Vatican News
Papa Francisko: Tamko la Haki Msingi za Binadamu: Utu, Ushirikiano wa Kimataifa na Dhamiri nyofu! Papa Francisko: Tamko la Haki Msingi za Binadamu: Utu, Ushirikiano wa Kimataifa na Dhamiri nyofu!  (ANSA)

Tamko la Haki Msingi za Binadamu! Utu, ushirikiano na maendeleo fungamani

Baba Mtakatifu anawaalika wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa haki msingi za binadamu na ushirikiano wa kimataifa. Maadhimisho ya kumbu kumbu ya Miaka 70 ya Tamko la Haki Msingi za Binadamu iwe ni fursa ya kuamsha dhamiri nyofu na kuendelea kujikita katika kulinda, kudumisha na kuendeleza utu na heshima ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kwa muda wa siku mbili kuanzia tarehe 10 -11 Desemba 2018, Baraza la Kipapa la Maendeleo Endelevu na Fungamani ya Binadamu kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian kilichoko mjini Roma, limekuwa likiendesha mkutano wa kimataifa unaoongozwa na kauli mbiu “Haki Msingi za Binadamu katika Ulimwengu Mamboleo: Mafanikio; Yaliyoachwa, Yaliyofutwa”.

Mkutano huu ni sehemu ya maadhimisho ya kumbu kumbu ya Miaka 70 ya Tamko la Haki Msingi za Binadamu, lililotiwa mkwaju na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 10 Desemba 1948, miaka sabini iliyopita, ambalo bado ni changamoto changamani kwa Jumuiya ya Kimataifa! Maadhimisho haya yanakwenda sanjari na Kumbu kumbu ya Miaka 25 ya Tamko la Vienna na Mpango Mkakati wa utekelezaji wa haki msingi za binadamu zinazofumbatwa katika misingi ya: Usawa, utu wa binadamu na maridhiano. Pamoja na mambo mengine Tamko la Vienna linakazia: ushirikiano wa kimataifa, maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu; elimu na majiundo makini kuhusu haki msingi za binadamu sanjari na ufuatiliaji wa utekelezaji wa haki msingi za binadamu.

Kardinali Peter  Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Maendeleo Endelevu na Fungamani ya Binadamu amesoma ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwenye mkutano huu kwa kukazia: utu na heshima ya binadamu: kiroho na kimwili na kwamba, kila raia anayo dhamana na wajibu mbele ya Jumuiya ya Kimataifa na kwamba, utu na heshima yake, vinapaswa kuendelezwa katika ukamilifu wake. Maadhimisho ya Miaka 70 ya Tamko la Haki Msingi za Binadamu ni fursa kwa Jumuiya ya Kimataifa kujizatiti zaidi katika kulinda, kutetea na kudumisha utu na usawa wa binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, kumekuwepo na uvunjifu mkubwa wa haki msingi za binadamu kiasi cha kuhatarisha uhai wa binadamu. Kuna watoto wanaotolewa mimba kabla ya kuzaliwa; kuna mamilioni ya watu wasiokuwa na elimu bora na makini inayoweza kuwasaidia kupambana na mazingira yao. Kuna watu wasiokuwa na makazi maalum wanaoteseka kwa baridi na utupu; kuna watu wanakufa kwa baa la njaa la utapiamlo wa kutisha; kutokana na ushindani usiokuwa na tija wala mashiko na matokeo yake kuna watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kwa kukosa fursa za ajira; au kulazimika kufanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuna wafungwa wanaotumikia adhabu zao katika mazingira tete dhidi ya utu na heshima yao kama binadamu; hata leo hii bado kuna watu wanateswa na kutoweka katika mazingira ya kutatanisha. Kuna watu wanaoendelea kunyanyaswa na kudhalilishwa; wanatengwa na kudhulumiwa kwa misingi ya udini, ukabila, rangi na utaifa. Watu wanateseka kutokana na madhara ya vita sehemu mbali mbali za dunia kutokana na kushamiri kwa biashara haramu ya silaha ambayo inaendelea kupandikiza mbegu ya kifo duniani kwa watu wasiokuwa na hatia!

Kutokana na uvunjifu mkubwa wa haki msingi za binadamu, hapa kila mtu anapaswa kutambua kwamba, anawajibika kuchangia kwa ujasiri, kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu zinazomwilishwa katika Matendo ya huruma: kiroho na kimwili; hasa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Haki na mshikamano ni dhamana  ya kimaadili ambayo Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema wanapaswa kuimwilisha katika maisha na utume wao; kwa kuendeleza wema na huruma, ili kuwapunguzia mateso na mahangaiko wale wote wanaokata tamaa ya maisha.

Baba Mtakatifu anawaalika wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa na kitaifa kuhakikisha kwamba, wanatoa kipaumbele cha kwanza kwa haki msingi za binadamu na ushirikiano wa kimataifa na hata pale, itakapowabidi kwenda kinyume cha mkondo wa bahari! Maadhimisho ya kumbu kumbu ya Miaka 70 ya Tamko la Haki Msingi za Binadamu iwe ni fursa ya kuamsha dhamiri nyofu na kuendelea kujikita katika kulinda, kudumisha na kuendeleza utu na heshima ya binadamu!

Papa: Haki Msingi za Binadamu
11 December 2018, 09:33