Cerca

Vatican News
Papa Francisko: Kristo Yesu, Bwana harusi ni chemchemi ya furaha ya kweli katika maisha! Papa Francisko: Kristo Yesu, Bwana harusi ni chemchemi ya furaha ya kweli katika maisha!  (Vatican Media)

Papa Francisko: Kristo Yesu ni chemchemi ya furaha ya kweli!

Kumhudumia Kristo Yesu, maana yake ni kusikiliza kwa makini maneno yake na kuyamwilisha katika uhalisia wa maisha. Hili ni ombi kutoka kwa Bikira Maria ambalo linakuwa sasa ni sehemu ya programu ya maisha ya Mkristo! Katika mahangaiko ya maisha na hali ya kukata tamaa, Baba Mtakatifu anawashauri waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumkimbilia Bikira Maria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kipindi cha Mwaka wa Kanisa ni safari ya kumfuasa Kristo Yesu katika maisha yake ya hadhara na utume katika kuwatangazia watu Habari Njema ya Wokovu. Akiwa kwenye harusi ya Kana, mji wa Galilaya, Kristo Yesu anafanya muujiza wake wa kwanza, kielelezo kwamba, Mwenyezi Mungu amefunga ndoa na watu wake. Hiki ni kiini cha Habari Njema, ingawa wale waliokuwepo harusini, hawakutambua kwamba, kati yao, alikuwepo Mwana wa Mungu, ambaye kimsingi ndiye Bwana harusi.

Muujiza wa harusi ya Kana ya Galilaya unafumbatwa kwa uwepo wa Kristo Yesu anayejifunua kati ya watu wake kama Bwana harusi, aliyetangazwa na kushuhudiwa na Manabii na kwamba, Yeye ndiye kiini cha Agano Jipya linalojikita katika upendo. Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 20 Januari 2019, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Bikira Maria alipogundua kwamba, wanaharusi wanatindikiwa na divai, mara akamwendea Yesu na kumwambia kwamba, “hawana divai” na Yesu akatenda muujiza wake wa kwanza, kwa kugeuza maji kuwa divai. Maandiko Matakatifu yanaonesha kuwa, divai ni sehemu muhimu sana kwenye karamu ya Kimasiha, kwa sababu ni chemchemi ya furaha! Yesu anageuza Sheria ya Musa katika Injili ili kuwakirimia watu furaha ya kweli!

Baba Mtakatifu akielezea nafasi ya Bikira Maria katika muujiza huu, anasema kwamba, Bikira Maria aliwaambia wale watumishi: “Lo lote atakalowaambia, fanyeni”. Maneno haya ni amana na hazina kubwa ambayo Bikira Maria amewaachia wafuasi wa Kristo Yesu. Wale watumishi wakatii na kuyajaziliza maji hata juu na baadaye Yesu akawaamuru kuyateka na kumpelekea mkuu wa meza, hii ni alama ya Agano Jipya kati ya Kristo Yesu na Kanisa lake linalopaswa kuwa ni chombo cha huduma kwa ajili ya utume wake.

Kumhudumia Kristo Yesu, maana yake ni kusikiliza kwa makini maneno yake na kuyamwilisha katika uhalisia wa maisha. Hili ni ombi kutoka kwa Bikira Maria ambalo linakuwa sasa ni sehemu ya programu ya maisha ya Mkristo! Katika mahangaiko ya maisha na hali ya kukata tamaa, Baba Mtakatifu anawashauri waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumkimbilia Bikira Maria na kumwambia kwamba, “hawana divai” na Bikira Maria atamwendea Kristo Yesu na kumwambia! Kumbe, sasa utakuwa ni wajibu wa waamini kutenda kadiri watakavyokuwa wameagizwa na Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, kuchota maji kutoka kwenye mabalasi maana yake ni kujiaminisha kwa Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa ili kumwezesha mwamini kupata neema katika maisha yake, ili hatimaye, kufurahia upya wa maisha kama alivyosikika mkuu wa meza akiisifia ile divai mpya. Kwa hakika, Kristo Yesu anaendelea kuwashangaza wafuasi wake kila kukicha! Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa aendelee kuwasaidia waamini kutenda kadiri ya maelekezo ya Yesu, ili hatimaye, kujifunua kwake na kumtambua katika maisha ya kila siku pamoja na alama za uwepo wake hai unaojenga na kuwaimarisha watu wake!

Papa: Harusi ya Kana ya Galilaya
20 January 2019, 12:01