Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Nendeni Bethlehemu mkajifunze kujisadaka na kupenda! Papa Francisko: Nendeni Bethlehemu mkajifunze kujisadaka na kupenda!  (Vatican Media)

Papa Francisko: Nendeni Bethlehemu mkajifunze kupenda!

Bethelehemu ni mahali ambapo mwanadamu anapewa changamoto ya kubadili mwelekeo wa maisha, Mwana wa Mungu anazaliwa katika nyumba ya mkate, mahali pa kulishia wanyama, ili aweze kuwa ni sadaka ya maisha inayotolewa kwa ajili ya maisha ya uzima wa milele. Hapa ni mahali pa kupenda bila kujibakiza!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Bethlehemu maana yake ni nyumba ya mkate, mahali anapozaliwa Kristo Yesu mkombozi wa ulimwengu katika pango la kulishia wanyama, huko kwenye Mji wa Daudi ambako Mwenyezi Mungu anataka kukutana na waja wake pasi na hofu na kwamba, hata leo hii, waamini wanahimizwa kukesha katika huduma na upendo! Huu ni muhtasari wa mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 24 Desemba 2018 wakati wa Mkesha wa Sherehe ya Noeli kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amesema, Bethlehemu maana yake ni nyumba ya mkate, mahali ambapo Mwenyezi Mungu anataka kukutana na binadamu, ili kuwapatia chakula kitakachowashibisha pamoja na kukata kiu ya maisha ya kiroho. Tangu wakati wa Agano la Kale, Adamu na Hawa walipokula tunda walilokatazwa, ulafi ukaingia ulimwengu, kiasi kwamba, kuna watu wanaoteseka kwa baa la njaa duniani na wengine wanakula na kusaza. Bethelehemu ni mahali ambapo mwanadamu anapewa changamoto ya kubadili mwelekeo wa maisha, Mwana wa Mungu anazaliwa katika nyumba ya mkate, mahali pa kulishia wanyama, ili aweze kuwa ni sadaka ya maisha inayotolewa kwa ajili ya maisha ya uzima wa milele.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Kristo Yesu ndiye mkate wa uzima ulioshuka kutoka mbinguni, mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujisadaka na kushirikishana na wengine, kwani Mwenyezi Mungu amejifanya kuwa mdogo, ili aweze kuwa ni chakula cha uzima wa milele, chemchemi ya upendo inayofyekelea mbali tamaa, uchoyo na ulafi. Katika nyumba ya mkate, Yesu anamrejesha tena mwanadamu nyumbani kwa Mungu na jirani yake. Mbele ya Pango la kulishia wanyama hapa kuna bubujika upendo, wema na kiasi, mambo yanayopaswa kuhifadhiwa.

Kristo Yesu, kila siku katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu anawajalia waamini mkate wa mbinguni kwa ajili ya maisha ya uzima wa milele, huu ni mkate usioweza kuharibika hata kidogo! Kutoka Bethelehemu, Mwenyezi Mungu anaendelea kumtunza mwanadamu na kwa njia ya Kristo Yesu, anampatia chachu ya mageuzi ya maisha yanayofumbatwa katika upendo. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kupanda kwenda Bethlehemu, nyumba ya mkate, ili kukutana na Kristo Mkate wa uzima wa milele, lakini wanapaswa kujiuliza mambo msingi wanayohitaji katika maisha, waguswe na umaskini wa mtoto Yesu; uwepo mwanana wa Bikira Maria, Mtakatifu Yosefu na wachungaji waliojitaabisha kwenda kumwona Mtoto Yesu, kwani Kristo ni mkate wa wasafiri; unaomegwa na kutolewa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengine, changamoto katika kipindi hiki cha Noeli ni mwaliko wa kugawana chakula na wale wanaohitaji zaidi.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Bethlehemu ni mji wa Daudi aliyechaguliwa kuwaongoza watu wa Mungu na ni katika mji huu, wachungaji kutoka kondeni wanakuwa watu wa kwanza kumpokea na kumkaribisha Kristo Yesu. Wachungaji waliingiwa na hofu kuu lakini Malaika wa Bwana akawatokea na kuwaambia wasiogope! Kutokana na madhara ya dhambi ya asili, mwanadamu daima ameendelea kumwogopa Mwenyezi Mungu! Mjini Bethlehemu, Mwenyezi Mungu anataka kufyekelea mbali hofu, kwa kuonesha kwamba, Yeye ni Immanueli, yaani Mungu pamoja na watu wake. Msigope ni neno ambalo Mwenyezi Mungu anawaambia wachungaji ambao walikuwa ni watu wa kawaida sana, kielelezo cha mshikamano wa upendo na uwepo wa endelevu wa Mungu katika maisha ya waja wake, ili kuvunjilia mbali hofu na upweke hasi kwani anawapenda wote pasi na ubaguzi!

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kwenda kukutana na Mtoto Yesu ambaye amezaliwa mjini Bethlehemu kwa kukesha, licha ya matatizo na changamoto za maisha, ili aweze kuwapatia mwanga aangavu, kwa kujiaminisha na kujialichilia mikononi mwa Mungu bila kuchelewa kama walivyofanya wale wachungaji, tayari kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu. Waamini wanapaswa kukesha kwa matendo ya huruma, ili aweze kuwa tayari kujibu kwa uhakika, ikiwa kama kweli wanampenda Kristo kama Mtakatifu Petro alivyoulizwa na kwamba, kila jibu analotoa mtu ni muhimu sana!

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kwenda Bethlehemu kujifunza kushusha milima ya ubinafsi, tabia ya kumezwa na malimwengu pamoja na ulaji wa kupindukia. Waamini waende Bethlehemu, huko ndiko mahali palipohifadhiwa mkate wao wa maisha ya uzima wa milele; ili wao pia waweze kuwa ni mkate unaomegwa kwa ajili ya ulimwengu. Wajiaminishe kwa Kristo Mchungaji mwema, ili kuchota upendo kutoka kwake, hata wao waweze kupenda na kuwasaidia jirani zao katika shida na mahangaiko yao, ili hatimaye, katika kipindi hiki cha Noeli, waweze kusema, kwa hakika Bwana wajua kwamba, mimi ninakupenda!

Papa: Mkesha wa Noeli
25 December 2018, 16:49