Papa Francisko: MAJILIO: Kipindi cha kukazia mambo msingi katika maisha, tayari kukutana na Kristo Yesu kwa njia ya upendo kwa jirani! Papa Francisko: MAJILIO: Kipindi cha kukazia mambo msingi katika maisha, tayari kukutana na Kristo Yesu kwa njia ya upendo kwa jirani! 

MAJILIO: Ni mwongozo wa mambo msingi na upendo kwa jirani!

Kipindi cha Majilio ni muda muafaka ambamo Mama Kanisa anawaalika watoto wake kuambata mambo msingi katika maisha yao kwa kujitahidi kumwilisha imani yao katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama njia ya kukutana na Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai anayeendelea kujifunua kati ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Kipindi cha Majilio ni muhtasari wa historia ya ukombozi inayofumbatwa katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Ni kipindi cha kujiandaa kikamilifu kwa kukesha katika sala, tafakari ya Neno la Mungu, Maisha ya Kisakramenti na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama njia muafaka ya kukutana na Kristo Yesu atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu na wala ufalme wake hautakuwa na mwisho! Kwa ufupi, Majilio ni kipindi cha kumbu kumbu, imani na matumaini ya uwepo na ujio wa Kristo katika historia ya maisha ya mwanadamu.

Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari zake mintarafu Kipindi cha Majilio anasema, huu ni muda muafaka ambamo Mama Kanisa anawaalika watoto wake kuambata mambo msingi katika maisha yao kwa kujitahidi kumwilisha imani yao katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama njia ya kukutana na Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai anayeendelea kujifunua kati ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Huu ni muda muafaka kwa waamini kujifunza kupendwa na Mungu na kurudisha upendo huu kwa jirani zao. Maandalizi makini ya Kipindi cha Majilio yawasaidie waamini kuzima kiu ya uwepo wa Mungu katika maisha yao.

Kipindi cha Majilio ni kumbu kumbu endelevu ya Fumbo la Umwilisho, pale Neno wa Mungu alipotwaa mwili kwake Bikira Maria na kukaa kati ya watu wake, akawa sawa nao katika mambo yote isipokuwa hakutenda dhambi. Sherehe ya Noeli ni kumbu kumbu ya unyenyekevu wa Mwana wa Mungu aliyefanyika mwili! Lakini, kila mara Kristo Yesu anawatembelea waja wake, ikiwa kama wako tayari kumfungulia malango ya maisha yao! Anawatembelea kwa njia ya Neno, Sakramenti za Kanisa na kwa njia ya Matendo ya huruma!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Mwisho wa nyakati, Yesu atakuja tena kuwahukumu wazima na wafu, jambo la msingi kwa waamini ni kuhakikisha kwamba, kipindi chote hiki cha maandalizi ya ujio wa Kristo kinatumika vyema, kwa ajili ya kujiwekea hazina mbinguni kwa njia ya matendo mema! Hukumu ya Mwisho itatolewa mintarafu Amri ya Upendo kwa jirani! Waamini wajitahidi kukesha kwa kumwilisha Amri ya Upendo kwa jirani zao, kwa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini wa nyakati hizi. Waamini watambue kwamba, wao wako duniani, lakini wakumbuke pia kwamba, wao si wa ulimwengu huu! Kumbe, wanapaswa kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya ujio wa pili wa Kristo.

Baba Mtakatifu anakazia dhana ya kukesha katika maisha ya Kikristo kama kielelezo makini cha Kipindi cha Majilio, kwa kuwa waaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; kwa kuambata na kumwilisha Heri za Mlimani kama chemchemi ya utakatifu wa maisha. Kipindi cha Majilio ni wakati wa muafaka wa kuendelea kupyaisha imani kwa Kristo na Kanisa lake; kwa kuendeleza mapambano ya imani; kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa uwepo, ukuu na utakatifu wa Mungu. Ni muda wa kutangaza na kushuhudia Injili ya haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati kama sehemu ya mchakato wa kukutana na Mwenyezi Mungu anayewaendea watu wake. Matukio yote haya anasema Baba Mtakatifu Francisko yawasaidie waamini kusoma alama za nyakati, tayari kumlaki Kristo Yesu atakapokuka siku ile ya mwisho, kuwahukumu wazima na wafu!

Papa: Majilio 2019

 

01 December 2018, 14:44