Tafuta

Mtakatifu Stefano: Shemasi na Shahidi ni mfano bora wa kujiaminisha kwa Mungu na msamaha wa kweli unaorutubishwa kwa sala! Mtakatifu Stefano: Shemasi na Shahidi ni mfano bora wa kujiaminisha kwa Mungu na msamaha wa kweli unaorutubishwa kwa sala! 

Mt. Stefano Shahidi ni mfano wa imani na msamaha wa kweli!

Mtakatifu Stefano, Shemasi ni Shahidi wa kwanza kumfuasa Kristo Yesu kwa njia ya mateso na kifo cha ajabu, kwa kupigwa mawe hadi kufa! Yesu alipokuwa kufani, alijiaminisha kwa Baba yake wa mbinguni pamoja na kuwasamehe watesi wake! Stefano Shahidi naye alipokuwa anakaribia kufa aliomba akisema, “Bwana Yesu pokea roho yangu”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Furaha ya Noeli bado inaendelea kusikika katika nyoyo za waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kwamba, Mtoto Yesu amezaliwa kwa ajili ya binadamu. Baada ya maadhimisho ya Sherehe ya Noeli, Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 26 Desemba, anaadhimisha Siku kuu ya kuzaliwa kwa Mtakatifu Stefano, Shemasi na Shahidi wa kwanza huko mbinguni, Siku kuu ambayo ina uhusiano wa pekee kabisa na Sherehe ya Noeli.

Huu ni mwanzo wa mateso na madhulumu ya Kanisa la Mwanzo na kwamba, Mtoto Yesu aliyezaliwa atawakomboa watu kwa njia ya Fumbo la Msalaba, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu! Mtoto Yesu, Neno wa Mungu aliyefanyika Mwili ambaye sasa amevikwa nguo za kitoto na kulazwa kwenye Pango la kulishia wanyama, baada ya mateso na kifo chake, atavikwa sanda na kuzikwa kaburini!

Hii ni tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican, Mama Kanisa anapoadhimisha Siku kuu ya Mtakatifu Stefano, Shemasi na Shahidi wa kwanza kumfuasa Kristo Yesu kwa njia ya mateso na kifo cha ajabu, kwa kupigwa mawe hadi kufa! Yesu alipokuwa kufani, alijiaminisha kwa Baba yake wa mbinguni pamoja na kuwasamehe watesi wake! Stefano Shahidi naye alipokuwa anakaribia kufa aliomba akisema, “Bwana Yesu pokea roho yangu”.

Sala hii ni sawa na ile sala ya Yesu alipokuwa kufani alisema, “Baba mikononi mwako naiweka roho yangu”. Huu ni mwaliko kwa waamini kupokea kwa imani na matumaini yale yote ambayo Mwenyezi Mungu anaweka mbele ya maisha yao: yawe mema au machungu ya maisha. Hii inatokana na ukweli kwamba, maisha ya mwanadamu yana pande mbili, yaani kuna upande wa furaha na upande mwingine umesheheni machungu. Lakini, kwa njia ya imani, mwamini anaweza kupokea magumu ya maisha kama sehemu ya changamoto ya kukua na kukomaa kwa imani sanjari na ujenzi wa mahusiano mapya na jirani zake. Huu ni mwaliko wa kujiaminisha mikononi mwa Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo kwa watoto wake!

Stefano Shemasi na Shahidi wakati wa kifo chake aliendelea kumuiga Kristo Yesu kwa kuwasamehe watesi wake, kama Kristo mwenyewe alivyofanya, mwaliko kwa waamini kujifunza kutoka kwa Kristo Yesu, kusamehe na kusahau, ingawa yataka moyo kweli kweli anakiri Baba Mtakatifu Francisko. Msamaha unapanua moyo, unachipua ushirikiano na mshikamano; unamkirimia mwamini amani na utulivu wa ndani. Stefano, Shahidi ni kielelezo na ushuhuda unaopaswa kufuatwa ili kukuza na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kifamilia; katika maeneo ya shule na kazi; katika parokia na maeneo mbali mbali ya shughuli za kitume na hata katika jumuiya, msamaha daima unapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, msamaha unarutubishwa kwa njia ya sala, kwa kumwangalia Kristo Yesu, kama ilivyokuwa kwa Stefano aliyekuwa amejazwa nguvu ya Roho Mtakatifu, kiasi cha kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu. Kwa njia ya sala akapata nguvu ya kuweza kukabiliana na kifodini. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kusali bila kuchoka, ili kumwomba Roho Mtakatifu awakirimie paji la nguvu linaloponya hofu na wasi wasi; udhaifu na hali ya kutojiamini, kiasi cha kuwajengea uwezo wa kusamehe. Kwa maombezi ya Bikira Maria na ya Mtakatifu Stefano Shemasi na Shahidi, waamini waendelee kujiaminisha kwa Mungu, hasa nyakati ngumu za majaribu pamoja na kuwawezesha kuwa kweli ni watu wanaoweza kusamehe!

Stefano Shahidi
26 December 2018, 15:52