Cerca

Vatican News
Sherehe ya Bikira MKaria Mkingiwa Dhambi ya Asili, tarehe 8 Desemba 2018 Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, tarehe 8 Desemba 2018 

Sherehe B.M. Mkingiwa Dhambi ya Asili: Watawa Dar & Roma kuweka nadhiri za daima!

Papa Pio IX kunako mwaka 1854 akatangaza rasmi kwamba, Mwenyeheri kabisa Bikira Maria, tangu nukta ya kutungwa kwake mimba, kwa neema na upendeleo wa pekee wa Mwenyezi Mungu, kwa kutazamia mastahili ya Kristo Yesu, Mwokozi wa wanadamu wote, alikingiwa na kila doa la dhambi ya asili. Haya ni mafundisho tanzu ya Kanisa, kielelezo cha mng’ao wa utukufu wa Bikira Maria!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, hapo tarehe 8 Desemba 2018 anatarajiwa kwenda kwenye Uwanja wa Spagna, kutoa heshima zake kwa Sanamu ya Bikira Maria inayoheshimiwa sana na familia ya Mungu mjini Roma. Tukio hili litatanguliwa na Kikosi cha Zima moto kuweka shada la maua kwenye Sanamu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili kama walivyofanya tarehe 8 Desemba 1857 mnara huu ulipozinduliwa rasmi kwa heshima ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Tangu mwaka 1953, viongozi wakuu wa Kanisa wamekuwa wakienda kutoa heshima zao kwa Sanamu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili.

Bikira Maria alipata upendeleo wa pekee kutoka kwa Mwenyezi Mungu aliyemkirimia karama na neema nyingi ili aweze kuwa ni Mama wa Mwanaye Mpendwa Kristo Yesu. Karne kwa karne Mama Kanisa ametambua kwamba, Bikira Maria aliyejazwa neema na Mwenyezi Mungu, alikombolewa tangu mwanzo alipotungwa mimba! Papa Pio IX kunako mwaka 1854 akatangaza rasmi kwamba, Mwenyeheri kabisa Bikira Maria, tangu nukta ya kutungwa kwake mimba, kwa neema na upendeleo wa pekee wa Mwenyezi Mungu, kwa kutazamia mastahili ya Kristo Yesu, Mwokozi wa wanadamu wote, alikingiwa na kila doa la dhambi ya asili. Haya ni mafundisho tanzu ya Kanisa, kielelezo cha mng’ao wa utukufu wa Bikira Maria!

Waamini sehemu mbali mbali za dunia wamekuwa wakijiandaa kwa novena kama sehemu ya maandalizi ya maisha ya kiroho, ili kusherehekea Siku kuu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Habari kutoka Jimbo kuu la Dar es Salaam zinasema kwamba, Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, tarehe 6 Desemba 2018 anaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Shirika la Masista Wakarmeli Wamisionari wa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu. Katika Ibada hii ya Misa Takatifu inayoadhimishwa kwenye Parokia ya Mwenyeheri Isidori Bakanja, Boko, Jimbo Kuu la Dar Es Salaam, watawa watano wa Shirika hili wataweka nadhiri zao za daima!

Wakati huo huo, tarehe 8 Desemba 2018 kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Trastevere, Jimbo kuu la Roma, Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Taasisi ya Kipapa kwa ajili ya maisha anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu ambamo watawa watano kutoka Shirika la Masista wa Upendo wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Ivrea, wataweka nadhiri zao za daima.  Masista hawa ni: Elizabeth Donati Kingo, Sr. Leticia Cyprian Mjungu; Sr. Masline Adhiambo Bumbria, Sr. Stella Ezekiel Bilinje pamoja na Sr. Angela Jeremiah Jorrow. Masista hawa wanataka kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani, kwani wanayaweza mambo yote katika Yeye awatiaye nguvu!

Papa: Dhambi Asili
05 December 2018, 12:15