Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Utamaduni wa mshikamano na majitoleo ni chachu ya ujenzi wa utu na udugu! Papa Francisko: Utamaduni wa mshikamano na majitoleo ni chachu ya ujenzi wa utu na udugu!  (Vatican Media)

Papa: Utamaduni wa mshikamano ni chachu ya utu na udugu!

Utamaduni wa mshikamano na majitoleo ni chachu ya ujenzi wa jamii inayosimikwa katika udugu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu, kama kielelezo makini cha umwilishaji wa Amri ya Upendo kwa Mungu na jirani, kiini cha Injili ya huruma na mapendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kituo cha Mshikamano wa Huduma ya Kujitolea huko Sardegna, Kusini mwa Italia, maarufu kama “Sardegna Solidale”, kinaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwake, kielelezo cha Injili ya huduma na upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wafanyakazi wa Kituo hiki cha Mshikamano, Ijumaa, tarehe 30 Novemba 2018 walikutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko ambaye amewapongeza kwa dhati kabisa kwa kazi kubwa ambayo wameifanya  katika kipindi cha miaka 20 iliyopita na ile ambayo wataendelea kuifanya huko mbeleni, kwa wananchi wa Sardegna na kwa wale wanaotoka katika Nchi zinazoendelea duniani.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Kituo cha Mshikamano kimeguswa na matatizo pamoja na changamoto za umaskini huko Kusini mwa Italia pamoja na kupiga hatua kubwa ya kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha watu wanaotafuta usalama, hifadhi na maisha bora zaidi kwa kukimbia vita, dhuluma, nyanyaso na umaskini sehemu mbali mbali za dunia. Watu hawa wamebahatika kupata amani na fursa ya kazi. Hii ni huduma inayowashirikisha watu wengi na hivyo kufanikisha mchakato wa mafungamano ya kijamii na ushirikiano, unaoleta mvuto na kuacha chapa ya kudumu kwa watu wasiokuwa na fursa ya ajira.

Baba Mtakatifu anapenda kuwatia shime wafanyakazi wa Kituo cha Mshikamano wa Huduma ya Kujitolea Sardegna kuendeleza maelewano, umoja na mshikamano, ili kuimarisha utamaduni wa mshikamano; kwa kusikiliza na kujibu kilio na matamanio halali ya watu wa Mungu. Ili kutekeleza vyema dhamana na wajibu huu, wanapaswa kuendeleza pia mshikamano na serikali pamoja na taasisi za kiserikali na parokia, ambazo daima zimekuwa pembeni mwa wale wote wanaoteseka pamoja na kutumainia maisha bora zaidi!

Utamaduni wa mshikamano na majitoleo ni chachu ya ujenzi wa jamii inayosimikwa katika udugu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu, kama kielelezo makini cha umwilishaji wa Amri ya Upendo kwa Mungu na jirani, kiini cha Injili ya huruma na mapendo. Amri hii inawawajibisha kuwapenda jirani zao pamoja na kusaidia mchakato kwa taasisi za kiraia na kiserikali kuwatambua na kuwathamini watu kama hawa. Chachu ya Injili inawasaidia kumwilisha tunu hizi msingi katika uhalisia wa maisha na utume wao; kwa kujenga na kuimarisha mtandao wa upendo katika jamii, kwa kuipamba jamii na sura ya Ukristo wenye mvuto na mashiko mbele ya watu wa Mataifa!

Huduma ya kujitolea na mshikamano wa upendo, vinawawezesha watu kuwa huru, daima wakiwa tayari kusikiliza na kujibu kilio na matamanio halali ya jirani zao! Kwa njia hii, wanaweza hata kusimama kidete: kulinda na kutetea haki, Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; kwa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote; kwa kuwasaidia na kuwahudumia wagonjwa na maskini. Huu ni utume mwanana katika ulimwengu mamboleo kwani unasaidia kuamsha dhamira kuhusu umuhimu wa kusimama kidete kutetea mafao ya wengi; huduma kwa maskini na wanyonge katika jamii. Baba Mtakatifu anahitimisha hotuba yake kwa kusema, leo hii ulimwengu unawahitaji mashuhuda wa wema, huruma na mapendo ya dhati. Ulimwengu unawahitaji watu watakaojenga na kudumisha mshikamano kwa ajili ya huduma kwa jirani zao; mfano bora wa kuigwa kutoka Sardegna.

Papa: Sardegna

 

01 December 2018, 15:11