Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anawataka wanandoa kutangaza na kushuhudia Injili ya familia kwa watu wa Mataiafa! Papa Francisko anawataka wanandoa kutangaza na kushuhudia Injili ya familia kwa watu wa Mataiafa!  (Vatican Media)

Papa Francisko: Tangazeni na kushuhudia Injili ya familia!

Baba Mtakatifu anawataka wanafamilia kulinda, kutetea na kushuhudia tunu msingi za ndoa na familia kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Wanandoa wawe na ujasiri wa kuangaliana usoni ili kuoneshana ule upendo wa awali kabisa uliowavuta kiasi hata cha kuamua kufunga ndoa! Yaani hadi raha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wazazi washirikishwe kikamilifu katika masuala ya elimu kwa watoto wao. Wasisite kusimama kidete, kuragibisha familia nchini Italia kuongeza idadi ya watoto, pamoja na kuhakikisha kwamba, wanasaidia kuhamasisha taasisi mbali mbali kutambua na kuthamini watoto wanaozaliwa kuwa ni zawadi kubwa kutoka kwa Mungu. Watoto ni kitega uchumi kikuu. Lakini kwa bahati mbaya, watoto hawa wanaonekana kuwa ni sababu ya umaskini wa familia, kiasi hata cha kugeuziwa kisogo na taasisi mbali mbali.

Matatizo na changamoto zote hizi zinapaswa kukabiliwa kwa ari, moyo mkuu na upendo, kwa kutangaza na kushuhudia tunu msingi za familia zinazofumbatwa katika utu na heshima ya binadamu! Familia ni amana na utajiri mkubwa wa kisiasa, kiuchumi na kijamii. Kumbe, Jukwaa la Vyama vya Kifamilia linapaswa kujielekeza zaidi na zaidi katika huduma kwa familia, kwa kusimama kidete kulinda Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi, tarehe 16 Juni 2018 alipokutana na kuzungumza na wanachama wa Jukwaa la Vyama vya Kifamilia nchini Italia, linalounganisha vyama vya kifamilia vipatavyo 500 kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 ya uwepo na utume wao katika kutangaza na kushuhudia Injili ya familia. Baba Mtakatifu anawataka wanafamilia kulinda, kutetea na kushuhudia tunu msingi za ndoa na familia kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Wanandoa wawe na ujasiri wa kuangaliana usoni ili kuoneshana ule upendo wa awali kabisa uliowavuta kiasi hata cha kuamua kufunga ndoa! Yaani hadi raha!

Wanandoa wajenge utamaduni wa kusikilizana, kujadiliana, kukumbushana na kusameheana pale mambo yanaypokwenda mrama! Kwa njia hii, wataweza kuadhimisha Jubilei ya Miaka 25, 50 na wenye bahati miaka 70 ya Ndoa kwa wale waliobahatika kuoana wakiwa vijana wabichi! Baba Mtakatifu anaendelea kudadavua kwa kusema, upendo wa dhati kati ya wanandoa wakati mwingine unapitia majaribu makubwa, jambo la msingi ni kujenga na kudumisha utamaduni wa kuvumiliana na kuridhiana, vinginevyo, wanandoa watachokana na huo ndio mwanzo wa kusambaratika kwa ndoa nyingi.

Baba Mtakatifu anawakumbusha wanandoa wapya kwamba, kukosa na kukoseana ni ubinadamu, kusamehe na kusahau ni mwanzo wa hija ya utakatifu wa maisha. Wanandoa wahakikishe kwamba, wanahitimisha siku kwa amani, utulivu na uhuru wa ndani; kwa kusamehe na kusahau! Kinyongo ni hatari sana kwani matokeo yake ni hasira, chuki na kutaka kulipiza kisasi. Maisha ya familia ni sadaka safi inayompendeza Mwenyezi Mungu. Upendo wa dhati ni changamoto kubwa sana kwa wanandoa hasa katika ulimwengu mamboleo.

Upendo katika ndoa kadiri ya mpango wa Mungu ni kati ya mwanaume na mwanamke, wanaopewa dhamana ya kushiriki katika kazi ya uumbaji, malezi na makuzi ya watoto wao ambao kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Mwanaume na mwanamke, wasaidiane, wakamilishane na kutakatifuzana kama sehemu ya hija ya maisha ya ndoa na familia. Uvumilivu na saburi ni muhimu sana kwa wanandoa kuweza kupita na hatimaye kuvuka mikimiki ya maisha ya ndoa na familia. Bila uvumilivu, huo unakuwa ni mwanzo wa “michepuko” isiyokuwa na tija wala mashiko; ni mwanzo wa kuambukizana magonjwa. Uvumilivu mtakatifu unafumbatwa katika subira; ni utakatifu unaothubutu kusamehe na kusahau kwa sababu kuna upendo wa dhati unaopaliliwa ili uendelee kushamiri.

Wanandoa wajifunze busara na hekima ya kukaripia au kujibu mashambulizi! Inapoonekana kwamba, inafaa, wajifunze kukaa kimya ili kuvusha shari, wajadiliane katika ukweli na uwazi, mambo yanapokuwa yametulia tuli kama maji mtunguni! Baba Mtakatifu Francisko anawaonya wanandoa “kupandishiana mashetani” kuwa ni hatari sana kwa ustawi, maendeleo na mafao ya familia zao. Wanandoa wajifunze kuomba ridhaa kama kielelezo cha kuheshimiana! Wawe na ujasiri wa kuomba msamaha pale wanapogundua kwamba, wameteleza na kuanguka katika udhaifu wao wa kibinadamu. Hii inatokana na ukweli kwamba, daima binadamu anaogelea katika dhambi, kumbe, daima anapaswa kulitambua hili na kuwa mwepesi kutubu na kumwongokea Mungu pamoja na kujipatanisha na mwenza wake wa ndoa.

Baba Mtakatifu Francisko anasema SURA YA NNE: Upendo ndani ya ndoa ndicho kiini cha Wosia wake wa Kitume “Amoris laetitia”. Anaianza sura ya nne kwa utenzi wa upendo kati ya ndugu kama anavyoutafakari Mtakatifu Paulo mtume, katika Waraka wake wa kwanza kwa Wakorintho 13: 4-7 na kuuweka katika mazingira ya familia: Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari, haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; haoni uchungu, hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote, huamini yote. Baba Mtakatifu anasema huu ndio urafiki unaojengwa katika upendo wa dhati; unathamini na kujali utajiri wa mwingine pamoja na kuwa na jicho pana zaidi kwani ndoa ni mchakato unaomwilisha zawadi za Mungu kwa binadamu!

Baba Mtakatifu anawahamasisha vijana kuchangamkia maisha ya ndoa na familia na wala wasione kuwa ni mzigo usioweza kubebeka bali safari ya maisha inayowaelekeza kwenye ukomavu, kwa kupokea kwa ukweli na busara mapungufu yao ya kibinadamu na changamoto zilizoko mbele yao. Vijana wanapaswa kujikita katika majadiliano ili kushuhudia, kuishi na kukomaa katika upendo. Watambue kwamba, wanatofautiana na kwamba, tofauti zao ni sehemu ya utajiri wao! Upendo wao ni chachu muhimu sana katika maisha ya ndoa na familia na huduma kwa maisha ya pamoja.

Hapa kuna haja kwa vijana kupata malezi makini kuhusu vionjo vya kimwili, ili kuwa na mwelekeo sahihi na mpana zaidi. Upendo ni zawadi ya ajabu inayofumbata utakatifu na tunu msingi za maisha! Vijana wawe na mwelekeo sahihi wa tendo la ndoa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia. Vijana waheshimu na kuthamini tendo la ndoa. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hata ubikira ni kielelezo cha upendo na kwamba, ndoa na ubikira ni mielekeo miwili tofauti ya upendo. Wanandoa wanaendelea kuhamasishwa na Kanisa kuhakikisha kwamba, wanaboresha mahusiano ya upendo wao kila siku kwa msaada wa Roho Mtakatifu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, katika Wosia huu wa kitume, amebainisha matatizo, changamoto na fursa ambazo wanandoa wanaweza kukabiliana nazo katika safari ya maisha yao hapa duniani. Kumbe, maandalizi ya wanandoa watarajiwa ni muhimu sana, ili waweze kufahamiana, watambue dhamana na wajibu wao, changamoto na matatizo wanayoweza kukumbana nayo na wapi pa kukimbilia ili kupata msaada wanapokuwa katika mtikisiko wa maisha ya kiroho. Ndoa ya Kikristo ni dumifu, hadi pale kifo kitakapowatenganisha! Kumbe, maandalizi ya awali na endelevu ni muhimu sana katika kutangaza na kushuhudia Injili ya familia. Mabaraza ya Maaskofu yatoe nafasi kwa wataalam mbali mbali waweze kudadavua dhana ya ndoa na familia, ili waweze kukua na kukomaa katika safari yao: Wanandoa watarajiwa wasaidiwe kujiandaa kutangaza na kushuhudia Injili ya familia.

Baba Mtakatifu anasema: Elimu, malezi na makuzi ya watoto ni dhamana na wajibu unaopaswa kutekelezwa kwanza kabisa na wazazi. Familia ni kitovu cha elimu, maadili na utu wema. Watoto wafundishwe kweli za maisha ya kiroho; huruma, upendo na ukarimu! Familia ni hija yenye furaha, lakini kwa vijana wengi, familia imekuwa kana kwamba, ni chanzo cha “majanga katika maisha yao”! Ndoa kwa wengi sasa linaokena kana kwamba, ni jambo la mpito na kusahau kwamba, kwa njia ya Sakramenti ya Ndoa, mwanaume na mwanamke wanashirikishwa katika kazi ya uumbaji, malezi na makuzi ya watoto wao walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Leo hii watu wamekuwa na ufafanuzi mpana kuhusu “dhana ya familia”. Lakini, familia kadiri ya mpango wa Mungu ni muunganiko imara kati ya Bwana na Bibi, wanaoshirikishwa Fumbo kuu la uumbaji kama anavyokaza kusema Mtakatifu Paulo katika nyaraka zake. Ndoa ni Sakramenti kubwa na ni “Fumbo katika maisha ya binadamu”. Gharama za kufunga ndoa ni changamoto kubwa inayowaogopesha vijana wengi kuamua kufunga ndoa Kanisani na matokeo yake ni “uchumba sugu”. Hali ngumu ya uchumi, ukosefu wa fursa za ajira ni kati ya mambo ambayo yanaendelea kuchangia kuporomoka kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.

Utamaduni wa kifo unaingia kwa kasi kiasi kwamba, wanandoa wanachagua ni mtoto wa aina gani wampokee na kumtunza! Matokeo yake, watoto wengi wanatolewa mimba wangali tumboni mwa mama zao kutokana na ubinafsi: Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Baba Mtakatifu anaendelea kusema, kuna wanandoa ambao hata baada ya kuishi kwa pamoja kwa miaka mingi, lakini bado hawajabahatika kupata watoto.

Wanandoa katika hali na mazingira kama haya, wajitoe sadaka kutimiza mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Lakini kwa mshangao mkubwa, kuna watu ambao hawawapendi watoto hata kidogo, kiasi kwamba, upendo wao wanauhamishia kwa wanyama, kwani, wanaweza kuwajibika kadiri wanavyotaka wao. Mwelekeo huu ni tofauti kabisa kwa watoto kwani wao ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, wanandoa wawe na moyo wa shukrani kuwapokea, kuwalea na kuwatunza hata kama watakuwa na ulemavu, kwani kazi ya Mungu haina makosa! Baba Mtakatifu anasikitika kusema, kuna watoto wengi wanaokatishiwa maisha kutokana na ulemavu. Haya ni mauaji.

Baba Mtakatifu Francisko anazitaka familia kujenga na kukuza; kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Injili ya familia: Wawe na ujasiri wa kukoleza: furaha na upendo wa maisha ya ndoa na familia; kujenga na kudumisha uvumilivu, upole, msamaha na udumifu: Wanandoa watenge muda wa kutosha kukaa pamoja na familia zao, ili kufahamiana, kusaidiana na kutakatifuza katika hija ya utakatifu wa maisha. Ukosefu wa fursa za ajira ni changamoto kubwa kwa vijana wa kizazi kipya. Baba Mtakatifu anawataka waamini kujibidisha katika mchakato wa ukomavu. Wazazi na walezi watenge muda wa kukaa, kucheza na kuwasikiliza watoto wao. Nao watoto wawapende na kuwaheshimu wazazi wao waliojitaabisha kuwaleta hapa duniani hata bila ya ridhaa yao.

Papa: Jukwaa la Familia
27 December 2018, 10:28