Cerca

Vatican News
Papa Francisko: Jivikeni unyenyekevu kugundua ukweli wa maisha! Papa Francisko: Jivikeni unyenyekevu kugundua ukweli wa maisha!  (Vatican Media)

Papa Francisko: jivikeni unyenyekevu kufahamu ukweli wa maisha!

Jorge Mario Bergoglio alizaliwa tarehe 17 Desemba 1936 nchini Argentina. Akapewa Daraja Takatifu ya Upadri tarehe 13 Desemba 1969. Mwaka 1992 akateuliwa kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Buenos Aires, Argentina na kuwekwa wakfu tarehe 27 Mei 1992. Mwaka 2001, Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Kardinali na tarehe 13 Machi 2013 akachaguliwa kuwa Papa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili, tarehe 16 Desemba 2018 amekutana na watoto, wazazi, wauguzi na wahudumu wa Zahanati ya Santa Marta iliyoko mjini Vatican, ili kuwatakia heri na baraka kwa ajili ya maadhimisho ya Sherehe ya Noeli kwa mwaka 2018. Na familia ya Zahanati ya Santa Marta, ambayo inaundwa na zaidi ya watu 800, imetumia fursa hii kumtakia heri na baraka, amani, utulivu na afya njema, Baba Mtakatifu Francisko anapoadhimisha kumbu kumbu ya miaka 82 tangu kuzaliwa kwake, tarehe 17 Desemba 2018. Zahanati ya Santa Marta ilianzishwa kunako mwaka 1922 na Papa Pio XVI na iko jirani sana na Hosteli ya Mtakatifu Martha, ambayo kwa sasa ni makazi ya Baba Mtakatifu Francisko.

Katika hotuba yake ya shukrani kwa wale wote waliofika kumtakia heri na matashi mema, amesema, ikiwa kama Bikira Maria angekuwa anaishi hapa Roma, hapana shaka kwamba, angempeleka Mtoto Yesu kupata huduma kwenye Zahanati ya Santa Marta. Anakaza kusema, kuwahudumia watoto si jambo rahisi sana, lakini, watoto wanawafundisha mambo mengi watu wazima. Kwa upande wake, anasema, wamemfundisha kwamba, ili kufahamu ukweli wa maisha, mtu hana budi kujinyenyekesha kama mtu anavyofanya wakati wa kutoa busu kwa mtoto mdogo. Kutokana na kiburi pamoja na majivuno, inakuwa ni vigumu sana kulifahamu fumbo la maisha, kwa sababu kunakosekana fadhila ya unyenyekevu.

Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, wote waliokuwepo hapo, yaani: wataalam na wahudumu wa sekta ya afya; waandaaji wa tukio hili, wakleri na watawa, wamekuwa mstari wa mbele kutoa mambo mema kwa watoto wagonjwa, lakini wao, wanawafundisha jambo moja la msingi: Unyenyekevu katika maisha. Kwa njia ya fadhila ya unyenyekevu, wataweza kulifahamu fumbo la maisha ya mwanadamu na watu wanaowazunguka. Hili ni jambo linalowezekana kabisa, ikiwa kila mtu atajitahidi kujivika fadhila ya unyenyekevu katika maisha na huduma kwa watu wa Mungu. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewatakia wote, heri na baraka kwa Sherehe ya Noeli.

Itakumbukwa kwamba, Jorge Mario Bergoglio alizaliwa kunako tarehe 17 Desemba 1936 huko Flores, Bueno Aires, nchini Argentina. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi na Kitawa, akapewa Daraja Takatifu ya Upadri hapo tarehe 13 Desemba 1969. Mtakatifu Yohane Paulo II, kunako mwaka 1992 akamteuwa kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Buenos Aires, Argentina na kuwekwa wakfu tarehe 27 Mei 1992 na kuchagua maneno: Miserando atque eligendo” yaani “Akamwangalia kwa jicho la huruma na kumteua”. Kunako mwaka 2001, Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa na kumsimika kuwa Kardinali na tarehe 13 Machi 2013 akachaguliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro na kuamua kuchagua jina la Mtakatifu Francisko wa Assisi, ili kukazia mambo makuu matatu: Amani, Maskini na Mazingira.

Katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, Baba Mtakatifu Francisko, amekuwa ni mtetezi, chombo na mjumbe wa haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Ameendelea kujipambanua kama mtetezi wa maskini, wanyonge na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na hali mbali mbali za maisha yao, ili kulinda utu, heshima na haki zao msingi! Baba Mtakatifu Francisko amekuwa ni mtetezi mkuu wa mazingira nyumba ya wote, ili kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwani athari kubwa za mabadiliko ya nchi zinaendelea kuwatumbukiza watu wengi katika ombwe la umaskini wa hali na kipato pamoja na kusigina utu, heshima na haki zao msingi!

Ad multos annos!

Papa: Salam 82 Yrs.

 

17 December 2018, 10:44