Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Wazazi na wauguzi wasaidieni watoto wanaosumbuliwa na saratani kupambana na hali yao! Papa Francisko: Wazazi na wauguzi wasaidieni watoto wanaosumbuliwa na saratani kupambana na hali yao!  (@VaticanMedia)

Papa Francisko: Wazazi na wauguzi wasaidieni watoto kupambana na hali yao!

Baba Mtakatifu Francisko anawataka wazazi, walezi na wauguzi wa watoto hawa kutekeleza dhamana na wajibu wao, ili waweze kukua na kusonga mbele licha ya changamoto wanazokutana nazo. Watenge muda wa kuwazungumza na kuwasikiliza watoto hawa ambao wanahitaji sana uwepo wao katika shida na mahangaiko yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 30 Novemba 2018 amekutana na watoto wagonjwa kutoka Hospitali ya Tiba ya Ugonjwa wa Saratani Wroclaw, Poland, ili kuwatia shime katika hija ya maisha na mapambano yao dhidi ya ugonjwa wa Saratani. Baba Mtakatifu anawataka watoto kuendelea na tiba ili hatimaye, waweze kupona au kuendelea kuishi kwa matumaini wakiwa na ugonjwa huo. Hii ni changamoto kubwa ambayo si rahisi sana kwa watoto kama hawa kuweza kuifikiria! Lakini, Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia watoto hawa kwamba, wanao marafiki, ndugu na jamaa wanaowasindikiza ili kusonga mbele kwa imani, matumaini na mapendo.

Katika maisha, kuna mambo ambayo pengine si rahisi kuweza kuyapatia ushindi, lakini kila mtu anaweza kushinda kivyake vyake anasema Baba Mtakatifu, bila kukata tamaa. Watambue kwamba, wanaye Malaika mlinzi, tangu pale wanapozaliwa hadi siku ile wanaporejea nyumbani kwa Baba mwenye huruma. Kumbe, watoto wajenge sanaa na utamaduni wa kuzungumza na Malaika wao walinzi, ili aweze kuwalinda katika hatari zote za roho na za mwili. Baba Mtakatifu anawataka wazazi, walezi na wauguzi wa watoto hawa kutekeleza dhamana na wajibu wao, ili waweze kukua na kusonga mbele licha ya changamoto wanazokutana nazo. Watenge muda wa kuzungumza na kuwasikiliza watoto hawa ambao wanahitaji sana uwepo wao katika shida na mahangaiko yao!

Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa Siku ya Wagonjwa kwa Mwaka 2018, anataka mchakato wa tiba na huduma kwa wagonjwa kuhakikisha kwamba, inazingatia kwanza kabisa utu, heshima na mahitaji msingi ya mgonjwa. Baba Mtakatifu anapembua kuhusu: wito wa Mama Kanisa wa huduma kwa wagonjwa na maskini; kumbu kumbu endelevu ya historia ya huduma kwa wagonjwa sanjari na nguvu ya uponyaji inayoonesha uhusiano uliopo kati ya utume wa uponyaji na mwamko wa imani kwa wagonjwa wanaokutana na Kristo Yesu, wakiomba huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Huduma ya uponyaji inayotekelezwa na Kristo Yesu kwa wagonjwa mbali mbali inahitaji jibu la imani thabiti kutoka kwa wahusika.

Baba Mtakatifu analitaka Kanisa kuhakikisha kwamba, linaendelea kupyaisha huduma kwa wagonjwa sanjari na kujikita katika uaminifu kwa amri iliyotolewa na Kristo Yesu mintarafu mng’ao wa mwanga wa utukufu wa Fumbo la Msalaba. Kwani hili ni fumbo la matumaini, huruma na upendo usiokuwa na kikomo. Ikumbukwe kwamba, fadhila ya upendo ni msingi wa maisha ya kila mfuasi wa Kristo na Jumuiya za Kikristo zinapaswa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya upendo wa Kristo kwa waja wake. Katika hija ya maisha yao hapa duniani, wafuasi wa Kristo watambue kwamba, wanasindikizwa, wanalindwa na kutunzwa na Bikira Maria, Mama wa Kanisa. Huyu, ndiye Mama ambaye upanga ulipenya moyoni mwake, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi.

Kristo Yesu katika maisha na utume wake, aliwapatia pia mitume na waandamizi wao nguvu ya uponyaji na kwamba, Kanisa linaendeleza huduma hii kwa huruma na mapendo na kwamba, inapaswa kupyaishwa na kumwilishwa kutoka katika familia, parokia hadi kufikia taasisi za huduma ya afya. Wagonjwa wa muda mrefu, walemavu na wazee wanapaswa kuangaliwa zaidi kwa jicho la upendo na kwamba, kuna haja pia ya kuwa na sera makini za huduma kwa wagonjwa. Wadau wa huduma ya afya watambue kwamba, wanashiriki katika maisha na utume wa Kanisa kwa wagonjwa, changamoto kwao ni kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kumwilisha tunu msingi za maisha ya Kikristo kama ushuhuda unaotajirisha huduma kwa wagonjwa.

Papa: Wagonjwa wa Saratani
01 December 2018, 15:39