Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Tunzeni ardhi; lindeni na kuhifadhi vyanzo vya maji; na tumieni lishe bora na salama kwa maisha yenu! Papa Francisko: Tunzeni ardhi; lindeni na kuhifadhi vyanzo vya maji; na tumieni lishe bora na salama kwa maisha yenu! 

Papa Francisko: Tumieni vyema chakula, tunzeni ardhi na maji!

Papa Francisko anasema, kuna uhusiano wa karibu kati ya maji, kilimo na chakula; mambo yanayopaswa kutumiwa kwa moyo wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu, tayari kugawana na wengine kama kielelezo cha mshikamano wa upendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, tarehe 13 Desemba 2018 limeadhimisha warsha ya siku moja, ilioongozwa na kauli mbiu “Maji, Kilimo na Chakula: Tujenge ya Mbeleni”. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe uliosomwa kwa niaba yake na Monsinyo Fernando Chica Arellano, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye: Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, FAO, Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo wa Umoja wa Mataifa, IFAD pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, WFP., amekazia umuhimu wa mshikamano wa upendo.

Katika ujumbe wake, Baba Mtakatifu amewataka watu kuonesha mshikamano wa upendo na wale wanaoteseka kutokana na baa la njaa duniani, kama kielelezo cha utamaduni wa watu kukutana na kusaidiana, ili kujenga umoja na udugu. Watu wajifunze kutunza chakula na kugawana na maskini pamoja na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi” ili kuwajengea leo na kesho yenye matumaini. Warsha hii ambayo imefanyika huko Madrid, Hispania, imehudhuriwa na wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu nchini Hispania.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, ulimwengu mamboleo unakumbana na changamoto nyingi zinazoweza kupatiwa ufumbuzi kwa njia ya: umoja, ushirikiano na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa; kwa kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine, uchoyo na ubinafsi. Kuna uhusiano wa karibu kati ya maji, kilimo na chakula; mambo yanayopaswa kutumiwa kwa moyo wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu, tayari kugawana na wengine kama kielelezo cha mshikamano wa upendo.

Baba Mtakatifu anawataka washiriki wa warsha hii kuhakikisha kwamba, wanatoa kipaumbele cha kwanza kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, ili kujenga ya mbeleni. Jambo la msingi ni ushirikiano unaofumbatwa katika mshikamano unaoongozwa na kanuni auni; daima haki msingi za binadamu, utu, heshima na mahitaji yake msingi yakipewa kipaumbele cha kwanza. Kwa njia hii, hata vijana wa kizazi kipya, wataweza kupata rasilimali na utajiri wa mali ya asili kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao kwa siku za usoni, ili kupata maisha bora na kufurahia utimilifu wa maisha.

Baba Mtakatifu anaitaka familia ya Mungu kujikita katika kilimo bora, kwa kuibua, kupanga na kutekeleza sera na mikakati ya kilimo endelevu, kinachoheshimu na kutunza mazingira nyumba ya wote. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, sera na mikakati ya kiuchumi inakuwa ni shirikishi, ili kupambana na baa la njaa duniani, ambalo linaendelea kusababisha majanga makubwa kwa watu sehemu mbali mbali za dunia. Wakulima walinde na kuhifadhi mazingira! Athari za mabadiliko ya tabianchi ni kazi ya mikono ya wanadamu, kumbe, kuna haja ya kutunza vyanzo vya maji, ili kupata maji safi na salama kwa ajili ya afya bora; watu wajifunze kuhifadhi taka, ili kuepuka na uchafuzi mkubwa wa mazingira ambao ni chanzo kikuu cha umaskini, magonjwa na njaa duniani.

Wazazi na walezi, wawasaidie watoto na vijana wao kupata lishe bora; wawaelimishe ulaji bora na salama; watambue umuhimu wa chakula, tayari kujinasua na ulaji wa kupindukia, ili kweli chakula mezani iwe ni fursa ya watu kukutana na kujenga umoja na udugu; tayari kulinda na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote; inayotoa hifadhi kwa watu wote na kwamba, kilimo bora kijenga umoja, amani na mshikamano wa dhati!

Papa: Maji, Kilimo na Chakula
14 December 2018, 10:33