Papa Francisko: Ijumaa ya Huruma ya Mungu, tarehe 7 Desemba 2018 awatembelea wagonjwa mjini Roma Papa Francisko: Ijumaa ya Huruma ya Mungu, tarehe 7 Desemba 2018 awatembelea wagonjwa mjini Roma 

Papa Francisko: Ijumaa ya huruma ya Mungu: Awatembelea wagonjwa!

Baba Mtakatifu akiwa ameandamana na Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la kuhamasisha Uinjilishaji mpya, ametembelea Kituo cha CasAmica pamoja na Kituo cha Tiba cha “Il Ponte e Albero”, vilivyoko kusini mwa Roma, ili kuwajulia hali vijana na wagonjwa wanaopata tiba kutoka katika vituo hivi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Huruma ya Mungu ni kiini cha Injili na njia muafaka ya uinjilishaji mpya, unaojikita katika mchakato wa ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kielelezo cha imani tendaji! Mwaka wa huruma ya Mungu ilikuwa ni fursa kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuchunguza dhamiri zao, ili kuangalia ikiwa kama maisha yao yanaendana na kweli za Kiinjili zinazotangazwa na kushuhudiwa na Mama Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu, alijiwekea utaratibu wa kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili katika maisha yake, dhamana ambayo anajitahidi kuiendeleza kila wakati anapopata fursa katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ijumaa, tarehe 7 Desemba 2018, Baba Mtakatifu akiwa ameandamana na Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la kuhamasisha Uinjilishaji mpya, ametembelea Kituo cha CasAmica pamoja na Kituo cha Tiba cha “Il Ponte e Albero”, vilivyoko kusini mwa Roma, ili kuwajulia hali vijana na wagonjwa wanaopata tiba kutoka katika vituo hivi.

Kituo cha CasAmica ni mahali ambapo wagonjwa wenye kipato cha chini kiuchumi wanaweza kupata tiba ya muda mrefu, huku wakiwa wanasindikizwa na ndugu zao. Hawa ni watu ambao wanakabiliwa na changamoto ya kupata mahitaji yao msingi kwa siku! Kumbe, Kituo cha CasAmonica ni kielelezo cha ushuhuda wa huruma ya Mungu inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu. Baba Mtakatifu amepata nafasi ya kuweza kusalimiana na wagonjwa, ndugu, jamaa na wahudumu wa Kituo hiki. Amesikiliza kwa makini simulizi za mateso na mahangaiko yao, akawapatia neno la faraja.

Dr.  Lucia Cagnacci Vedani amemtembeza Baba Mtakatifu sehemu mbali mbali za Kituo hiki ili kujionea mwenyewe hali halisi ya mateso na mahangaiko ya watu wa Mungu kutokana na magonjwa ya muda mrefu. Kabla ya kuondoka kituoni hapo, Baba Mtakatifu amewapatia zawadi na kumbu kumbu ya uwepo wake Kituoni hapo! Ikumbukwe kwamba, huruma ya Mungu inapaswa kuendelea kumwilishwa katika maisha ya watu sehemu mbali mbali za dunia, kama alama ya mwendelezo wa Mwaka wa Huruma ya Mungu uliotoa nafasi kwa waamini kuonja tena huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka katika maisha yao!

Baba Mtakatifu baadaye ametembelea Kituo cha “Il Ponte e Albelo”, hili ni kati ya maeneo ya Roma yanayoogelea katika dimbwi la umaskini mkubwa. Baba Mtakatifu amewatembelea vijana kumi na wawili, ambao miezi kadhaa iliyopita, walimwandikia barua kumwelezea matatizo, changamoto na matamanio yao halali kwa siku za usoni, kwa kuendelea kupata tiba mahali hapo. Walimwambia kwamba, walitamani walau siku moja, aende kuwatembelea na kuwafariji katika shida na mahangaiko yao kutokana na kuteteleka kwa afya ya akili. Baba Mtakatifu amekaa pamoja nao, akawasikiliza na kuwafariji katika shida na mahangaiko yao. Amejibu maswali kadhaa waliyomuuliza na hatimaye, wakamshukuru kwa kuwajali sanjari na kuonesha uwepo wa karibu kwa maskini na wale wote wanaoteseka.

Baba Mtakatifu pia amepata nafasi ya kumsikiliza Dr. Paolo Stievano, Mkuu wa Kitengo cha Saikolojia Kituoni hapo, aliyemsimulia matatizo makubwa wanayokabiliana nayo vijana hawa na jinsi ambavyo wanajitahidi kuwahudumia. Baba Mtakatifu amewapatia zawadi ya Noeli na hatimaye, akawabariki na kuondoka kurejea tena mjini Vatican kuendelea na shughuli zake.

Papa: Ijumaa ya Huruma ya Mungu

 

08 December 2018, 15:38