Tafuta

Papa Francisko: Ujumbe wa Siku ya 52 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2019: Siasa safi ni huduma ya amani" Papa Francisko: Ujumbe wa Siku ya 52 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2019: Siasa safi ni huduma ya amani" 

PAPA: UJUMBE WA SIKU YA KUOMBEA AMANI DUNIANI 2019

Baba Mtakatifu anakazia Injili ya amani kama sehemu ya utume wa Kanisa; Changamoto za siasa safi; Upendo na fadhila za kiutu kwa ajili ya siasa inayohudumia haki msingi na amani; vilema vya wanasiasa; umuhimu wa siasa safi inayowashirikisha vijana na kujengeana imani; pamoja na kukataa kishawishi cha vita na mbinu mkakati wa vitisho, kwa kuwekeza katika mradi mkubwa wa amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 52 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2019 sanjari na Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu inayoadhimishwa tarehe Mosi Januari, yanaongozwa na kauli mbiu “Siasa safi ni huduma ya amani”. Kwa muhtasari Baba Mtakatifu anakazia Injili ya amani kama sehemu ya utume wa Kanisa; Changamoto za siasa safi; Upendo na fadhila za kiutu kwa ajili ya siasa inayohudumia haki msingi na amani; vilema vya wanasiasa; umuhimu wa siasa safi inayowashirikisha vijana na kujengeana imani; anasema, kuna haja ya kukataa kishawishi cha vita na mbinu mkakati wa vitisho, kwa kuwekeza katika mradi mkubwa wa ujenzi wa amani.

Baba Mtakatifu anasema Kanisa linatumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya amani kwa watu wa Mataifa wanaoogelea katika dimbwi la vita, kinzani na mipasuko ya kila aina. Amani inapaswa kukita mizizi yake katika maisha ya mtu binafsi bila kubaguliwa, amani katika familia na jamii katika ujumla wake sanjari na kulinda pamoja na kutunza mazingira nyumba ya wote. Haya ndiyo matashi mema, ambayo Baba Mtakatifu anawatakia waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanapouanza mwaka mpya wa 2019.

Changamoto za siasa safi! Baba Mtakatifu anafafanua kwa kusema, amani ni sawa na matumaini yanayosongwa na changamoto pamoja na magumu yanayowaandama walimwengu, hasa kutokana na uchu wa mali, madaraka na utajiri wa haraka haraka na matokeo yake ni matumizi mabaya ya madaraka na uvunjwaji wa haki msingi za binadamu. Siasa safi ni nyenzo inayosaidia ujenzi wa huduma kwa binadamu, lakini ikitumiwa vibaya inaweza kuwa ni chombo cha dhuluma, mipasuko na hatimaye kusababisha madhara makubwa kwa jamii.

Siasa safi inafumbatwa katika unyenyekevu, kielelezo makini cha huduma katika ngazi mbali mbali za maisha ya binadamu. Lengo ni kukuza na kudumisha dhamana, utu, heshima na tunu msingi za maisha zinazoiwezesha jamii kutekeleza mafao ya wengi. Kumbe, utekelezaji makini wa siasa safi ni changamoto endelevu kwa viongozi wanaopewa dhamana ya kuongoza, kwani wanapaswa kuwalinda raia wao; kwa kushirikiana kikamilifu ili kuboresha maisha ya wananchi wao katika misingi ya haki, uhuru, utu na heshima ya binadamu na kwa njia hii, siasa safi inakuwa ni chombo cha upendo!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, upendo na fadhila za kiutu ziwe ni kwa ajili ya siasa safi inayohudumia haki msingi na amani, kila mtu akijitahidi kujikita katika mafao ya wengi, kama sehemu ya ujenzi wa mji wa Mungu hapa duniani, ili kuendeleza historia ya maisha ya familia ya binadamu. Haki na usawa; tabia ya kuheshimiana na kuthaminiana kama binadamu; ukweli, uwazi na uaminifu ni tunu msingi zinazoboresha siasa safi na kwamba, mwanasiasa bora ni yule anayetambua dhamana na wajibu wake kwa jamii; anayeaminika na kuthaminiwa na jamii; ni kiongozi anayejitaabisha kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; mwaminifu katika ahadi zake kwa wananchi waliomchagua, daima akijitahidi kujenga na kudumisha umoja na mshikamano, tayari kuchochea mageuzi katika maisha ya watu; kwa kuwasikiliza na kutenda kwa ujasiri!

Baba Mtakatifu anasema, hivi ni vigezo muhimu sana wakati wa kufanya chaguzi mbali mbali, ili kuhakikisha kwamba, haki, dhamana na wajibu vinatekelezwa kikamilifu. Siasa safi ni chombo cha huduma ya amani inayosimikwa katika kulinda na kutetea haki msingi za binadamu; kwa vizazi kuheshimiana na kuthaminiana. Vilema vya wanasiasa vinajionesha katika maisha ya hadhara, kwenye taasisi wanazohudumia pamoja na utunzaji bora wa mazingira; mambo yanayoweza kuwafanya watu kumwamini mwanasiasa, katika kupanga na kutekeleza sera na mikakati yake kama kielelezo cha demokrasia. Vinginevyo, wanasiasa wanaoelemewa na vilema vyao ni hatari sana katika kujenga na kukuza demokrasia jamii.

Ni watu ambao “wamepekenywa” kwa rushwa na ufisadi; watu wasioheshimu wala kujali utawala wa sheria; ni watu wenye uchu wa mali, madaraka na utajiri wa haraka haraka; ni wachochezi wa ubaguzi na hofu miongoni mwa jamii wala utunzaji bora wa mazingira kwao si kipaumbele, lakini matokeo yake ni wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani! Baba Mtakatifu anaendelea kuhimiza umuhimu wa kudumisha siasa safi inayowashirikisha vijana na kujengeana imani, kiasi kwamba, hata vijana wa kizazi kipya wanajisikia kuwa ni sehemu ya mchakato wa ujenzi wa jamii yao na kwamba, wanaweza kushirikisha karama na mapaji  waliokirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya mafao ya wengi. Hawa ni vijana ambao dhamana ya amani inapenyeza katika akili na nyoyo zao, tayari kujitosa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Siasa safi inayojikita katika ujenzi wa amani inatambua karama za watu na inaendeleza majadiliano na watu kuaminiana na kuthaminiana badala ya kuangaliana kwa “jicho la kengeza”. Hizi ni dalili za ubinafsi unaofumbatwa katika dhana ya utaifa usiokuwa na tija wala mashiko badala ya kukuza umoja na udugu, wao wanakuwa ni sumu ya kusambaratisha watu. Jamii inawahitaji wajenzi wa amani, watakaokuwa ni watangazaji, mashuhuda na vyombo vya wema, huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake ambaye anawatakia watoto wake furaha.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, kuna haja ya kukataa kishawishi cha vita na mbinu mkakati wa vitisho; mambo yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu. Matumizi ya nguvu ni kinyume cha kanuni maadili inayopania suluhu ya amani na utulivu. Kuna baadhi ya wanasiasa wanaotumia wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kuwa ni mbinu mkakati wa kujijenga kisiasa kwa kuwashutumu wakimbizi na wahamiaji kuwa ni sababu ya umaskini na majanga yanayowaandama watu wao. Ikumbukwe kwamba, amani ya kweli inafumbatwa katika utu, heshima na haki msingi za binadamu; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi bila kusahau utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Huu ni ushuhuda wa urithi wa utajiri wa kimaadili kizazi baada ya kizazi! Watoto wanaoishi katika maeneo ya vita, vurugu na kinzani wanapaswa kulindwa na haki zao msingi na utu wao kuheshimiwa na kamwe wasipelekwe mstari wa mbele kama chambo cha vita kwani wao ndio leo na kesho ya binadamu!

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha ujumbe wake wa Siku ya 52 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2019 kuitaka Jumuiya ya Kimataifa kuwekeza katika mradi mkubwa wa ujenzi wa amani duniani unaofumbatwa katika wajibu fungamani na unaokamilisha. Wakati huu, Jumuiya ya Kimataifa inapoadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 70 tangu Tamko la Haki Msingi za Binadamu lilipotolewa na Umoja wa Mataifa. Hapa changamoto ni kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu; utu na heshima yake; kwa kutambua haki na dhamana zao. Amani ni changamoto endelevu inayofumbatwa katika toba na wongofu wa ndani na kwamba, amani inabubujika kutoka katika sakafu ya moyo wa mwanadamu, inayowezesha mtu kukataa kishawishi cha kukosa uvumilivu na hivyo kutawaliwa na hasira.

Amani inadumishwa kwa kujenga mahusiano mema na jirani hata kwa kuthubutu kukutana naye na kumsikiliza. Amani inajengwa kwa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Siasa safi kama huduma ya amani ni tete sana, lakini inaweza kujifunza kutoka kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Malkia wa amani, ambaye katika utenzi wake “Magnificat” anatoa sifa kwa Mwenyezi Mungu ambaye ameutaza unyonge wa mjakazi wake, kwani tazama, tokea sasa vizazi vyote watamwita mbarikiwa. Amefanya nguvu kwa mkono wake; amewatawanya walio na kiburi katika mawazo ya mioyo yao. Amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi; na wanyonge amewakweza... ili kukumbuka rehema zake; kama alivyowaambia baba zetu, Ibrahimu na uzao wake hata milele!

Papa Francisko: Ujumbe Amani 2019
29 December 2018, 11:03