Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anawataka vijana wa Taizè kujenga umoja, udugu na mshikamano wa kweli! Papa Francisko anawataka vijana wa Taizè kujenga umoja, udugu na mshikamano wa kweli!  (AFP or licensors)

Papa Francisko: Vijana jengeni umoja, udugu na mshikamano!

Papa Francisko anawataka vijana kuhakikisha kwamba, wanatumia vyema karama na mapaji yao kama sehemu ya mchakato wa maboresho ya maisha, ili ulimwengu uweze kuwa ni mahali bora zaidi pa kuishi. Utamaduni wa ukarimu, uwawezeshe vijana kumfungulia Kristo Yesu, malango ya maisha yao, ili kuweza kusikiliza Neno lake na kulimwilisha katika uhalisia wa maisha yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Vijana wa Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè kutoka sehemu mbali mbali za Bara la Ulaya, wametinga timu mjini Madrid, Hispania kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya 41 ya Vijana wa Kiekumene kwa Mwaka 2018 yanayoongozwa na kauli mbiu “Kamwe hatuwezi kusahau ukarimu”. Viongozi wakuu wa Makanisa na Jumuiya ya Kimataifa wamewatumia vijana hawa ujumbe wa kuwatia moyo, ili waendelee kudumu katika imani, matumaini na mapendo yanayofumbatwa katika mshikamano wa udugu wa kibinadamu, kwa kuheshimu na kuthamini utu na heshima yao kama binadamu!

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anawataka vijana kuhakikisha kwamba, wanatumia vyema karama na mapaji yao kama sehemu ya mchakato wa maboresho ya maisha, ili ulimwengu uweze kuwa ni mahali bora zaidi pa kuishi.  Utamaduni wa ukarimu, uwawezeshe vijana kumfungulia Kristo Yesu, malango ya maisha yao, ili kuweza kusikiliza Neno lake na kulimwilisha katika uhalisia wa maisha yao.

Baba Mtakatifu anawataka vijana kujenga na kudumisha utamaduni wa kukutana na kusaidiana; kwa kuheshimiana na kuthaminiana katika ukweli na uwazi hata katika tofauti zao msingi. Vijana wajitahidi kuwa ni mashuhuda na vyombo vya ukarimu kwa jirani zao. Anawakumbusha kwamba, hivi karibuni, Mama Kanisa ameadhimisha Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa mwaka 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito”. Baba Mtakatifu pamoja na Kanisa zima, lina imani na matumaini kwa vijana wa kizazi kipya.

Baba Mtakatifu anawataka vijana wa Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè kufanya tena rejea katika ujumbe wa Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2018 ili kupyaisha tena ari na mwamko wao katika maisha ya kiroho! Baba Mtakatifu anawahimiza vijana kufurahia zawadi ya maisha kwa kukutana na vijana wenzao kutoka sehemu mbali mbali za Bara la Ulaya. Iwe ni fursa ya kujenga na kuimarisha urafiki pamoja na kuendelea kuota ndoto na kutembea kwa pamoja kama ndugu. Ikumbukwe kwamba, Wakristo wa kweli, hawana hofu wala mashaka ya kujifunua kwa wengine, kushirikishana fursa mbali mbali wanazozigeuza kuwa ni nafasi ya ujenzi wa umoja na udugu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema kwamba, inawezekana kabisa kumwilisha utamaduni wa ukarimu; kwa kujifunza kutajirishana na wengine kutokana na tofauti zao msingi, kiasi cha kutumia vyema karama na mapaji waliokirimiwa na Mungu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Vijana wanaweza kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa ujenzi wa madaraja kati ya makanisa, dini na jamii ya watu. Mkutano huu wa kiekumene unawashirikisha vijana kutoka katika madhehebu ya Kikristo pamoja na dini mbali mbali.

Baba Mtakatifu anawaombea vijana hawa mwanga wa Roho Mtakatifu, ili waweze kupokea tofauti zao msingi kama kielelezo cha umoja na mshikamano unaowawezesha kutembea pamoja. Anawataka kutumia vyema karama na mapaji yao; nguvu na uweza kwa ajili ya kuboresha ulimwengu ili uweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Kila mtu aweze kupata nafasi katika tumbo la familia kubwa ya binadamu. Kwa mfano wa Bikira Maria, mwanga angavu na mfano bora wa kuigwa katika upendo kwa kujisadaka bila ya kujibakiza, hata vijana pia wawe na ari na moyo wa kuthubutu kujisadaka kwa ajili ya jirani zao. Mkutano wa vijana umezinduliwa tarehe 28 Desemba, 2018 na utafungwa rasmi hapo tarehe Mosi, Januari 2019.

Papa Taizè

 

 

28 December 2018, 09:02