Tafuta

Vatican News
Mwanga wa nyota,safari ya Mamajusi na zawadi kwa Yesu,ujasiri,hofu  hata zawadi ambazo tunapaswa kumtolea Yesu ni mada katika tafakari za Papa tangu 2014-1019 wakati wa Epifania Mwanga wa nyota,safari ya Mamajusi na zawadi kwa Yesu,ujasiri,hofu hata zawadi ambazo tunapaswa kumtolea Yesu ni mada katika tafakari za Papa tangu 2014-1019 wakati wa Epifania   (Vatican Media)

Tafakari juu ya safari ya Mamajusi kwa mujibu wa Papa Francisko!

Mada ambazo Baba Mtakatifu Francisko amejikita nazo katika Misa alizoadhimisha wakati wa Sikukuu ya Epifania ya Bwana tangu kuanza utume wake kama kharifa wa mtume Petro amejikita kutazama mwanga wa nyota, safari ya Mamajusi na zawadi kwa Yesu ambazo hata sisi tunapaswa kuzitoa katika maisha yetu, lakini pia tahadhali ya ulaghai na hofu za wakati ule

Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Mwanga wa nyota, safari ya Mamajusi, zawadi kwa Yesu ambazo hata sisi tunatoa katika maisha yetu, ulaghai wa dunia hii, hofu na mashaka, lakini pia ujasiri na mengineyo, ndizo mada kuu ambazo Baba Mtakatifu Francisko ameweza kujikita nazo wakati wa mahubiri ya Misa zake alizoadhimisha katika  Sikukuu ya Epifania ya Bwana tangu kuanza utume wake kama kharifa wa Mtume Petro 2013-2019.

Misa ya Epifania ya Bwana tarehe 6 Januari 2019, zawadi za Mamajusi

Baba Mtakatifu katika misa Takatifu amesema, kwa kutazama uzoefu wa Mamajusi  ( taz (Mt 2,1-12) walikuja kutoka mashariki ya mbali, wakiwakilisha watu wote walio mbali na imani ya utamaduni wa kiyahudi. Licha ya hayo waliacha waongozwe na nyota na kukabiliana na safari ndefu na hatari hatari ya kutoweza kufika na kujua ukweli wa Masiha. Walikuwa wamejifungulia mapya kwa maana hiyo walioneshwa yaliyo makuu na mshangao mpya wa historia.

Mungu alijifanya mtu na Mamajusi walimshuhudia Yesu na kumtolea zawadi muhimu ya dhahabu, uvumba na manemane. Hiyo ni kutokana na kwamba anayemtafuta Bwana si kwamba anavumilivu wa safari ndefu, bali hata kuwa na ukarimu wa moyo. hivyo hatimaye Mamajusi walirudi katika nchi yao (Mt 2,12) wakiwa wamejazwa ndani ya mioyoni mwao fumbo la yule Mfalme mnyenyekevu na maskini; Baba Mtakatifu anaongeza kusema, tunaweza kufikiria na kuthibitisha kuwa,  hawa walipata kusimulia uzoefu walioupata wa wokovu unaotoka kwa Mungu kwa njia ya Kristo na  kwamba aliuja kwa ajili ya wote, wawe  wa karibu na mbali. Na ni wokovu ambao siyo rahisi kuumiliki kama mtoto badala yake yeye ni zawadi kwa watu wote.

Mamajusi walimwona Yesu na wakati wa kurudi kwao walipitia njia nyingine (Mt 2,12). Kupitia njia nyingne  na  tofauti na ile ya Herode. Baba Mtakatifu anasema ni kutafuta njia mbadala katika dunia kama ile ambayo ilipitiwa na wale wote ambao katika Noeli wako na Yesu. Maria na Yosefu na wachungaji. Hawa ni kama Mamajusi ambao waliacha makazi yao na kujiweka katika hija, katika njia za Mungu. Hiyo ni kutokana kwamba, ni yule tu anaye acha mashiko ya ulimwengu huu na kujikita katika njia ya kutafuta fumbo la Mungu.

Misa ya Epifania ya Bwana tarehe 6 Januari   2018

Baba Mtakatifu alisema Mamajusi walithubutu, wakaondoka kwa kuifuata ile nyota,na hiyo ni changamoto kwa waamini kuwa na ari na moyo mkuu katika maisha. Je, inawezekanaje, umati mkubwa wa watu waliiona ile nyota lakini wakashindwa kuifuata? Mamajusi walipoiona nyota ya Mtoto Yesu mashariki, waliendelea kuifuata kwani hii ni nyota angavu inayowaalika watu na wala haipofushi macho wala kumpotosha mtu. Kadhalika akiendelea kuelezea juu ya nyota ambayo ni Kristo mwenyewe alisema, kumfuasa Kristo Yesu hakuna protokali inayotakiwa kufuatwa, bali ni hija ambayo inapaswa kujikita kila siku katika uhalisia wa maisha ya watu. Mungu aliwakomboa watu wake kutoka utumwani, akawataka kufuata nyota, inayowapatia uhuru na furaha kuu na hivyo kuondokana na woga ulikuwa umeawagandamiza, uvivu na kudhani kwamba, tayari mtu amefika mwisho wa safari yake. Kuna haja ya kuthubutu ili kukutana na Mtoto Yesu, ili kuonja huruma na upendo wake. mambo ambayo yanapaswa kushuhudiwa katika maisha ya waamini, alisisitiza Papa.

Misa ya Epifania ya Bwana tarehe 6 Januari 2017

Baba Mtakatifu Francisko alielezea tamanio la ndani ya moyo la kuhitaji Mungu kwamba ni tabia ambayo inavunja uvivu na ukawaida ili kuweza kutoka nje  binafsi ya ubinafsi wetu. Mamajusi ni kama picha ya waamini, wanaongaza sura ya watu wote ambao katika maisha yao, hawabaki wamegandisha mioyo yao, bali wanafungua na kugundua mtazamo wa Mfalme asiyejulikana, lakini anayetamaniwa, hasiyenyenyekesha na wala  kukufanya uwe mtumwa au kufungwa.  Ni kutambua mtazamo wa Mungu anayekuamsha anayekusamehe  anayekuponyesha. Kugundua Mungu ambaye amependelea kuzaliwa mahali ambapo hapakuwa panatarajiwa, mahali ambapo labda sisi hatupendi na wakati mwingine hata kupakataa kabisa. Kugundua mtazamo wa Mungu ya kuwa  kuna nafasi ya majeruhi wote, ya wenye kuelemewa, wenye kusongwa na kuteseka, wenye kuacha pembezoni, kwa nguvu na uwezo uitwao huruma.

Misa ya Epifania ya Bwana tarehe 6 Januari 2016

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Misa ya Epifania ya Bwana tarehe 6 Januari 2016 alisema, Mamajusi walipoona nyota walihisi furaha kubwa ( Mt 2,10). Hata sisi ni faraja kubwa kuona nyota au kuhisi tunaongozwa na siyo kuachwa pekee katika hatima yetu. Nyota ni Injili na Neno la Bwana kama zaburi isemavyo “ Neno lako ni taa ya miguu yangu na mwanga wa safari yangu ( Zab119, 105) Mwanga huo unatuongzwa kuelekea kwake Yesu Kristo. Bila kusikiliza Injili, siyo rahisi kukutana naye. Mamajusi kwa dhati katika kufuata nyota hiyo iliweza kuwaongoza hadi mahali ambapo alikuwa amezaliwa Yesu. Waliomwana Mtoto na Mama yake, wakamwabudu  na kumsujudu ( Mt 2,11). Uzoefu wa Mamajusi, unatuhimiza tusiridhike na unafiki na kujizeesha, badala yake ni kuendelea kutafuta maana ya mambo na kuyatafakari kwa shauku ya fumbo kuu la maisha. Ni mfano wa kutufundisha ili tuache kudharau udogo na umasikini, badala yake ni kuutambua katika unyenyekevu wa Mkuu huyo na kutambua kupiga magoti mbele yake na kusujudu! Bikira Maria aliyewapokea Mamajusi huko Bethlehemu, atusaidie kuamsha kwa shauku kubwa  mtazamo wa uso wetu katika maisha yetu binafsi na kuacha tuongozwe na nyota ya Injili ili kuweza  kukutana na Yesu na kutambua kuinama kwa ajili ya kuabudu. Na kwa kufanya hivyo tutaweza kupeleka mishale ya mwanga wake kwa wengine na kuwashirikisha furaha hiyo ya safari.

Misa ya Epifania ya Bwana tarehe 6 Januari 2015

Katika tafakari ya Baba Mtakatifu Francisko kwenye sherehe za Tokeo la Bwana mwaka 2015  alisema, katika safari ya mamajusi walikutana na matatizo mengi, kwani wao walikwenda moja kwa moja katika jumba la kifalme kwa maana walifikiri kwamba kama mfalme mpya atakuwa katika Jumba la kifalme. Lakini kwa kufanya hivyo wao walipoteza nyota. Je ni mara ngapi inatokea kupoteza nyota katika mtazamo. Pia walikutana na kishawishi, kilichowekwa na shetani, kwa maana ya ulaghai wa Herode. Yeye alijionesha mkarimu na mpole wa kutaka kumwona  mtoto na kumbe si kwa ajili ya kumwabudu bali kumteketeza kabisa. Katika jumba la kifalme la Herode, kwa hakika Mamajusi walikumbana na kipindi cha giza nene na cha upweke, lakini wakashinda kwa njia ya ushauri wa Roho Mtakatifu ambaye alizungumza kwa njia ya unabii wa Maandiko Matakatifu. Na maandiko hayo ni kwamba Masiha atazaliwa huko Bethlehemu katika mji wa Daudi. Kwa kuongozwa na Roho Mtakatifu waliweza kutambua mantiki ya Mungu ya kwamba ni tofauti na ile ya mwanadamu; na kwamba Mungu hajioneshi katika nguvu za dunia hii, lakini anajionesha katika unyenyekevu wa upendo wake. Upendo wa Mungu ni mkuu, japokuwa upendo huo ni wa unyenyekevu wa kweli. Mamajusi mfano wa mtindo wa kweli  katika uongofu wa imani ya kweli kwa sababu waliamini zaidi wema wa Mungu ambaye hajioneshi wazi katika mwanga wa wenye mabavu na nguvu!

Epifania ya Bwana tarehe  6 Januari 2014

Katika Misa ya Sikukuu ya Epifania ya Bwana  tarehe 6 Januari 2014, Baba Mtakatifu anasema, katika siku hii tunakumbuka tokeo la Yesu kwa binadamu kupitia uso wa mtoto na tunahisi ukaribu na Mamajusi, ambao walikuwa ni wenye hekima na wasindikizaji katika njia. Mfano wao, unasaidia kuamsha mtazamo wetu juu ya nyota na kufuata kwa  shauku za mioyo yetu. Ni mwaliko wa kuacha kuambukiza na mshangao wa kile ambao ni chema  na cha kweli na ambacho Mungu anatoa kwa namna hii ya ajabu na daima kubwa!

Ni kupata fundisho hasa la kuacha kudanganywa na ujujuu kwa kile ambacho dunia inafikiria ni kikubwa, chenye hekima na nguvu. Ni kuwa na tahadhali ya kuhepuka na kusimamia ujuu juu wa  mambo hayo  badala yake, ni lazima kwenda zaidi ya giza nene, zaidi ya honi za nguvu, kwenda zaidi ya udunia huu, zaidi ya mitindo mipya ya kile ambacho dunia leo inaonesha na kutoa. Ni lazima kwenda huko Bethlehemu, mahali ambapo kuna nyumba rahisi katika sehemu ya pembezoni, mahali ambapo kuna mama na baba waliojazwa na upendo na Imani kuu, mahali ambapo jua limechomoza kutoka juu yaani la Mfalme wa ulimwengu! Kwa mfano wa mamajususi, kwa mfano wa mianga yetu midogo ni ndi hatua wazi ya kutafuta Mwanga na kulinda Imani hiyo.

SAFARI YA MAMAJUSI
07 January 2019, 12:06