Cerca

Vatican News
Tamasha la Muziki wa Noeli Vatican 2018: Walengwa: Wakimbizi na Wahamiaji kutoka Uganda na Iraq. Tamasha la Muziki wa Noeli Vatican 2018: Walengwa: Wakimbizi na Wahamiaji kutoka Uganda na Iraq.  (Vatican Media)

Tamasha la Muziki wa Noeli Vatican: Wakimbizi na Wahamiaji!

Tamasha la Muziki wa Noeli kwa Mwaka 2018 hapa mjini Vatican ni kuchangia miradi ya elimu kwa watoto wakimbizi na wahamiaji huko Iraq na Uganda. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, hata Kristo Yesu katika maisha yake, alikumbana na mkono katili wa Mfalme Herode, kiasi kwamba, Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, ikalazimika kukimbilia uhamishoni Misri.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Waamini wanajiandaa kuadhimisha Sherehe ya Noeli, yaani kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu, takribani miaka elfu mbili iliyopita. Hii ni sherehe inayopambwa kwa tamaduni na mapokeo ya watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia na kwa namna ya pekee, hata wasanii wanao mchango wao katika maadhimisho ya Tamasha la Muziki wa Noeli kwa Mwaka 2018 hapa mjini Vatican. Kila mwaka, Sherehe ya Noeli ni mpya kwa sababu inapyaisha imani, inafungua matumaini na kuwasha moto wa mapendo na kwa namna ya pekee mwaka huu, jicho la huruma na upendo wa Mungu linaelekezwa kwa wakimbizi na wahamiaji.

Hawa ni watu wanaokimbia vita, maafa na majanga asilia; ukosefu wa haki msingi pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi. Ni watu wanaotafuta: usalama, hifadhi na kwamba wanayo ndoto ya maisha bora zaidi kwa siku za usoni. Kristo Yesu, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, katika hali ya unyenyekevu mkubwa, aliamua kuja na kukaa kati ya watu wake katika mambo yote alikuwa sawa na binadamu, lakini hakutenda dhambi na badala yake, kwa fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wake, ameweza kuwakomboa watu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, kwa kuwashirikisha huruma na upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi, tarehe 14 Desemba 2018, kwa wasanii wanaoshiriki katika Tamasha la Muziki wa Noeli kwa Mwaka 2018 hapa mjini Vatican ili kuchangia miradi ya elimu kwa watoto wakimbizi na wahamiaji huko Iraq na Uganda. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, hata Kristo Yesu katika maisha yake, alikumbana na mkono katili wa Mfalme Herode, kiasi kwamba, Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, ikalazimika kukimbilia uhamishoni, huko Misri. Yesu anawakumbusha waamini kwamba, leo hii nusu ya wakimbizi na wahamiaji ni watoto wadogo, wanaoteseka kutokana na ukosefu wa haki jamii!

Kanisa kama Mama na Mwalimu anapenda kujibu changamoto zote hizi kwa huruma na upendo unaomwilishwa katika mshikamano, ukarimu na wema, kwa kutambua kwamba, kuna changamoto nyingi zinazopaswa kupatiwa ufumbuzi wa kudumu, kiasi cha kuwashirikisha watu katika medani mbali mbali za maisha, kielelezo cha umoja na udugu, ili kujenga na kudumisha mtandao wa upendo, ili kutoa elimu, malezi na majiundo ya kina kwa watoto wadogo, kama kielelezo cha upendo na mshikamano wa dhati!

Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, kutengeneza mtandao wa elimu maana yake ni kuwawezesha  watu kusimama tena, ili kuwaunga mkono wakimbizi na wahamiaji, kuenzi utu na heshima yao; wakiwa na nguvu pamoja na ujasiri wa kukabiliana na changamoto za maisha; huku wakitumia karama na uwezo wao wa kufikiri na kutenda. Mtandao wa elimu ni “nyundo makini” ya kuvunjilia mbali malango ya kambi za wakimbizi, ili kutoa fursa kwa watoto na vijana kuingia tena ndani ya jamii, ili kukutana na hatimaye, kuona mshikamano na ukarimu.

Baba Mtakatifu anawashukuru wasanii na wanamuzi wanaoshiriki katika tamasha hili kwa ajili ya kuchangia gharama za utume wa Shirika la Wadon Bosco kwa ajili ya watoto nchini Uganda pamoja na mradi wa Taasisi ya Kipapa ya "Scholas Occurentes" huko Iraq, kielelezo cha usambazaji wa ujumbe wa matumaini katika kipindi cha Noeli. Utume na maisha ya Kanisa yanajionesha hata kwa njia ya kipaji cha ubunifu na karama za wasanii, kwani kwa njia yao, ujumbe unaweza kupenya zaidi katika dhamiri ya watu wa nyakati zote. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewashukuru wasanii wote kwa kazi kubwa wanayofanya kwa ajili ya ustawi na mafao ya watu wa Mungu ili kuendeleza wema na huruma ya Mungu katika kipindi cha Noeli.

Papa: Tamasha Noeli

 

14 December 2018, 14:12