Ratiba elekezi ya maisha na utume wa Papa Francisko kwa mwaka 2019 Ratiba elekezi ya maisha na utume wa Papa Francisko kwa mwaka 2019 

Papa Francisko: Maisha na utume wake kwa mwaka 2019

Baba Mtakatifu Francisko kwa mwaka 2019 inaonesha kwamba, anatarajia kufanya hija ya kitume kwenye Falme za Kiarabu; Kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani, huko Panama; kutembelea Morocco, Bulgaria na Yugoslavia ya zamani. Anatarajia kushiriki katika mkutano wa Kanisa kuhusu nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto pamoja na Sinodi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Siasa safi ni huduma ya amani ndiyo kauli mbiu iliyoongoza ujumbe wa Siku 52 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2019. Kwa muhtasari Baba Mtakatifu Francisko, anakazia Injili ya amani kama sehemu ya utume wa Kanisa; Changamoto za siasa safi; Upendo na fadhila za kiutu kwa ajili ya siasa inayohudumia haki msingi na amani; vilema vya wanasiasa; umuhimu wa siasa safi inayowashirikisha vijana na kujengeana imani; anasema, kuna haja ya kukataa kishawishi cha vita na mbinu mkakati wa vitisho, kwa kuwekeza katika mradi mkubwa wa ujenzi wa amani.

Ujumbe wa Noeli kwa mwaka 2018, kutoka kwa Baba Mtakatifu, unafumbatwa katika udugu kati ya watu wa mataifa na tamaduni; watu wenye mawazo tofauti, lakini wenye uwezo wa kuheshimiana na kusikilizana; udugu kwa watu wa dini mbali mbali, kwani Kristo Yesu amekuja ulimwenguni ili kuwafunulia Uso wa Mungu, wale wote wanaomtafuta Mwenyezi Mungu katika hija ya maisha yao. Ratiba elekezi ya maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko kwa mwaka 2019 inaonesha kwamba, anatarajia kufanya hija ya kitume kwenye Falme za Kiarabu; Kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani, huko Panama. Baba Mtakatifu anatarajia kutembelea Morocco, Bulgaria na Yugoslavia ya zamani. Kati ya matukio makubwa yaliyoko mbele yake ni pamoja na mkutano wa Kanisa kuhusu nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo utakaofanyika mwezi Februari pamoja na Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Ukanda wa Amazonia, itakayoadhimishwa Mwezi Oktoba, 2019.

Lakini, mapema mwezi Januari, Baba Mtakatifu anatarajia kukutana na kuzungumza na Wanadiplomasia wanaowakilisha nchi na mashirika ya kimataifa hapa mjini Vatican. Mwaka, 2018, alikazia umuhimu wa Haki Msingi za Binadamu kama sehemu ya ujenzi wa amani na maendeleo fungamani ya binadamu! Januari mwaka 2019, Panama itakuwa ni gumzo la watu wa mataifa kutokana na maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, yatakayowashirikisha vijana kutoka kila sehemu ya dunia. Ni muda wa kutafakari vipaumbele vya maisha na utume wa vijana, changamoto, matatizo na fursa walizo nazo kama mashuhuda na vyombo vya furaha ya Injili.

Maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 huko Panama, yataanza kutimua vumbi kuanzia tarehe 22–27 Januari 2019, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Mimi ni mtumishi wa Bwana nitendewe kama ulivyonena” Lk. 1:38. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa vijana wa kizazi kipya wanapoendelea kujiandaa kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 huko Panama anawakumbusha kwamba, mapinduzi ya huduma ndiyo nguvu ya vijana wa kizazi kipya!

Kuanzia tarehe 3 hadi 5 Februari 2019, Baba Mtakatifu Francisko atatembelea huko Abu Dhabi, kwenye Falme za Kiarabu ili kuhudhuria Mkutano wa Kimataifa wa majadiliano ya kidini utakaoongozwa na kauli mbiu "Udugu wa kibinadamu". Mwaka huu, umechaguliwa na Falme za Kiarabu kuwa ni mwaka wa maridhiano kati ya watu, kwa lengo na kutaka kukomesha vitendo vya kigaidi, ili kujenga na kudumisha umoja na udugu hata katika tofauti msingi za maisha!

Mbinu mkakati wa kuwalinda watoto dhidi ya nyanyaso za kijinsia unapania pia kuliwezesha Kanisa kujitakatifuza kwa kujikita katika maadili na utu wema, changamoto inayovaliwa njuga kwa wakati huu na Baba Mtakatifu Francisko, ambaye ameunda Kamati kuu itakayoratibu mkutano maalum wa Kanisa kwa ajili ya kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia utakaofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 21-24 Februari 2019. Mkutano huu utaongozwa na mambo makuu matatu: uwajibikaji, dhamana ya uwajibikaji; ukweli na uwazi. Hapa Kanisa linahimiza toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha.

Baba Mtakatifu Francisko amekubali mwaliko uliotolewa kwake na Mfalme Mohammed VI pamoja na Maaskofu Katoliki nchini Morocco, kutembelea nchi yao kuanzia tarehe 30-31 Machi 2019. Katika hija hii ya kitume, Baba Mtakatifu anatarajiwa kutembelea mji wa Rabat na Casablanca. Baba Mtakatifu anataka kuendeleza majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali duniani, ili kujenga na kudumisha umoja, upendo, haki na mshikamano wa dhati na kwamba, tofauti zisiwe ni chanzo cha vurugu na mitafaruku ya kijamii na kidini. Mkazo ni haki msingi za binadamu, uhuru wa kuabudu, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Kuanzia tarehe 5-7 Mei 2019 Baba Mtakatifu anatarajiwa kutembelea Bulgaria pamoja na Yugoslavia ya zamani, mahali alikozaliwa Mtakatifu Mama Theresa wa Calcutta, shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa maskini! Hija hii inaongozwa na kauli mbiu “Msiogope enyi kundi dogo” LK. 12:23. Wakati huo huo, Hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Bulgaria inaongozwa na kauli mbiu “Pacem in terris”, yaani “Amani duniani”, mwangwi wa Waraka wa Kitume wa Mtakatifu Yohane XXIII “Pacem in terris” anayekazia umuhimu wa haki, uhuru, ukweli, upendo na msamaha kama mambo msingi ya kujenga na kudumisha amani duniani sanjari na kukuza mahusiano mema kati ya wananchi na viongozi wao, Jumuiya za kisiasa na ulimwengu katika ujumla wake.

Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia yatakayofanyika mjini Vatican mwezi Oktoba 2019 kwa kuongozwa na kauli mbiu "Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ya ekolojia fungamani". Hati ya maandalizi ya Sinodi ya Amazonia inakazia umuhimu wa: kuona, kung'amua na kutenda! Ni Sinodi itakayopembua tema mbali mbali:kuhusu: haki jamii, malezi, katekesi, liturujia na utambulisho wa Kanisa katika Ukanda wa Amazonia. Kati ya mambo ambayo Baba Mtakatifu anatamani kuyatekeleza ni pamoja na Hija ya Kitume nchini Japan.

Papa Francisko mwaka 2019
02 January 2019, 08:48