Tafuta

Papa Francisko: Matumizi haramu ya dawa za kulevya ni janga kwa utu na heshima ya binadamu! Papa Francisko: Matumizi haramu ya dawa za kulevya ni janga kwa utu na heshima ya binadamu! 

Matumizi haramu ya dawa za kulevya ni janga kwa binadamu!

Matumizi haramu ya dawa za kulevya ni matokeo ya kukengeuka kwa jamii, ulaji wa kupindukia; tabia ya kutaka kujitosheleza; kunong’onyoka kwa kanuni maadili na tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu; utupu wa maisha katika mambo msingi pamoja na kuporomoka kwa mahusiano na mafungamano ya kijamii. Yote haya ni madonda wazi yanayowaandama walimwengu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Kipapa la Maendeleo Endelevu na Fungamani ya Binadamu kuanzia tarehe 29 Novemba hadi tarehe 1 Desemba 2018 limekuwa likiendesha Kongamano la Kimataifa lililokua linaongozwa na kauli mbiu “Matumizi haramu ya dawa za kulevya na madhara yake ni kikwazo kwa maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu”. Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 1 Desemba 2018 amekutana na kuzungumza na washiriki wa kongamano hili kwa kukazia tena: madhara ya matumizi haramu ya dawa za kulevya hasa katika ulimwengu wa kidigitali pamoja na dhamana ya Kanisa katika kusaidia mchakato wa kuwarejeshea tena waathirika utu na heshima yao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema, madhara ya matumizi haramu ya dawa za kulevya na utegemezi unaoendelea kujitokeza nyakati hizi, ni kikwazo kikuu cha maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu. Haya ni matokeo ya kukengeuka kwa jamii, ulaji wa kupindukia; tabia ya kutaka kujitosheleza; kumong’onyoka kwa kanuni maadili na tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu; utupu wa maisha katika mambo msingi pamoja na kuporomoka kwa mahusiano na mafungamano ya kijamii. Yote haya ni madonda wazi yanayowaandama walimwengu, kiasi cha waathirika kukosa uhuru wao kutokana na kuzamishwa katika janga hili ambalo limekuwa ni mwiba kwa utu na heshima ya binadamu!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, matumizi haramu ya dawa za kulevya yana madhara makubwa kwa afya, maisha na jamii katika ujumla wake, changamoto kwa watu wote wenye mapenzi mema kujifunga kibwebwe ili kupambana dhidi ya uzalishaji, uchakataji, usambazi na matumizi haramu ya dawa hizi sehemu mbali mbali za dunia. Ni dhamana pevu kwa serikali kuhakikisha kwamba, zinapambana kufa na kupona na biashara pamoja na matumizi haramu ya dawa za kulevya, kwa kuwashughulikia kisheria wale wote wanaoendelea kupandikiza kifo miongoni mwa vijana! Matumizi haramu ya dawa za kulevya kwa njia ya mitandao ni hatari inayoendelea kujionesha kila kukicha na kwamba, vijana ndio wanaotumbukizwa kwa urahisi katika janga hili, kiasi cha kupoteza maana ya maisha.

Kutokana na changamoto hizi, Mama Kanisa anapenda kujipambanua katika masuala haya, ili kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu, ili kwamba, binadamu na mahitaji yake msingi apewe kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya kiuchumi, kijamii na kitamaduni. Utu wa binadamu ndiyo msingi wa Injili ya huruma ya Mungu. Ni kutokana na msingi huu, wakristo wanapaswa kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji ili kusaidia mchakato wa kuzuia, kuganga na kuponya magonjwa yanayotokana na matumizi haramu ya dawa za kulevya. Katika ulimwengu wa utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine, Kanisa linataka kumweka binadamu kuwa ni kiini cha sera na mikakati yake ya shughuli za kichungaji.

Mama Kanisa ataendelea kushirikiana na kushikamana na wadau sehemu mbali mbali za dunia katika kuelimisha, kuzuia, kurekebisha na kuwaponya waathirika wa matumizi haramu ya dawa za kulevya, ili kuwarejeshea tena utu na heshima yao kama binadamu. Ushindi dhidi ya matumizi haramu ya dawa za kulevya unafumbatwa kwa namna ya pekee katika umoja na mshikamano kati ya taasisi, familia na sekta ya elimu katika ujumla wake. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, kongamano hili limeweza kuibua sera na mikakati ya kupambana na matumizi haramu ya dawa za kulevya na kwamba, anawatakia kila la kheri katika mchakato huu, ili kuwaondoa watu wanaelemewa na janga hili katika maisha yao, ili waweze kuona tena mwanga unaodumisha utu na heshima yao kama binadamu!

Papa: Dawa Haramu za Kulevya
01 December 2018, 16:24