Tafuta

Papa Francisko: Siku ya 52 ya Kuombea Amani Duniani 2019: Siasa safi ni huduma ya amani. Papa Francisko: Siku ya 52 ya Kuombea Amani Duniani 2019: Siasa safi ni huduma ya amani. 

Siku ya Kuombea Amani Duniani 2018: Siasa safi ni huduma ya amani

Baba Mtakatifu anakazia Injili ya amani; changamoto katika siasa safi; upendo na fadhila zinazoweza kudumisha siasa safi kwa ajili ya haki msingi za binadamu na amani duniani; maovu ya wanasiasa; siasa safi katika kudumisha ushiriki wa vijana pamoja na hali ya kuaminiana: umuhimu wa kukataa kishawishi cha vita na sera vitisho na umuhimu wa kudumisha amani duniani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe Mosi, Januari, Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu pia ana adhimisha Siku ya Kuombea Amani Duniani. Maadhimisho ya Siku ya 52 kwa Mwaka 2019 yanaongozwa na kauli mbiu “Siasa safi ni huduma ya amani”. Siasa safi ni msingi wa maendeleo endelevu na fungamani; demokrasia shirikishi na uongozi bora unaojikita katika hoja zenye mashiko na huduma kwa wananchi. Siasa safi inafumbatwa katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi yanayowashirikisha wadau mbali mbali mbali katika jamii; marika pamoja na tamaduni, daima wakijitahidi kujenga imani kati yao kama sehemu ya kukuza na kudumisha amani. 

Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson na Monsinyo Bruno Marie Duffè, Mwenyekiti na Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Maendeleo Endelevu na Fungamani ya Binadamu, Jumanne, tarehe 18 Desemba 2018 wamewasilisha ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa waandishi wa habari mjini Vatican. Katika ujumbe huu, Baba Mtakatifu anakazia Injili ya amani; changamoto katika siasa safi; upendo na fadhila zinazoweza kudumisha siasa safi kwa ajili ya haki msingi za binadamu na amani duniani; maovu ya wanasiasa; siasa safi katika kudumisha ushiriki wa vijana pamoja na hali ya kuaminiana: umuhimu wa kukataa kishawishi cha vita na sera vitisho na umuhimu wa kudumisha amani duniani!

Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson anasema, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kukunjua jamvi la mwaka 2019 kwa kuwatakia watu wote wenye mapenzi mema amani inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, hii ni sehemu ya Habari Njema ya Wokovu. Salam hii inawakumbusha walimwengu kwamba, Kristo Yesu ni zawadi ya amani ya Baba wa milele, inayotolewa pote pale ambapo Injili inatangazwa na kushuhudiwa. Amani ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomwajibisha mwanadamu, ili kweli waweze kuwa ni watoto wa amani. Amani ya kweli inapata chimbuko lake kutoka katika sakafu ya moyo wa mwanadamu. Lakini, wakati mwingine, moyo huu unasheheni maovu kama vile: rushwa na ufisadi; uvunjaji wa haki msingi za binadamu; vita katika mifumo mbali mbali; utumiaji mbaya wa madaraka na uongozi mbovu usiozingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi na matokeo yake ni: ukosefu wa fursa za ajira, huduma mbovu za kijamii katika sekta ya elimu, afya na makazi; njaa na ukosefu wa maji safi na salama; uhamiaji wa shuruti; sera za ubaguzi wa rangi; uchafuzi wa mazingira na matumizi mabaya ya rasilimali na utajiri wa nchi.

Kardinali Turkson anasema, huduma ya amani inaweza kukwama kutokana na vizingiti hivi, changamoto na mwaliko wa Baba Mtakatifu Francisko kwa wanasiasa  ni kuhakikisha kwamba, kweli wanajikita katika siasa safi kama huduma ya amani. Amani hii inapaswa kudumishwa katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu, ili kwamba, rasilimali na utajiri wa nchi viweze kutumika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, ili watu wengi zaidi waweze kupata furaha na utulivu. Siasa safi isaidie kuimarisha utawala wa sheria; sera na matumizi bora ya rasilimali za nchi; kwa kuwawezesha vijana kupata fursa za ajira, kwani hii ni changamoto pevu katika ulimwengu mamboleo!

Monsinyo Bruno Marie Duffè kwa upande wake anakaza kusema, amani ni dhamana na utume wa Kanisa, kwa ajili ya watu wanaoteseka kutoka na vita na matumizi mabaya ya madaraka. Hii ni amani inayojengwa kwa njia ya majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu; kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama watoto wa Mungu. Ili kutekeleza dhamana hii, kuna haja kwa wanasiasa kuendelea kujikita katika majadiliano na upatanisho, ili kuvunjilia mbali kuta za utengano, tayari kushirikiana na kushikamana.

Baba Mtakatifu anasema, siasa safi ni huduma kwa ajili ya wananchi; inayofumbatwa katika sanaa ya kusikiliza na kushirikisha karama na mapaji kwa ajili ya ujenzi wa jamii inayosimikwa katika misingi ya haki na usawa; maskini na akina “yakhe pangu pakavu tia mchuzi” wakipewa kipaumbele cha kwanza. Lakini, ikumbukwe kwamba, amani ni tete sana inapaswa kulindwa na kuhifadhiwa kama mboni ya jicho! Huduma ya amani inajengwa katika mahusiano na mafungamano ya kijamii; kwa njia ya ushirikiano na mshikamano wa jamii na jumuiya ya Kimataifa.

Monsinyo Bruno Marie Duffè anakaza kusema, amani ya kweli inalinda na kuheshimu haki msingi; utu na heshima ya binadamu kama unavyofafanuliwa kwenye Tamko la Haki Msingi za Binadamu. Hizi ni haki ya: uhai, elimu, afya, utamaduni, uhuru wa kujieleza na uhuru wa kidini. Mtakatifu Yohane XXIII katika Waraka wake wa Kitume “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani” uliochapishwa kunako mwaka 1963 anakazia: Ukweli, haki, upendo na uhuru na kwamba, haki na wajibu ni sawa na chanda na pete ili kujenga na kudumisha jamii inayofumbatwa katika msingi wa amani inayodumishwa katika upendo na msamaha.

Baba Mtakatifu anapenda kuwachangamotisha wanasiasa, kuhakikisha kwamba, wanaondokana na mizizi ya dhambi inayowatumbukiza watu wengi katika majanga na badala yake, wajikite katika ujenzi wa siasa safi na amani kwa kukataa kishawishi cha uchu wa mali na madaraka; unafsia wa haki msingi za binadamu; maamuzi mbele, ubaguzi wa rangi; hofu zisizokuwa na mvuto wala mashiko; sera potofu dhidi ya wakimbizi na wahamiaji; yote haya ni mambo ambayo yanasigana kimsingi na siasa safi kama huduma ya amani. Uwajibikaji na utunzaji wa amani unafumbatwa katika siasa safi kukita mizizi yake katika sakafu ya moyo wa mtu. Heri yao wanaojitaabisha katika ujenzi wa amani; amani jamii, amani katika utunzaji bora wa mazingira na amani katika dhamiri za watu!

Amani Duniani 2019
19 December 2018, 10:44