Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anawataka waamini kuwa ni mashuhuda wa Injili ya Ujasiri. Papa Francisko anawataka waamini kuwa ni mashuhuda wa Injili ya Ujasiri.  (ANSA)

Papa Francisko awataka waamini kuwa mashuhuda wa Injili ya Ujasiri!

Baba Mtakatifu katika hotuba yake kwa waamini hawa amewataka kuwa ni mashuhuda wa Injili ya Ujasiri inayowawezesha kuwa kweli ni chemchemi ya furaha inayiobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, tayari kuimwilisha katika uhalisia wa maisha yao kwa njia ya upendo kwa jirani, hali ambayo inafutilia mbali simanzi moyoni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kumbu kumbu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 tangu alipofariki dunia Askofu Tonino Bello, (1935-1993) kiongozi wa watu, mhudumu wa Neno na Baba wa maskini, lilipambwa kwa uwepo na ushuhuda wa Baba Mtakatifu Francisko kwa kutembelea Puglia, Kusini mwa Italia, Mwezi Aprili, 2018. Kwa ari na moyo mkuu, familia ya Mungu kutoka katika majimbo ya Urgento-Santa Maria di Leuca pamoja na Jimbo la Molfetta-Ruvo-Giovinazzo-Terlizzi, tarehe Mosi Desemba, 2018, ilimtembelea Baba Mtakatifu mjini Vatican kama kielelezo cha shukrani kwake kwa kuwatembelea na kuwaimarisha katika imani, matumaini na mapendo!

Baba Mtakatifu katika hotuba yake kwa waamini hawa amewataka kuwa ni mashuhuda wa Injili ya Ujasiri inayowawezesha kuwa kweli ni chemchemi ya furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, tayari kuimwilisha katika uhalisia wa maisha yao kwa njia ya upendo kwa jirani, hali ambayo inafutilia mbali simanzi moyoni. Furaha ya Injili ni amana na utajiri wa Mungu kwa binadamu katika ulimwengu mamboleo ambao umesheheni vita, chuki na misigano ya kila aina. Licha ya matatizo na changamoto za maisha, lakini, waamini wanapaswa kuwa ni chemchemi ya furaha ya Injili, kwa kuona hata mambo mazuri yanayotendeka katika maisha.

Kwa waamini wanaompatia Mungu nafasi ya kwanza katika maisha yao, anawajalia kuwa na furaha, inayowawezesha hata wao kuwafariji na kuwasaidia jirani zao. Hii ndiyo maana halisi ya kipindi cha Majilio, kinachofungua Mwaka Mpya wa Liturujia ya Kanisa inayowaletea waamini upya wa maisha kutoka kwa Mwenyezi Mungu, asili ya faraja zote na ndiye anayezima kiu ya matamanio halali ya waja wake. Yote haya yanaweza kutekelezeka ikiwa kama waamini watamfungulia Mungu malango ya maisha yao, tayari kuwakirimia upya wa maisha kama walivyofanya Manabii katika Agano la Kale na kama alivyofanya Mtumishi wa Mungu Askofu Tonino Bello katika maisha na utume wake.

Hii ni fursa ya kumwachia Mungu kuwa ni dira na mwongozo wa maisha yao, kama alivyofanya hata Mtakatifu Yosefu, Mtu wa haki, kwa kuilinda na kuitunza Familia Takatifu. Mwenyezi Mungu awe ni chachu ya upyaisho wa maisha, ambao wanapaswa kuungojea kwa kutenda mema kwa jirani na kamwe wasikubali “kutumbukia kaburini”, kwa kukata tamaa katika maisha! Wakristo wanaitwa na kutumwa kuwa ni walinzi na mashuhuda wa furaha inayomngoja Mwenyezi Mungu, anayekuja kuwatembelea katika maisha na majumbani mwao na kwamba, anataka kujenga makao ya kudumu katika maisha yao, leo na hata daima! Vinginevyo, Mwenyezi Mungu ataendelea kubaki akibisha hodi mlangoni.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kipindi cha Majilio, iwe ni fursa ya upya wa faraja na furaha ya maisha, kwa kuendelea kumngojea Kristo Yesu atakapokuja mara ya pili, kuwahukumu wazima na wafu na wala Ufalme wake hautakuwa na mwisho. Mwenyezi Mungu anawangoja kwa hamu kubwa, ili waweze kumwendea tena kwa moyo wa toba na wongofu wa ndani, bila woga wala makunyanzi. Leo hii watu wengi wamemezwa na hofu pamoja na wasi wasi ya maisha; watu wanajiogopa na kuogopana; wanaogopa kupenda na kupendwa; watu wana wasi wasi wa kutopata fursa za ajira!

Lakini ikumbukwe kwamba, kwa hofu, wasi wasi na mashaka, ni vigumu sana kuweza kuleta mageuzi duniani, badala yake, waamini na watu wenye mapenzi mema wanapaswa kuwa kweli ni mashuhuda wa Injili ya Ujasiri, tayari kuinua vichwa vyao ili kumpokea Kristo Yesu anayekuja kuwakomboa. Waamini watambue kwamba, wao ni watoto wa Mungu na wala si watoto wa hofu na woga unaowafanya kujitafuta wao wenyewe na hatimaye, kutumbukia katika ubinafsi!

Baba Mtakatifu anasisitiza kwamba, Injili ya upendo iwasaidie waamini kuboresha maisha yao, kwa njia ya imani na matumaini; tayari kutweka hadi kwenye vilindi vya Injili, ili kuzaa matunda yatakayowawezesha kusimama kidete kwa ajili ya huduma kwa jirani zao kama alivyofanya Mtumishi wa Mungu Askofu Tonino Bello! Kusimama na kuondoka maana yake ni kubomolea mbali ubaya wa moyo, nafasi ya dhambi na maisha ya undumila kuwili yanayoendelea kuuzeesha ulimwengu! Hii ni hali inayofumbatwa katika huduma kwa jirani na kwa njia ya faraja, waamini “watafyekelea” mbali hofu, mashaka na wasi wasi walio nao! Imani yao kwa Kristo Mfufuka, iwe ni chemchemi ya matumaini na furaha kwa wengi!

Papa: Tonino Bello
03 December 2018, 08:58