekumene katika sala; majadiliano na mafungamano ya kijamii kati ya wazee na vijana wa kizazi kipya; maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa; utekelezaji wa maamuzi ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, elimu bora na majadiliano katika shughuli za kichungaji ni kati ya mambo ambayo Baba Mtakatifu aligusia wakati wa mazungumzo yake na Wayesuit huko Lithuania.

Baba Mtakatifu aliwataka Wayesuit kufanya mang’amuzi kuhusu maisha na utume wao, tayari kuchagua vipaumbele ambavyo watavifanyia kazi kwa weledi mkubwa zaidi, daima wakijitahidi kutunza amani na utulivu wa ndani; uhusiano wa karibu na Kristo Yesu kwa njia ya: sala, tafakari na maisha ya kisakramenti pamoja na kupata muda wa mapumziko! Wajesuit wajitahidi kutekeleza yale yanayotekelezeka, daima wakiwa wanajiweka chini ya ulinzi na maongozi ya Kristo mwenyewe, ili kukuza na kudumisha amani! Baba Mtakatifu anasema, hizi ni kanuni tatu zinazowaongoza Wayesuit katika maisha na utume wao!

Baba Mtakatifu amewataka Wayesuit, kujizamisha katika mahangaiko ya watu, ili kusikiliza na hatimaye, kujibu kilio na matamanio yao halali; tayari kuganga na kuponya madonda, makovu na machungu ya utawala wa Kikomunisti nchini Lithuania. Kuna watu wanaohangaika na kuteseka sana kutokana na biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Kuna wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi katika nchi zilizoendelea, lakini, wakiwa njiani wanakumbana na vizingiti na wengi wao, wanapoteza maisha kwa kufa maji kwenye Bahari ya Mediterrania.

Wafanyabiashara haramu ya binadamu wamejenga ngome za kutisha wanamosulubiwa watu! Huu ni mwendelezo wa mateso ya Kristo Yesu yanayojionesha kati ya watu wake, kumbe, changamoto na mwaliko wa kusikiliza kilio chao na kuwapatia majibu muafaka! Baba Mtakatifu anawaalika waamini kutafakari kwa kina na mapana Njia ya Msalaba, ili kuwakumbusha tena na tena mateso ya Yesu yanayoendelea kati ya waja wake.

Baba Mtakatifu anawataka Wayesuit kukuza na kudumisha ari na mwamko wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika maisha ya sala na tafakari ya Neno la Mungu, daima wakiwa tayari kusikiliza sauti ya Roho Mtakatifu kwa ajili ya Kanisa la Kristo! Majadiliano katika ukweli na uwazi ni chachu ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu. Baba Mtakatifu anawahamasisha vijana wa kizazi kipya kutafuta nafasi ya upweke chanya, ili kusali, kutafakari na kufanya mang’amuzi ya maisha yao.

Viongozi wa Kanisa wajenge sanaa na utamaduni wa majadiliano kati ya wazee na vijana wa kizazi kipya ili kuwashirikisha tunu msingi za maisha ya Kikristo, maadili na utu wema, mambo msingi yatakayowasaidia vijana kumwilisha ndoto zao katika uhalisia wa mambo. Utume wa Kanisa kwa vijana unafumbatwa katika mambo makuu matatu: kuwasikiliza, kuwasindikiza na kuwasaidia vijana kufanya mang’amuzi makini katika maisha na wito wao. Vijana ni amana na utajiri wa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Wazazi kwa kushirikiana vyema na wazee wanaweza kuwasaidia malezi na majiundo bora zaidi ya vijana wa kizazi kipya, jambo la msingi ni marika haya kujenga utamaduni wa majadiliano unaofumbatwa katika sanaa na utamaduni wa kusikilizana!

Baba Mtakatifu anawataka wakleri ambao ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu, kuonesha uwepo wa Mungu katika maisha ya waja wake kwa njia ya: tafakari makini ya Neno la Mungu; maadhimisho na ushiriki mkamilifu wa watu wa Mungu katika Sakramenti za Kanisa kwa kutambua kwamba, Sakramenti ya Upatanisho ni chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake! Kanisa linahitaji waungamishaji, watakaosaidia waamini kuonja huruma na msamaha wa dhambi zao, kama ilivyokuwa katika Injili ya Baba mwenye huruma kwa Mwana mpotevu! Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ni mwaliko kwa waamini kujisadaka kwa ajili ya huduma makini kwa jirani zao kama kielelezo cha imani tendaji na uwepo wa Mungu unaoshuhudiwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili!

Wajesuit wanampongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuendelea kujisadaka kwa ajili ya maendeleo, ustawi na mafao ya wengi kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa: maskini ambao ni amana na utajiri wa maisha na utume wa Kanisa, Injili ya familia dhidi ya utamaduni wa kifo; haki na amani sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu anawataka wakleri kuzama zaidi katika toba na wongofu wa kimisionari, ili kuhakikisha kwamba, Kanisa kama familia ya Mungu linamwilisha sera na mikakati ya shughuli za kichungaji iliyopembuliwa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Msaada mkubwa ambao familia ya Mungu inaweza kuutoa kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro ni kuendeleza maisha na utume wa Kanisa kwa hali na mali; kwa kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kanisa lihakikishe kwamba, linatoa elimu bora na makini kwa vijana wa kizazi kipya, ili kuwasaidia vijana kuweza kupambana na mazingira yao, kwa kuhakikisha kwamba, elimu inasaidia kumfunda mtu mzima; kiroho, kiakili, katika kuamua na kutenda! Shule, taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu viwe ni mahali pa majadiliano na majiundo kwa vijana wa kizazi kipya. Baba Mtakatifu anawataka Wayesuit kuendelea kujizatiti kwa kuwekeza zaidi katika sekta ya elimu!

Baba Mtakatifu katika mazungumzo yake na Wayesuit huko Lithuania amewakumbusha kwamba, Kanisa linapaswa kutoka sakristia, ilikuwaendelea watu walioko pembezoni mwa vipaumbele vya maisha ya kijamii, ili kuwaonjesha furaha ya Injili, kwa kutambua kwamba, Kanisa ni kama hospitali iliyoko kwenye uwanja wa mapambano, kumbe, inapaswa kuwa ni alama ya huruma na upendo. Hakuna sababu ya kuogopa, bali viongozi wa Kanisa wawe na jeuri na ujasiri wa kutoka ili kuwaendea watu!

Katika mapambano ya utekelezaji wa shughuli za kichungaji, daima viongozi wa Kanisa wajiaminishe kwa Kristo kwa njia ya sala na majadiliano ya kina na Jumuiya zao ili kushirikishana mang’amuzi, uzoefu na changamoto zinazojitokeza katika maisha na utume wa Kanisa; katika ukweli na uwazi; kwa kusikilizana na kusaidiana. Huu ni wakati w akujenga na kudumisha maisha ya kijumuiya yanayofumbatwa katika udugu na mshikamano wa dhati. Anawaalika Wayesuit kusoma tena na tena nyaraka za Mtakatifu Paulo VI aliyetangazwa hivi karibuni kama sehemu ya rejea katika maisha na utume wao sehemu mbali mbali za dunia, daima wajuvie katika maisha na utume wa sala!

Papa & Wayesuit
16 January 2019, 06:50