Papa Francisko: Kristo Yesu anapaswa kutangazwa na kushuhudiwa na wengi! Papa Francisko: Kristo Yesu anapaswa kutangazwa na kushuhudiwa na wengi! 

Papa: Yesu anapaswa kutangazwa na kushuhudiwa!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, ikiwa kama watu watajifunza historia na kumakinika, watageuka kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa watu wenye kiu ya ukweli, haki na amani duniani. Hapa watu wangeweza kujifunza athari ambazo vita imeacha katika mapito ya historia ya mawanadamu hapa duniani! Watu wamtangaze na kumshuhudia Kristo kwa vitendo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Chama cha Majaalimu wa Historia ya Kanisa nchini Italia, AIPSC, katika maadhimisho ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake kunako mwaka 1967, kilichapisha na kusambaza matokeo ya tafiti za historia ya Kanisa tangu baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Chama hiki kimetoa mchango mkubwa katika uelewa wa historia ya Kanisa kwa nyakati mbali mbali na kwa sasa kinaendelea kujielekeza katika historia ya Kanisa kijiografia pamoja na kuendelea kufanya semina, mikutano na makongamano katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 12 Januari 2019 amekutana na kuzungumza na Chama cha Majaalimu wa Historia ya Kanisa nchini Italia kwa kukazia kwamba, historia ni mwalimu wa maisha “historia magistra vitae”, lakini kwa bahati mbaya, hana wanafunzi wengi wanaojitaabisha kujifunza kutokana na historia kama anavyokumbusha Padre Giacomo Martina, Jaalimu wa historia ya Kanisa kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian.

Jambo la kufurahisha ni kuona kwamba, Chama hiki kina wanafunzi wengi wanaotoka Seminarini, taasisi za elimu ya juu na katika Vyuo Vikuu vya Kipapa. Kinaendesha shughuli zake kwa njia ya mikutano, makongamano na semina mbali mbali, chombo muhimu sana cha kueneza ukweli mintarafu historia ya Kanisa, ushuhuda wenye mvuto na mashiko anasema, Baba Mtakatifu Francisko. Ikiwa kama watu watajifunza historia na kumakinika, watageuka kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa watu wenye kiu ya ukweli, haki na amani duniani. Hapa watu wangeweza kujifunza athari ambazo vita imeacha katika mapito ya historia ya wanadamu hapa duniani!

Baba Mtakatifu anasema, Kanisa na kwa namna ya pekee nchini Italia, lina utajiri mkubwa wa shuhuda zilizopita. Huu ni utajiri na amana ya Kanisa inayopaswa kutumiwa kikamilifu ili kutembea vyema kwa wakati huu na hatimaye, kusonga mbele kwa wakati ujao. Kanisa nchini Italia ni kituo rejea kwa wale wote wanaotaka kufahamu na hatimaye, kufurahia historia iliyopita, bila kutaka kuihifadhi katika majumba ya makumbusho au mbaya zaidi, kuizika makaburini kama kumbu kumbu zilizopita, bali kutaka kuipyaisha na kuiweka tena mbele ya macho ya wengi.

Kiini cha historia ya mwanadamu ni Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na kutolewa na Mwenyezi Mungu kama zawadi ya ukombozi; Neno ambaye anapaswa kutangazwa na kushuhudiwa, ili kuwaletea watu mageuzi kutoka katika undani wa maisha yao. Ni Neno anayeendelea kutenda na kuleta mageuzi katika historia na maisha ya binadamu. Kristo Yesu ndiye kipimo kabla na baada yake na wala hakuna mwingine, mwaliko wa kupokea utume wake unaohurumua na kuokoa; kwa kuheshimu ukweli wake; kwa kumtafuta kwa ari na moyo mkuu na hatimaye, kumshuhudia katika mchakato wa kufundisha!

Mwelekeo huu wa historia ni kiboko kinachofyekelea mbali mitazamo ya kidunia ya kudhani kwamba, wanafahamu mambo yote; au kama “vigogo” wa taaluma au watu wanaosifika kwa weledi wao au kwa kuwa na kiburi cha kudhani kwamba, kama mtu binafsi anaweza kuwa hakimu wa watu na matuio mbali mbali. Mchakato wa kuvamia uwepo wa Kristo na safari ya Kanisa katika historia, unapasa kuwasaidia kuwa wanyenyekevu na hatimaye, kuwaondolea kile kishawishi cha kutaka kukimbilia katika mambo yaliyopita ili “kupotezea” na mambo ya sasa.

Baba Mtakatifu anawataka Majaalimu kwa njia ya ushuhuda wa maisha na taaluma yao, kuwasaidia watu kumtafakari Kristo Yesu, Jiwe kuu la pembeni anaendelea kutekeleza utume wake katika historia, katika kumbu kumbu za binadamu na tamaduni za watu mbali mbali. Kristo Yesu, awawezeshe kuonja uwepo wake unaookoa katika matendo, nyaraka na matukio mbali mbali katika maisha! Baba Mtakatifu anahitimisha hotuba yake kwa kusema, historia ya maskini na wanyonge katika jamii inapaswa kupewa kipaumbele cha pekee, kwani hata wao pia ni sehemu ya historia. Na kwa njia hii, wataweza kupata wanafunzi wengi, ambao ni wema, wakarimu na watu waliojiandaa barabara!

Papa: Historia ya Kanisa
12 January 2019, 16:27