Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Matukio ya Mwaka 2018 katika Mwanga wa Furaha ya Injili. Papa Francisko: Matukio ya Mwaka 2018 katika Mwanga wa Furaha ya Injili.  (Vatican Media)

Papa: Matukio ya Mwaka 2018: Furaha ya Injili!

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuhakikisha kwamba, furaha inayobubujika kutoka katika imani inaganga na kuponya madonda na changamoto za maisha na utume wa Kanisa, daima Kristo Yesu akipewa kipaumbele cha kwanza. Waamini wawe ni mashuhuda na vyombo vya Furaha ya Injili baada ya kukutana na Kristo Yesu katika: Neno, Sakramenti na Matendo ya huruma kwa jirani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika salam na matashi mema ya Sherehe za Noeli kwa mwaka huu 2018, alizozitoa kwa Sekretarieti kuu ya Vatican amesema, huu ni mwaka ambao Kanisa limetikiswa na misukosuko mikubwa, lakini bado linaendelea kuchanja mbuga kwa neema na huruma ya Mungu. Matukio ya Mwaka 2018 ambao umegota ukingoni yanapaswa kutazamwa kwa mwanga wa Waraka wa Kitume, “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” uliotolewa takribani miaka mitano iliyopita. Katika waraka huu wa kitume, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuhakikisha kwamba, furaha inayobubujika kutoka katika imani inaganga na kuponya madonda na changamoto za maisha na utume wa Kanisa, daima Kristo Yesu akipewa kipaumbele cha kwanza. Waamini wawe ni mashuhuda na vyombo vya kueneza Furaha ya Injili baada ya kukutana na Kristo Yesu katika: Neno lake, Sakramenti za Kanisa na matendo ya huruma kwa jirani.

Kwa wale wote wanaojiaminisha kwa Kristo Yesu Mkombozi wa ulimwengu anawaondolea kwanza kabisa mzigo wa dhambi, majonzi, utupu na upweke hasi, ili kuonja furaha ya Injili na kuwashirikisha wengine kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika imani iunayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili! Waamini wahakikishe kwamba, wanatumia vyema kipaji chao cha ugunduzi, tayari kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia upya wa Injili kama sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa katika mchakato mzima wa shughuli za kimisionari.

Lengo ni kuhakikisha kwamba, upendo wa Mungu unaookoa uliofunuliwa kwa njia ya Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu unawafikia na kuwaambata watu wa Mungu. Kwa bahati mbaya mkazo umewekwa zaidi kwa sheria, taratibu na kanuni za Kanisa na kusahau neema na huruma ya Mungu kwa waja wake; watu “wanachonga sana” kuhusu Kanisa na kumsahau Kristo Yesu, kichwa cha Fumbo la Mwili wake, yaani Kanisa; watu wengi wanajitaabisha sana kumzungumzia Khalifa wa Mtakatifu Petro na kusahau Neno la Mungu.

Baba Mtakatifu anataka kuona Kanisa ambalo liko wazi, linalojikita na kumwilisha Injili ya huduma ya upendo na ukarimu kwa watu wa Mungu, lakini zaidi kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, kiwe ni chakula kinachowatia waamini nguvu ya kusonga mbele kwa imani na matumaini. Kanisa halina budi kuthubutu kutoka nje na kujikita katika mambo msingi na vipaumbele vya maisha na utume wa Kanisa kwa kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu unaookoa, ili kuwapatia tena waamini fursa ya kujenga na kuimarisha uhusiano na mafungamano yao na Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali Rozari kwa ajili ya kuliombea Kanisa, ili kwa sala, maombezi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa, Mwenyezi Mungu aweze kulikinga Kanisa na mashambulizi dhidi ya Shetani anayetaka kupandikiza ndago za kashfa, chuki, uhasama na mipasuko, kiasi hata cha viongozi wa Kanisa kusaliti dhamana na uaminifu wao kwa Kristo na Kanisa lake. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Mama Kanisa ni Mtakatifu lakini kwa bahati mbaya, watoto wake ni wadhambi! Watoto wa Kanisa wanachangamotishwa kujikita katika mchakato wa: sala, toba na wongofu wa ndani, ili kupyaisha uso wa Kanisa kwa njia ya ushuhuda wa utakatifu wa maisha. Mwenyezi Mungu anaendelea kuzungumza na waja wake pamoja na kuliwezesha Kanisa kutekeleza dhamana na wajibu wake, ili kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha: maisha, utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Kanisa kwa kusoma alama za nyakati, limeendelea kuboresha Mapokeo na Mafundisho yake kadiri ya mwanga wa Roho Mtakatifu, kama ilivyojitokeza katika historia ya Kanisa kwa kipindi cha miaka 2,000 iliyopita! Kufutwa kwa adhabu ya kifo ni mwendelezo wa Mapokeo na Mafundisho yaliyotolewa na: Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, Yohane Paulo II na hata Mtakatifu Paulo VI katika nyaraka na kwa nyakati mbali mbali. Kwa mabadiliko haya, Baba Mtakatifu Francisko anataka kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu. Kama sehemu mwendelezo wa Mapokeo na Mafundisho hai ya Kanisa, Baba Mtakatifu Francisko ameridhia kwa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa kufanya marekebisho kwenye Katekisimu ya Kanisa Katoliki, kifungu namba 2267 kinachozungumzia kuhusu adhabu ya kifo na tafsiri mpya inapaswa kuingizwa katika vipengele mbali mbali vya Katekisimu ya Kanisa Katoliki. Kanisa Katoliki limefuta adhabu ya kifo katika Mafundisho na Mapokeo yake kwa kukazia: njia zinazotetea na kulinda maisha ya watu, amani na usalama wao dhidi ya adui; kwani hizi ni njia zinazodumisha utu, ustawi na mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, mwaka 2018 katika maisha na utume wa Kanisa, umegubikwa na mawimbi mazito ya kashfa na nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo! Kumwekuwepo na uchu wa mali, madaraka na utajiri wa haraka haraka, kiasi hata cha Kanisa kuonekana kana kwamba, limemezwa na malimwengu! Lakini, tangu sasa, Kanisa litaendelea kutekeleza dhamana na wajibu wake wa kimaadili katika misingi ya ukweli na uwazi, kwa kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia pamoja na kuwahudumia waathirika. Kila kiongozi atapaswa kuwajibika kadiri ya sheria, kanuni na taratibu za Kanisa na kwa nchi husika.

Baba Mtakatifu anasema, kuibuka na kuzagaa kwa kashfa ndani ya Kanisa ni kutokana na baadhi ya mihimili ya Kanisa kupoteza sifa na dhamana ya wito na utume wao kama maaskofu, mapadre na watawa! Huu ni wakati wa toba na wongofu wa ndani; fursa ya kwa mihimili ya uinjilishaji kujiandaa kikamilifu ili kukabiliana uso kwa uso na haki ya Mungu. Kwa sasa Kanisa linajiandaa kwa ajili ya mkutano maalum dhidi ya nyanyaso za kijinsia na utaongozwa na mambo makuu matatu: uwajibikaji, dhamana ya uwajibikaji; ukweli na uwazi. Hii mbinu mkakati wa kuwalinda watoto dhidi ya nyanyaso za kijinsia na unapania pia kuliwezesha Kanisa kujitakatifuza kwa kujikita katika maadili na utu wema, changamoto inayovaliwa njuga kwa wakati huu na Baba Mtakatifu Francisko, ambaye ameunda Kamati kuu itakayoratibu mkutano maalum utakaofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 21-24 Februari 2019.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa linaundwa na waamini watakatifu na wadhambi. Ndiyo maana katika Wosia wake wa Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo” anasema, Kristo Yesu anawaalika wote wanaoteseka au kudhulumiwa kwa ajili yake, kufurahi na kushangilia, kwani Yeye ni chemchemi ya maisha na furaha ya kweli. Lengo la Wosia huu ni mwaliko wa kuwa watakatifu katika ulimwengu mamboleo; kwa kutambua vizingiti, changamoto na fursa ambazo zinaweza kutumiwa na waamini kufikia utakatifu wa maisha. Kristo Yesu anawaalika waja wake ili wawe watakatifu, watu wasiokuwa na hatia mbele zake katika upendo. Mtakatifu Paulo VI na Askofu mkuu Osca Armulfo Romero ni kati ya umati mkubwa wa waamini watakatifu na wenyeheri waliotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko kwa mwaka 2018 kama mfano bora wa kuigwa katika huduma na utakatifu wa maisha! Baba Mtakatifu katika hija zake za kitume ndani na nje ya Vatican zimeendelea kuwa ni chachu ya imani, matumaini na mapendo kwa Kristo na Kanisa.

Katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya Miaka 70 ya Tamko la Haki Msingi za Binadamu mambo muhimu yanayopaswa kuzingatiwa: Utu na heshima ya binadamu; uhai unaopaswa kulindwa na kuendelezwa, sanjari na kujikita katika mchakato wa maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu: kiroho na kimwili. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuheshimu haki msingi za binadamu dhidi ya kile kinachodaiwa kuwa ni “Haki Mpya” ambazo zinasigana na tamaduni za watu. Baba Mtakatifu anawaalika wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa: haki msingi za binadamu na ushirikiano wa kimataifa. Maadhimisho ya kumbu kumbu ya Miaka 70 ya Tamko la Haki Msingi za Binadamu iwe ni fursa ya kuamsha dhamiri nyofu na kuendelea kujikita katika kulinda, kudumisha na kuendeleza utu na heshima ya binadamu!

Hivi karibuni, Vatican na China viliwekeana sahihi kuhusu uteuzi wa Maaskofu, mkataba ambao kimsingi ni wa shughuli za kichungaji, ili kuliwezesha Kanisa kutangaza na kushuhudia Furaha ya Injili kwa familia ya Mungu nchini China. Kanisa litaendelea kuwa ni sauti ya maskini na wanyonge sehemu mbali mbali za dunia; kwa kusimamia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; kwa kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu bila kusahau uhuru wa kidini. Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya mageuzi makubwa kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican anakazia dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa; umoja na mshikamano wa Maaskofu katika kuamua, kupanga na kutekekeza maamuzi mbali mbali pamoja na kuhakikisha kwamba, rasilimali fedha ya Kanisa inatumika katika shughuli za uinjilishaji wa kina ili kukidhi mahitaji ya mtu kiroho na kimwili. Fedha ya Kanisa itumike kwa kuzingatia misingi ya ukweli, uwazi, uaminifu na uadilifu kwa kuzingatia pia sheria, kanuni na taratibu za Kanisa.

Papa Francisko katika Barua yake Binafsi “Imparare a congedarsi” yaani “Kujifunza Kustaafu” anatoa wosia na sala kwa viongozi wa Kanisa kujiandaa vyema kung’atuka kutoka madarakani, kwa kutambua kwamba, hii pia ni sehemu ya huduma inayohitaji mfumo mpya wa uwepo na uwajibikaji. Haya ni maandalizi muhimu sana ya maisha ya ndani, kwani inawezekana kabisa kung’atuka kutoka madarakani kwa kigezo cha umri au pale ambapo Askofu anaombwa kuendelea na utume wake kwa muda mrefu kidogo, hata kama atakuwa ametimiza umri wa miaka 75, ambao kisheria: Maaskofu pamoja na wale walioteuliwa na Papa wanapaswa kuachia madaraka!

Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro amekazia zaidi huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake; changamoto na mwaliko kwa waamini kuendelea kujikita katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi; katika huruma na mapendo; kwa kudumisha na kukuza ari na mwamko wa shughuli za kimisionari; kwa kuheshimu utu na haki msingi za binadamu sanjari na kuendelea kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu na kwamba, huruma ya Mungu ni muhtasari wa historia nzima ya ukombozi wa mwanadamu!

Papa Francisko anawaalika waamini kujitambua kwamba wao ni wadhambi, wanapaswa kutubu na kumwongokea Mungu ili aweze kuwaonjesha huruma na upendo wake usiokuwa na kifani. Hii kimsingi ni neema ambayo waamini wanapaswa kuiomba kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa kutambua kwamba, huruma ya Mungu ni kubwa zaidi kuliko hata dhambi zinazotendwa na mwanadamu na kwamba,  msamaha wake ni dawa makini dhidi ya dhambi.  Mwenyezi Mungu kama ilivyokuwa kwa Baba mwenye huruma, daima anawasubiri watoto wake kukimbilia huruma, kwa njia ya toba. Kitendo cha mwamini kukimbilia kiti cha huruma ya Mungu kinaonesha toba ya ndani, sala inayopaswa kujikita katika unyenyekevu wa moyo badala ya litania ya maneno mengi.

Papa Francisko. Mwaka 2018
31 December 2018, 11:24