Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 13 Desemba 2018 amepokea hati za utambulisho kutoka kwa Mabalozi kadhaa wanaowakilisha nchi zao mjini Vatican. Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 13 Desemba 2018 amepokea hati za utambulisho kutoka kwa Mabalozi kadhaa wanaowakilisha nchi zao mjini Vatican.  (Vatican Media)

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Mabalozi wapya mjini Vatican!

Baba Mtakatifu anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inasimama kidete kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu kwa kuondokana na vita isiyokuwa na mvuto wa mashiko kwa ustawi na maendeleo ya binadamu. Ni wakati wa kupambana na baa la umaskini duniani, ubaguzi na ukosefu wa usawa mambo yanayohatarisha ustawi na mafungamano ya kijamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 13 Desemba 2018 amepokea hati za utambulisho kutoka kwa Mabalozi wapya kumi wanaoziwakilisha nchi zao mjini Vatican na kuwaomba kuwafikishia salam na matashi mema wakuu wao wa nchi na kwamba, anawaombea wananchi wao. Mabalozi wapya ni: Balozi Akima PAUL LAMBERT kutoka Grenada, Balozi Francis René BLAIN kutoka Gambia; Balozi Basil Walter BARNETT kutoka Bahamas; Balozi Denis KNOBEL kutoka Uswiss.

Wengine ni: Balozi Eurico CORREIA MONTEIRO kutoka Cabo Verde; Balozi Sigríđur Ásdís SnÆvarr kutoka Iceland; Balozi Atageldi HALJANOV kutoka Turkmenistan; Balozi Frank ZAMMIT kutoka Malta; Balozi Nasser Bin Hamad Mubarak AL-KHALIFA kutoka Qatar pamoja na Balozi Paul TEESALU kutoka Estonia.  Baba Mtakatifu katika hotuba yake kwa Mabalozi hawa wapya amekumbushia umuhimu wa kulinda na kudumisha amani duniani kwa njia ya majadiliano yanayofumbatwa katika ukweli na uwazi, Jumuiya ya Kimataifa linapoadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 100 tangu kusitishwa kwa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia na huo ukawa ni mwanzo wa kuzaliwa kwa Umoja wa Mataifa.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Mabalozi wapya wataweza kutekeleza dhamana na wajibu wao, kwa kuhamasisha amani inayofumbatwa katika haki na upendo sanjari na kuhakikisha kwamba, wanatumia kila nyenzo zilizopo kwenye uwezo wao kudumisha amani duniani! Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha pia kumbu kumbu ya Miaka 70 ya Tamko la Haki Msingi za Binadamu, hati muhimu sana ambayo ni dira na mwongozo wa kuhakikisha kwamba kunakuwepo na amani duniani inayosimikwa katika maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu; mambo msingi yanayotegemeana na kukamilishana. Kwa njia ya haki msingi za binadamu, usawa, uhuru, haki na amani vitaweza kutawala ulimwenguni!

Baba Mtakatifu anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inasimama kidete kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu kwa kuondokana na vita isiyokuwa na mvuto wa mashiko kwa ustawi na maendeleo ya binadamu. Ni wakati wa kupambana na baa la umaskini duniani, ubaguzi na ukosefu wa usawa mambo yanayohatarisha ustawi na mafungamano ya kijamii. Viongozi wakumbuke kwamba, huu ni wajibu wao wa kimaadili katika kupambana na changamoto mamboleo ambazo zimepelekea kuibuka kwa wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ni muhimu na kwamba, ili kukabiliana na changamoto ya wakimbizi na wahamiaji Kanisa linapenda kukazia umuhimu wa kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji katika maisha ya jamii inayowakirimia. Kanisa litaendelea kushirikiana na kushikamana na wadau mbali mbali ili kuhakikisha kwamba, changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji inapatiwa ufumbuzi wa kudumu, sanjari na kuendeleza: maisha, utu, heshima na haki msingi za binadamu; kwa kujikita pia katika sera na mikakati ya maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu.

Papa: Mabalozi Wapya
13 December 2018, 14:43