Tafuta

Vatican News
Papa Francisko ametembelea makao makuu ya gazeti la "Il Messaggero" Papa Francisko ametembelea makao makuu ya gazeti la "Il Messaggero"  

Papa Francisko atembelea makao makuu ya gazeti la "Il Messaggero"

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 8 Desemba 2018 alitembelea makao makuu ya gazeti la “Il Messaggero” linalochapishwa kila siku nchini Italia, kama sehemu ya kumbu kumbu ya maadhimisho ya Miaka 140 tangu kuanzishwa kwake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 8 Desemba 2018 ameadhimisha Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili,  kwa kutembelea na kusali kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu na kutoa heshima zake kwa Sanamu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili iliyoko kwenye Uwanja wa Spagna, mjini Roma. Katika sala yake kwa Bikira Maria amekazia: umuhimu wa viongozi waliopewa dhamana kutekeleza wajibu wao kwa: hekima, wakiwa na mwono mpana, moyo wa huduma na ushirikiano. Ameziweka familia zote zinazoogelea katika dimbwi la mahangaiko na shida mbali mbali chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, ili haki zao msingi ziweze kulindwa na kudumishwa na wote.

Baada ya shughuli zote, hizi, Baba Mtakatifu alitembelea makao makuu ya gazeti la “Il Messaggero” linalochapishwa kila siku nchini Italia, kama sehemu ya kumbu kumbu ya maadhimisho ya Miaka 140 tangu kuanzishwa kwake! Hili limekuwa ni tukio la kihistoria kwa wafanyakazi wa gazeti la “ Il Messaggero”, chini ya uongozi wa Azzurra Caltagirone, mwakilishi wa kampuni pamoja na Bwana Virman Cusenza, Mkurugenzi mkuu wa gazeti hili, ambalo linatoa ajira kwa wafanyakazi zaidi ya 200 walioshuhudia uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko mahali hapo!  Bwana Virman Cusenza anasema, uwepo wa Baba Mtakatifu kwenye Makao makuu ya gazeti lao ni ushuhuda unaofumbatwa katika uhuru wa habari mchanganyiko, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Papa Gazeti

 

10 December 2018, 09:09