Papa Francisko: Tamko la Haki Msingi za Binadamu: Miaka 70 Ujenzi wa amani ni chachu ya maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu! Papa Francisko: Tamko la Haki Msingi za Binadamu: Miaka 70 Ujenzi wa amani ni chachu ya maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu! 

Papa Francisko: Miaka 70 ya Tamko la Haki za Binadamu! Amani!

Tamko la haki msingi za binadamu: Mambo muhimu: Utu na heshima ya binadamu; uhai unaopaswa kulindwa na kuendelezwa, sanjari na kujikita katika mchakato wa maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu: kiroho na kimwili. Jumuiya ya Kimataifa kuheshimu haki msingi za binadamu dhidi ya kile kinachodaiwa kuwa ni “Haki Mpya” ambazo zinasigana na tamaduni za watu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tamko la Haki Msingi za Binadamu, lililotiwa mkwaju na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 10 Desemba 1948, miaka sabini iliyopita ni changamoto endelevu kwa Jumuiya ya Kimataifa kwa wakati huu. Kipaumbele cha kwanza kinapaswa kuwa ni utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; uhai unaopaswa kulindwa na kuendelezwa, sanjari na kujikita katika mchakato wa maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu: kiroho na kimwili. Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuheshimu haki msingi za binadamu dhidi ya kile kinachodaiwa kuwa ni “Haki Mpya” ambazo kimsingi zinasigana na tamaduni, mila na desturi za mataifa mengi.

Uhuru wa kweli hauna budi kudumishwa dhidi ya utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba na kifo laini; biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo; mambo yanayokwenda kinyume cha Injili ya uhai. Kumbe, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuhakikisha kwamba, watu wengi zaidi wanapata huduma ya afya na dawa muhimu katika mapambano dhidi ya magonjwa duniani. Ili kudumisha uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, kuna haja pia ya kujikita katika ujenzi wa amani kama chachu ya maendeleo endelevu ya binadamu.

Hivi karibuni, Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, amepongeza na kufurahia msimamo wa serikali ya Tanzania dhidi ya kauli ya baadhi ya mataifa ya Magharibi kutishia kusitisha misaada kwa Tanzania kwa kuwa nchi inapinga ushoga. Ametoa msimamo huo hivi karibuni katika maadhimisho ya Misa Takatifu ya Mavuno iliyofanyika kijimbo katika Viwanja vya Msimbazi Centre, vilivyopo Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Kardinali Pengo amesema kuwa yapo baaadhi ya mataifa yanayotishia kukata misaada kwa nchi zinazopinga ushoga na mahusiano ya watu wa jinsia moja hivyo Kardinali Pengo amesisitiza kuwa, ni heri kufa kwa njaa kuliko kupokea misaada yenye shinikizo la kufanya mambo machafu yaliyo kinyume na Mungu.

Kardinali Pengo asema kuwa, uchafu wa mahusiano ya watu wa jinsia moja ndio uliosababisha Sodoma na Gomora kuangamizwa na kwamba, mambo hayo ni kinyume na mpango wa Mungu katika uumbaji, hivyo hayawezi kukubalilika. “Tunaishukuru Serikali kwa msimamo wake kuhusu jambo hili, na sisi kama Watanzania hatuwezi kuyakubali mambo hayo yasiyompendeza Mungu; na kama ni kufa na njaa basi tufe na Mungu wetu,” amesema Kardinali. “Tunalolifanya tunasema kitu kimoja kwa Mungu kwamba, kama tutakufa kwa njaa tutakufa na wewe, kama wanataka tuwe na ndege zisizo na marubani katika mambo machafu, basi sisi tutabaki na wewe na si ndege wala magari ya kifahari, kwa sababu kumpuuza Mwenyezi Mungu ni kujipuuza wenyewe,” amesema Kardinali Pengo.

Ikumbukwe kuwa hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, alisema kamwe vitendo vya ushoga haviruhusiwi na kila kiungo kilichoumbwa na Mungu katika mwili wa mwanadamu kina kazi yake hivyo, Serikali ya Tanzania haitakubali vibadilishiwe matumizi. Waziri Lugola alitoa kauli bungeni Dodoma baada ya Mbunge wa Konde, Khatibu Saidi Haji, kutaka msimamo wa Serikali kuhusu vitendo vya ushoga. Akasema: “Serikali yetu kamwe haitaruhusu mwanadamu yeyote kubadili matumizi ya kiungo ambacho kimekusudiwa kwa ajili ya kutolea haja, kitumike katika matumizi mengine ambayo Mungu hakuyakusudia.” Kauli hiyo imeridhisha Maaskofu wa Kanisa Katoliki na Mwadhama Kardinali Pengo ambaye anakuwa Askofu wa pili kupinga ushoga hadharani huku Marehemu Askofu Evaristo Chengula aliyekuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Mbeya akiwa wa kwanza kupinga vitendo vya ushoga hadharani siku kadhaa kabla hajafikwa na mauti.

Pia katika Ibada ya Misa Takatifu ya kumwaga Marehemu Askofu Chengula iliyofanyika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Kurasini Dar es Salaam Novemba 29 mwaka huu kabla ya kusafirishwa kwenda Mbeya kwa maziko, Rais John Magufuli alimtaja Mhashamu Chengula kama mtu wa Mungu aliyesimamia kweli za Kiinjili!

Papa: Haki Msingi za Binadamu

 

 

08 December 2018, 16:18