Papa Francisko: Sala ya Baba Yetu ni mfano wa: Kusali, Kuomba na Kushukuru! Papa Francisko: Sala ya Baba Yetu ni mfano wa: Kusali, Kuomba na Kushukuru! 

Sala ya Baba Yetu: Mfano wa kusali, kuomba na kushukuru!

Sala ya Baba Yetu inakita mizizi yake katika uhalisia wa maisha ya mwanadamu mintarafu mahitaji yake msingi yaani: chakula, kwani imani inafumbatwa katika uhalisia maisha ya mwanadamu na wala si marembo ya nje! Sala ya Baba Yetu inaanza katika maisha, ushuhuda wa watu wanaopambana na baa la njaa na masumbuko mbali mbali.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sala ya Bwana yaani “Baba Yesu” ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake. Hii ni sala inayofumbatwa katika moyo safi, imani thabiti na dumivu; pamoja na ujasiri wa kimwana. Huu ni mwaliko wa kukesha na kwa njia ya Kristo Yesu, maombi yao yataweza kupelekwa kwa Baba wa milele. Hii ni sala yenye matini mafupi ambayo yameendelezwa na Mwinjili Mathayo na kufikishwa maombi saba, alama ya utimilifu katika Maandiko  Matakatifu. Ni mwaliko wa Yesu kwa wafuasi wake kujenga uhusiano wa karibu na Mwenyezi Mungu, kwa kuvunjilia mbali woga na mashaka yasiyokuwa na mvuto wala mashiko, kwani daima Mwenyezi Mungu yuko kati na karibu na watu wake. Jambo la msingi ni kwa waamini kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu kwa kuwa na ujasiri wa kimwana!

Hayo yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano, tarehe 12 Desemba 2018 kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Paulo VI, ulioko mjini Vatican. Sala ya Baba Yetu inakita mizizi katika uhalisia wa maisha ya mwanadamu mintarafu mahitaji yake msingi yaani: chakula, kwani imani inafumbatwa katika maisha ya mwanadamu na wala si marembo ya nje! Sala ya Baba Yetu inaanza katika maisha, ushuhuda wa watu wanaopambana na baa la njaa na masumbuko mbali mbali; watu wanaojiuliza kwa nini? Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, sala ya kwanza kwa kila mwanadamu ni kile kilio cha mtoto mchanga mara tu anapozaliwa. Ni kilio endelevu cha njaa, kiu na furaha ya kweli katika maisha!

Kristo Yesu katika Sala ya Baba Yetu, anawaalika waja wake, kumkimbilia Mwenyezi Mungu kwa imani na matumaini thabiti kwa njia ya majadiliano yanayofumbatwa katika imani kama ilivyokuwa kwa Timayo, Bartimayo, yule mwombaji kipofu, aliyethubutu kupaaza sauti yake, kwa Kristo Yesu ili aweze kumhurumia na kupata kuona tena na kwa hakika Yesu akamsikiliza, akamhurumia na kumponya upofu wake kutokana na imani thabiti aliyokuwa nayo Timayo mwana wa Bartimayo. Hii ni sala ya kilio cha imani kinachofumbata kwa namna moja wokovu unaomwondolea mwamini hali ya kukata tamaa, kinyume kabisa na mtu asiye kuwa na imani kwani, atashindwa kuona njia na mwelekeo wa kujikwamua kutoka katika matatizo na changamoto zinazomwandama katika maisha!

Waamini wanahisi kutoka ndani mwao umuhimu wa kumtukuza Mwenyezi Mungu, kwa kutambua utukufu, ukuu na wema wake usiokuwa na mipaka. Ni kutokana na mang’amuzi haya, mwishoni, Wakristo wa Kanisa la Mwanzo wakaongeza maneno: “Kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu na utukufu hata milele. Hiki ni kielelezo cha ukweli wa nguvu ya sala inayotaka kuzima kiu ya mwamini anayemtafuta Mwenyezi Mungu katika maisha yake. Hiki ni kielelezo cha imani kwa Mwenyezi Mungu ambaye ni Baba wa milele. Ni mwema na mwenye nguvu. Sala ni kielelezo cha imani kwa mtoto wa Mungu anayejisikia mnyonge, mdhambi na mhitaji.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Sala kwa ajili ya kuomba ni jambo la kawaida katika maisha ya mwamini, kwani Mwenyezi Mungu ni Baba mwema na mwingi wa huruma na mapendo, anayewataka watoto wake kuzungumza naye katika uhuru kamili, bila kumezwa na woga, hofu na mashaka; wala kuzungusha zungusha maneno, bali kwenda moja kwa moja na kusema, Baba Yetu aliye mbinguni nimekosa! Ni katika mwelekeo huu, mwamini anaweza kumsimulia Mwenyezi Mungu undani wa maisha yake bila kumficha jambo lolote, hadi siku ile, atakapokuwa anakunja kilago cha maisha yake hapa duniani!

Mwenyezi Mungu anawafahamu na kuwapenda sana watoto wake anasema Baba Mtakatifu Francisko na wala hakuna haja ya kukariri Sala ya Baba Yetu, bali huu ni mfano wa namna ya kusali, kushukuru na kuomba mambo msingi katika maisha. Waamini wanapaswa kuwa na nia moja, furaha na amani ya ndani na wala wasijisumbue kwa neno lolote kama anavyokaza kusema Mtakatifu Paulo anapowaandikia Wafilipi, bali katika kila neno kwa kusali, kuomba na kushukuru, ili haja zao zijulikane na Mungu.

Papa: Baba Yetu
12 December 2018, 14:26